HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 29, 2021

Wizara ya Maliasili na Utalii kuja na mkakati,kufufua utalii Njombe

 Na Amiri Kilagalila,Njombe

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dkt.Damas Ndumbaro amesema wizara hiyo inatarajia kuandaa mpango mkakati ili kufufua utalii katika mkoa wa Njombe kutokana na mkoa huo kuwa nyuma ili hali umekuwa na aina nyingi za utalii.

Waziri Ndumbaro amebainisha hayo wakati akizungumza na baadhi ya viongozi pamoja na mkuu wa mkoa wa Njombe alipofika mkoani hapo kwa ajili ya ziara ya kikazi.

“Kutokana na upekee wa mkoa huu yaani tunapata aina 6 za utalii katika mkoa huu lazima tuje na mpango mkakati wa kufufua utalii wa mkoa wa Njombe” alisema Dkt.Damas Ndumbaro

Ndumbaro amesema vivutio vilivyopo mkoani Njombe ni pamoja na utalii wa mali kale (majumba na makanisa), Hifadhi ya taifa ya kipekee (Kitulo),Misitu,Kilimo,Fukwe na hata utamaduni kwa hiyo ni lazima wizara kuja na mpango huku pia akisikitishwa kuona mkoa huo umekosa afisa utalii.

“Mkoa wa Njombe ni wa kitalii lakini nimesikitika kuona hakuna afisa wa utalii hata mmoja nimesikitika sana.Mikoa mingine inasifika sana kwa utalii lakini hawana rasilimali na vivutio ambavyo Njombe vipo”aliongeza Dkt.Damas Ndumbaro

Vile vile amesema wizara itaendelea kuboresha utalii wa michezo nchini na kubainisha kuwa mkoa wa Njombe ni miongoni mwa mikoa michache michache nchini yenye viwanja vya gofu hatua inayowalazimu kukuza mchezo huo.

“Njombe ni kati ya mikoa michache ambayo ina viwanja vya Gofu,tuna kiwanja hapa cha mashimo tisa.Lile eneo (Kibena Club) wawekezaji wameshaanza kulivuruga ninaomba tuwaambie tuliwakaribisha kuwekeza na sio kuvuruga mipango ya eneo lile” alisema Dkt.Damas Ndumbaro

Ameongeza kuwa “Ninaomba Mh,RC kwasababu tunahamasisha utalii wa gofu na utalii wa michezo na tumepanga kuzunguka na mashindano nchi nzima,ule uwanja ni vizuri ufufuliwe nitakacho kusaidia ni kutuma chama cha gofu ili kukagua eneo lile na kama kuna mtu alivamia apishe tu”alisema Ndumbaro.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Njombe Mhandisi Marwa Rubirya amekiri kuwepo na vivutio vingi katika mkoa huo.

“Moja ambalo halizungumzwi ni asili ya Njombe ambapo ukifika pale Mdandu utaona kama kuna kitu tunataka kukipoteza,lakini kuna eneo linguine kule kwenye jiwe lenye ramani ya Afrika kwa hiyo kwa kwli vipo vivutio vingi ambavyo tuna kila sababu ya kuhakikisha tuna vitangaza”alisema Rubirya

Awali katibu tawala wa mkoa wa Njombe Bi,Judica Omary amesema licha ya mkoa huo kuwa na vivutio vingi lakini wamekuwa na uhaba wa watumishi pamoja na vyombo vya usafiri hali inayorudisha nyuma jitihada za utalii na kuiomba wizara kuwasaidia kutatua changamoto hizo.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt,Damas Ndumbaro akieleza mikakati ya wizara katika kukuza sekta ya utalii mkoani Njombe alipofika kwa ajili ya ziara ya kikazi mkoani humo.
Baadhi ya watumishi wa mkoa wa Njombe wakimsikiliza waziri wa Maliasili na Utalii alipofika mkoani humo kwa ajili ya ziara.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad