MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KUWA SULUHISHO LA UHARIBIFU WA MAZINGIRA-MAKAMBA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 17, 2021

MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KUWA SULUHISHO LA UHARIBIFU WA MAZINGIRA-MAKAMBA

 Hafsa Omar-Dar es Saalam

WAZIRI wa Nishati, January Makamba amesema kuwa mradi wa kuboresha njia endelevu za matumizi ya Nishati safi ya kupikia utasaidia kulinda mazingira na itakuwa suluhisho la uharibifu wa Mazingira hapa nchini.

Ameyasema hayo, Novemba 17, 2021 wakati akiwa na kikao na Balozi wa Umoja wa Ulaya kilichofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati, zilizopo Jijini Dar es Saalam.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Felchesmi Mramba, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio na watalaamu kutoka Wizara ya Nishati na timu kutoka katika Ubalozi wa Umoja wa Ulaya hapa nchini.

Akizungumza na Balozi huyu, aliupongeza ubalozi huo kwa kazi nzuri ya kuandaa miradi ya Nishati jadidifu ambayo itatoa suluhuhisho la uharibifu wa mazingira na kuwatoa watanzania kwenye matumizi ya mkaa na kuni.

Ubalozi huo unatarajia kuzindua mradi wa kuboresha njia endelevu za matumizi ya Nishati safi ya kupikia hivi karibuni ambao utagharimu Euro milioni 30 ambao utaanza kuzinduliwa katika maeneo ya mjini.

“Nawaahidi nitakuwa na nyie bega kwa bega kuhakikisha mnafanikiwa katika mradi huo muhimu kwa Taifa letu kwasababu njia peke ya kumaliza matumizi ya mkaa ni Gesi ya kwenye mitungi ( Liquefied Petroleum Gas -LPG),” alisisitiza Makamba.

Aidha, alisema Serikali itahakikisha inatoa ushirikiano kwa Ubalozi huo ili waweze kufanikisha kwa urahisi miradi yote ya Nishati inayokusudiwa kutekelezwa hapa nchini.

Kwa upande wake, Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) hapa nchini, Manfredo Fanti, amesema kuwa wataendelea kufanya kazi na Serikali ya Tanzania na wapo tayari kuzindua miradi hiyo hivi karibuni.

Alisema, Dhumuni la kubuni mradi hiyo ni kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na kuongeza kasi ya matumizi ya Nishati jadidifu katika mikoa ya Dar es Saalam, Morogoro, Pwani na kuendelea na maeneo mengine hapa nchini.
Waziri wa Nishati, January Makamba (kulia) akizungumza na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) hapa nchini, Manfredo Fanti, wakati alipokuwa na kikao na balozi huyo katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati zilizopo jijini Dar es Saalam, Novemba 17, 2021.

Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Felchesmi Mramba (kwanza-kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), James Mataragio (katikati) Katibu wa Waziri, Danford Mpelumbe, wakimsikiliza Waziri wa Nishati, January Makamba (hayupo pichani) wakati wa kikao na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) hapa nchini, kilichofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati zilizopo jijini Dar es Saalam, Novemba 17, 2021.
Picha mbalimbali wakati wa kikao cha Waziri wa Nishati, January Makamba na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) hapa nchini kilichofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati zilizopo jijini Dar es Saalam, Novemba 17, 2021.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad