HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 15, 2021

WAZIRI MKENDA AWATAKA WANACHAMA WA VYAMA VYA USHIRIKA WA AKIBA NA MIKOPO KUTIMIZA WAJIBU WAO KUPATA VIONGOZI BORA

 Wito umetolewa kwa wanachama wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kuwa wasimamizi na wafuatiliaji wa mali Pamoja na uendeshaji wa shughuli za vyama vyao vya Ushirika ili kuongeza tija na ukuaji ya Vyama vya Ushirika nchini.

Hayo yamesemwa kupitia Hotuba ya Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Aldolf Mkenda iliyosomwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) Prof. Alfred Sife wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo Duniani (ICUD) 14 Oktoba, 2021, yaliyofanyika mkoani Morogoro

Katika hotuba hiyo Waziri amewataka wanachama kutimiza wajibu wao kwa kushiriki kupata viongozi bora wa vyama, kutoa huduma zenye ubunifu na uadilifu katika utendaji. Aidha, amewataka wanaushirika kuwa makini katika uwekezaji bora wa rasilimali za vyama vyao vya ushirika. Hivyo, Serikali itaendelea kuwaunga mkono.

“Serikali kwa kutambua umuhimu wa Sekta ya Ushirika hasa Ushirika wa kifedha imekuwa ikichangia maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, niwahakikishie kuwa tutasimamia ushirika kwa kuzingatia Sheria na kuhakikisha kuwa hautetereki,” alisema Prof. Sife

Sambamba na hilo Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege amewataka wanachama wa vyama vya Ushirika kufuatilia utendaji wa vyama vyao ili kuhakikisha usimamizi unaimarika katika vyama na Hati safi za ukaguzi zinaongezeka

“Mtu wa kwanza wa kuhakikisha chama kinapata hati safi ni mwanachama wa chama cha ushirika kwa kufika kwenye mikutano inapoitishwa, kushiriki kwenye maamuzi yenye maslahi kwa chama ni lazima tubadilike na kusimamia mali zetu nguvu ya ushirika lazima ianzie kwa wanachama wenyewe,” alisema Mrajis

Aidha, Mrajis amesema ni wakati sahihi sasa kwa vyama vya Ushirika wa mazao kuwa na vyama vya Akiba na Mikopo ili kuongeza mzunguko wa fedha kwa wakulima hasa kuwawezesha kumudu gharama mbalimbali za kilimo wakati wa misimu ya mazao.

Dkt. Ndiege ameongeza kwa kutoa rai kwa vyama ambavyo bado havijaomba Leseni za uendeshaji wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo kwa mujibu wa Sheria Na.10 ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 kufanya hivyo ili kuendana na matakwa ya Sheria, Kanuni na Taratibu zinazolenga kuongeza ufanisi wa vyama.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (SCCULT) Dkt. Gervas Machimu ameeleza lengo la maadhimisho hayo ni kuwaenzi na kukumbuka mchango wa waasisi wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo, wanaushirika kukaa pamoja kubadilisha uzoefu na kutathmini mchango wa SACCOS katika maendeleo ya nchi.

Akieleza baadhi ya changamoto zinazokabili Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo amesema bado vyama hivyo vinakabiliwa na changamoto katika ukokotoaji wa gharama za malipo ya kodi, ugumu wa kupata tafsiri za kisheria za Ushirika hasa katika utatuzi wa migogoro wa kesi za ushirika ili kufikia muafaka na utatuzi kufikiwa kwa haraka.

Mwenyekiti huyo ameshauri kuwa vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo kuendelea kushiriki katika michakato ya mabadiliko ya Sheria Pamoja na mapitio mengine ya maboresho na mabadiliko ya mifumo ya Ushirika hapa nchini.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Ushirika Moshi (MoCU) Prof. Alfred Sife akikabidhi tuzo kwa Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Arusha Emmanuel Sanka kwa niaba ya Chama Bora cha Ushirika chenye Leseni daraja A, Arusha Teachers saccos wakati wa Kilele cha maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Ushirika wa Akiba na Mikopo, Mkoani Morogoro.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Dkt.Christine Ishengoma akitoa salamu za kamati wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Ushirika wa Akiba na Mikopo (ICUD), Mkoani Morogoro

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akielezea suala la Ushirika wakati wa Kilele cha maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Ushirika wa Akiba na Mikopo, Mkoani Morogoro

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad