BITEKO- WAJUMBE KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI WAPATIWA MAFUNZO JUU YA MIRADI INAYOTEKELEZWA NA SEKTA YA MADINI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 8, 2021

BITEKO- WAJUMBE KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI WAPATIWA MAFUNZO JUU YA MIRADI INAYOTEKELEZWA NA SEKTA YA MADINI

 

Na Mwandishi wetu
IMEELEZWA kuwa Katika kuwajengea uelewa wananchi, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeandaa semina elekezi juu ya uanzishwaji wa Vituo vya Mfano vya Katente na Lwamgasa pamoja na miradi mipya ya uchimbaji mkubwa wa madini kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini.

Lengo ni kuwa chachu ya kuwahabarisha wabunge wengine na baadaye wabunge kutoa elimu hiyo kwa wananchi ili kama nchi kuwa na uelewa juu ya masuala mtambuka yanayosimamiwa na Wizara ya Madini.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini na viongozi wengine wa Wizara waliohudhuria semina hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ofisi ndogo zilizopo GST mjini Dodoma.

Alisema ujenzi wa vituo hivyo uliwezeshwa kwa fedha kutoka Benki ya Dunia ujenzi wa vituo vya mfano vilivyojengwa ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kutoka katika uchimbaji duni na kuchimba kwa teknolojia rahisi na bora ili waweze kuchimba kwa tija pia semina hiyo imegusia eneo la leseni ya uchimbaji mkubwa ya Tembo Nickel Corporation iliyotolewa hivi karibuni ili kuwafahaisha wabunge matarajio ya uchimbaji huo pamoja na changamoto zinazoambatana nayo.

Alisema kufuatia maelekezo yanayotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuifungua sekta ili watu wengi zaidi waweze kushiriki katika kuwekeza kwenye Sekta ya Madini. Waziri Biteko alisema hivi sasa Serikali inakwenda kutoa leseni tatu (3) za uchimbaji mkubwa wa madini ambazo hazijatolewa kwa miaka 15 iliyopita ikiwa ni pamoja na kufufua miradi iliyokuwa imesimama kwa muda mrefu kama ule wa Buckreef kuanza uzalishaji.

Aidha,Waziri Biteko aliwashukuru wajumbe wa Kamati hiyo kwa michango na maelekezo yao na kuahidi kufanyia kazi maelekezo na maoni waliyotoa yenye lengo la kuifanya Sekta ya Madini kujiendesha kwa tija.

Akiwasilisha mada juu ya uanzishwaji wa vituo vya mfano vya Katente na Lwamgasa Mhandisi Moses Kongola alisema vituo hivyo vilianzishwa kwa lengo la kuwawezesha wachimbaji kuchimba kwa kutumia teknolojia sahihi na ya kati yenye urahisi katika kuitumia huku ikihusisha gharama nafuu.

Alibainisha kuwa uanzishwaji wa vituo hivyo utawasaidia wachimbaji wadogo kuongeza uzalishaji wa madini na mapato, kupata maarifa na ujuzi, utahamasisha afya na usalama migodini pamoja na kupunguza athari za kijamii na mazingira wakati wa shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba akiwasilisha mada juu ya miradi ya uchimbaji mkubwa wa madini alisema ili mradi ujulikane kama ni uchimbaji mkubwa lazima uhusishe umiliki wa leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini ambayo uwekezaji wake unaanzia Dola za Marekani milioni 100.

Aidha, mhandisi Samamba alibainisha kuwa mradi wa uchimbaji Mkubwa wa Madini ya Nickel unamilikiwa na Kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited (TNCL) kwa ubia kati ya kampuni ya Kabanga Nickel Limited (KNL) ya nchini Uingereza na Serikali ya Tanzania kupitia Msajili wa Serikali.

Alisema utekelezaji wa mradi huo utafanyika katika eneo la Kabanga wilaya ya Ngara mkoani Kagera ambapo uhai wa mgodi huo ni miaka 33 utakao iletea serikali mapato ya kiasi cha dola za Marekani 7,543,065,250 sawa na shilingi za kitanzania trilioni 17.35 kwa kipindi chote cha uzalishaji.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na Mbunge wa Jimbo la Manonga, Seif Gulamali alizungumza kwa niaba ya wajumbe wa kamati hiyo aliitaka Wizara ya Madini kuhakikisa inashughulikia vibali vyote vitakavyohitajika na kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa mradi huo ili kusiwe na mkwamo wowote na hivyo kupelekea mradi kukamilika na kuanza uzalishaji kwa wakati.

Akitoa maelekezo juu ya usimamizi wa Vituo vya Mfano vilivyojengwa kwa fedha zilizotolewa na Benki ya Dunia vya Katente na Lwamgasa, Gulamali aliagiza miradi hiyo iwe na matokeo chanya kwa maana ya kuwa na faida kwa taifa na faida kwa wananchi wanaonufaika na miradi hiyo ili uwekezaji uliofanywa katika maeneo hayo uwe na tija.

Kwa upande wake, Mbunge wa Ngara, Ndaisaba George alisema wananchi wa Jimbo la Ngara, kata na vijiji vinavyozunguka mradi huo wameupokea vizuri mradi wa uchimbaji wa madini ya nickel na wapo tayari kufuata maelekezo ya serikali ili waweze kupisha mradi mara baada ya fidia kulipwa na kupewa maeneo watakayopaswa kuhamia.

Alibainisha kuwa, kiasi cha dola za Marekani milioni 59 zimetengwa kwa ajili ya kulipa fidia wananchi wa eneo hilo wanaotarajia kuachia maeneo yao mara tu ya fedha hizo kulipwa kwa wananchi na kuwezesha mradi kuendelea pasipokuwa na migogoro yeyote wakati wa utekelezaji wake.

Mafuzo kama haya yanalenga kuongeza uelewa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini inayoisimamia Wizara ya Madini juu ya kazi zinazotekelezwa na wizara na kuwaongezea wajumbe wa kamati uwanja mpana wa uelewa juu ya miradi inayosimamiwa na wizara.No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad