SOKO LA MADINI LASOGEZWA KWA WACHIMBAJI WADOGO KILINDI-BITEKO - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 23, 2021

SOKO LA MADINI LASOGEZWA KWA WACHIMBAJI WADOGO KILINDI-BITEKO

 Waziri wa Madini Doto Biteko akitoa maagizo kwa wachimbaji wadogo wa madini Kilindi katika Kata ya Kikunde kijiji cha Chamtui wilayani Kilindi mkoa wa Tanga.

Na, Mwandishi wetu, Tanga
WAZIRI wa Madini Doto Biteko amemuagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga ,Zabibu Napachu kuhakikisha Soko la Madini la Wilaya ya Kilindi linafunguliwa katika eneo la mgodi wa Seita ili wachimbaji wasisafiri umbali mrefu kwenda kuuza madini yao.

Waziri Biteko amesema hayo, alipotembelea mgodi wa Seita uliopo Kata ya Kikunde kijiji cha Chamtui wilayani Kilindi mkoa wa Tanga ambapo amekagua shughuli za uchimbaji madini na kuzungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika mgodi huo.

“Afisa Madini, ndani ya wiki moja kuanzia leo uhakikishe Soko la Madini la Wilaya ya Kilindi linafunguliwa katika eneo hili la wachimbaji na baada ya kufungua soko, asiruhusiwe mtu yoyote kusafirisha madini bila kupita Soko la Madini la Kilindi ili kudhibiti otoroshaji na kuisaidia Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi kupata mapato yake,” amesema Waziri Biteko.

Pia, Waziri Biteko amewataka wanunuzi wote wa madini (brokers) katika mgodi wa Seita kuhakikisha wananunua madini kwa bei elekezi ambayo inapangwa na Tume ya Madini kutokana na Soko la Dunia la siku husika.

Aidha, Waziri Biteko amesema kuna Sheria ya Ardhi na Sheria ya Madini, hizi ni Sheria mbili tofauti, kuna baadhi ya watu wanazichanganya hizi Sheria na wengine wanazani madini yakiwa kwenye ardhi yao basi madini hayo ni mali yao, hapana madini ni mali ya Serikali haruhusiwi mtu yoyote kuyachimba mpaka awe na leseni.

“Kiongozi na Msimamizi Mkuu wa Sekta ya Madini nchini ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan na sisi Wizara ya Madini ni wasaidizi wake,” amesema Waziri Biteko.

Waziri Biteko amesema Rais Samia Suluhu Hassan anataka awaone wachimbaji wadogo wanatajirika kupitia shughuli zao za uchimbaji na wanashiriki kikamilifu katika uchumi wa madini ambapo anataka aone utulivu kwenye ya uchimbaji wa madini.

Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Aberi Busalama amesema wilaya yake haijanufaika ipasanyo na uwepo wa madini wilayani humo kwa sababu ya kukosekana kwa soko la kuuzia madini katika wilaya hiyo ambapo madini yanayopatikana hupelekwa kuuzwa wilaya jirani ya Handeni, hivyo kukosa mapato yatokanayo na madini na kuchochea utoroshwaji wa Madini.

Pamoja na mambo mengine, Busalama amemuomba Waziri Biteko kupeleka Afisa Migodi Mkazi katika wilaya ya Kilindi ili awasaidie wachimbaji wadogo mbinu bora za uchimbaji na kutoa elimu juu ya utunzaji wa mazingira na uchimbaji salama pamoja na kudhibiti utoroshaji wa madini wilayani humo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad