TANZANIA NA UINGEREZA KUKUTANA KUJADILI FURSA ZA BIASHARA NA UWEKEZAJI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, November 13, 2021

TANZANIA NA UINGEREZA KUKUTANA KUJADILI FURSA ZA BIASHARA NA UWEKEZAJI

 Balozi wa Uingereza nchini Tanzania David William Concar akizungumza na waandishi wa habari (hawamo pichani,) kuhusu kongamano hilo baina ya Uingereza na Tanzania na kusema kuwa uhusiano baina ya mataifa hayo mawili utadumishwa, leo jijini Dar ees Salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo akizungumza na waandishi wa habari (hawamo pichani,) juu ya kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza na kueleza kuwa kongamano hilo ni sehemu ya utekelezaji kwa vitendo wa dhamira ya Serikali ya kujipambanaua na kuitangaza nchi kama sehemu salama yenye mazingira bora ya uwekezaji, leo jijini Dar es Salaam.
* Mwakilishi wa Waziri Mkuu wa Uingereza kushiriki


* Waziri Mkumbo asema watakuza soko la Tanzania katika nchi za Umoja wa Ulaya


TANZANIA na Uingereza watakutana na kujadili fursa za kiuchumi kwa mataifa hayo mawili katika kongamano maalumu la Biashara na Uwekezaji litakalofanyika Novemba 16,2021 jijini Dar es Salaaam na kufunguliwa rasmi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na mjumbe maalumu wa masuala ya Biashara wa Waziri Mkuu wa Uingereza Lord John Walney ambaye ataambatana na wawakilishi wa kampuni 20 kutoka nchini Uingreza.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo amesema, kongamano hilo limeandaliwa kipekee ili kuongeza tija ya matokeo tarajiwa katika ukuaji wa uchumi na limebeba kauli mbiu ya '' Kuimarisha Ustawi Endelevu wa Uchumi kati ya Tanzania na Uingereza.''

''Kongamano limegawanyika katika makundi matatu yatakayofanya mijadala kwa wakati mmoja yaani, majadiliano kati ya Serikali ya Tanzania na Uingereza, majadiliano baina ya Sekta Binafsi ya Tanzana na Sekta Binafsi ya Uingereza pamoja na mdahalo kati ya Serikali na Sekta Binafsi....Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji,) Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania pamoja na Taasisi ya Sekta binafsi Tanzania (TPSF,) tumeratibu kongamano hili ili kutekeleza azma ya Serikali ya awamu ya sita katika msimamo wa kufungua zaidi fursa za kiuchumi ndani na nje ya nchi.'' Amesema.

Waziri Mkumbo amesema kongamono litahudhuriwa na washiriki wapatao 200 na wengine kushiriki kwa njia ya mtandao.

''Kongamano litatoa fursa kubwa ya kujadili kwa kina ushirikiano baina ya nchi hizi mbili hasa katika kupanua zaidi wigo wa uwekezaji hususan katika sekta za nishati, madini, miundombinu, kilimo, uchumi wa buluu na utalii, mkakati wa kupeleka bidhaa ya nyama nchini Uingereza upo na utasaidia kupanua soko katika nchi za umoja wa Ulaya ....pia tutajadili changamoto mbalimbali za kisera zilizokuwa zinawakabili wawekezaji wa Uingereza na zitapatiwa ufumbuzi.'' Amesema Mkumbo.

Aidha amesema, Tanzania na Uingereza zimekuwa na uhusiano wa karibu kwa muda mrefu na umekuwa ukiimarishwa kwa Serikali zake kukaa pamoja na kufanya mashauriano ya mara akwa mara na kueleza kuwa kongamano hilo litajadili na kuridhia mikakati ya pamoja ya itakayolenga kupunguza pengo la urari wa biashara na kukuza soko la mauzo katika nchi za Tanzania na Uingereza.

''Kwa mujibu wa takwimu za kituo cha Uwekezaji (TIC,) Uingereza ni nchi ya pili baada ya China kwa uwekezaji hapa nchini ikiwa na miradi ya takribani 945 yenye thamani ya dola za kimarekani 5.42 Bilioni na kutoa ajira takribani 275,384, na kwa mujibu wa takwimu za Serikali ya Uingereza jumla ya thamani ya biashara baina ya nchi hizi mbili kwa mwaka 2021 ni pauni za Uingereza 156 milioni huku Uingereza ikiuza hapa nchini bidhaa zenye thamani ya Pauni 127 milioni na Tanzania ikiuza Uingereza bidhaa zenye thamani yaa Pauni 29 milioni.'' Ameeleza.

Kwa upande wake Balozi wa Uingereza nchini Tanzania David William Concar amesema, uhusiano wa Uingereza na Tanzania ni imara na kupitia kongamono hilo fursa za kiuchumi zitakuwa nyingi zaidi hasa kwa wakati huu wa mlipuko wa janga la virusi vya UVIKO- 19 ambapo nchi nyingi zimekuwa zikitafuta nafasi ya kukuza uchumi ikiwemo Tanzania kupitia Serikali ya awamu ya sita ambayo imekuwa ikitoa kipaumbele katika ukuzaji wa uchumi.

Balozi Concar amesema, Lord Walney atakuja Tanzania kwa mara ya kwanza tangu apate nafasi hiyo Agosti 2021, na alipata fursa ya kukutana na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan nchini Uingereza Oktoba 31.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad