MAMLAKA ya Hali ya hewa Tanzania (TMA) imesema Upungufu wa Mvua unatarajiwa kujitokeza kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa Mvua kwa mwaka unaoanza mwezi Novemba 2021 hadi Aprili 2022.
Imeelezwa kuwa mvua hizo zinatarajiwa kuwa chache
yaani za chini ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya kigoma,
Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya na Iringa huku kwa mikoa
ya Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara na kusini mwa mkoa wa Morogoro mvua zikitarajiwa
kuwa wastani hadi chini ya wastani.
Mkurugenzi wa TMA, Dkt Agnes Kijazi ameyasema hayo leo
Oktoba 27, 2021 jijini Dar es salaam wakati akitoa utabiri wa hali ya hewa kwa waandishi
wa habari.
Amesema kuwa vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa
kuwa kati ya mwezi Novemba 2021, na Januari 2022 huku Ongezeko la kidogo la mvua
likitarajiwa Machi 2022.
Amesema kuwa Mvua katika maeneo mengi zinatarajiwa kuanza kunyesha katika wiki ya
tatu ya mwezi Novemba 2021, na kuisha kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi
Aprili 2022.
Kufuatia hali hiyo ya mvua chache Dkt Kijazi amezitaja
athari zinazoweza kujitokeza ni pamoja na upungufu wa unyevunyevu katika udongo
unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi yanayopata mvua za msimu na kuathiri
ukuaji wa mazao.
Aidha Mkurugenzi huyo amesema kina cha maji katika
mito mabwawa na hifadhi za maji ardhini kinatarajiwa kupungua hususani katika
maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani huku mlipuko wa Magonjwa
ukitarajiwa kujitokeza kutokana na upungufu wa upatikanaji wa maji safi na salama.
Amesema Mwelekeo huo unaonesha kuchangiwa na Joto la
Bahari Katika Vyanzo hivyo Vya Mvua kwa nchi ya Tanzania kuwa la Wastani.
Pia ushauri na tahadhari zimetolewa kwa wadau wa
sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa
majukumu yao kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi,
maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, usafirishaji (nchi kavu,
kwenye maji na angani), mamlaka za miji, afya, sekta binafsi pamoja na
menejimenti za maafa.
Mvua za Msimu ni mahususi katika maeneo ya magharibi
mwa nchi, kanda ya kati, nyanda za juu
kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo
ya kusini mwa mkoa wa Morogoro. Maeneo
haya yanapata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, unaoanza mwezi Novemba na kuisha
kati ya mwezi Aprili na Mei ya mwaka unaofuata.
Kutokana na mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa mvua
za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya mikoa ya
Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya na Iringa.
Aidha, mvua za wastani hadi chini ya
wastani zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara na kusini mwa Morogoro.
Katika nusu ya kwanza ya msimu (Novemba - Januari) vipindi virefu vya ukavu
vinatarajiwa. Hata hivyo, ongezeko kidogo la
mvua linatarajiwa mwezi Machi, 2022 katika nusu ya pili ya msimu.
Mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa
katika mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi. Mvua hizo zinatarajiwa kuanza katika
wiki ya tatu ya mwezi Novemba, 2021 katika
maeneo mengi. Mvua hizo zinatarajiwa kuisha wiki ya pili ya mwezi
Aprili, 2022 katika mkoa wa Katavi na
wiki ya tatu ya mwezi Aprili, 2022 katika maeneo mengine yaliyosalia.
Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuwa za chini
ya wastani hadi wastani na zinatarajiwa
kuanza kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Disemba, 2021. Mvua zinatarajiwa kuisha wiki ya tatu ya mwezi
Aprili, 2022. Nyanda za juu kusini magharibi (Mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya,
Iringa, Njombe, pamoja na maeneo ya
kusini mwa mkoa wa Morogoro):
Mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa
katika maeneo ya mikoa ya Rukwa, Iringa, Songwe na Mbeya.
Aidha, mvua za wastani hadi chini ya wastani
zinatarajiwa katika mikoa ya Njombe, kusini mwa Morogoro na maeneo ya miinuko
ya mkoa wa Mbeya. Mvua katika maeneo
haya zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Novemba, 2021
na kuisha katika wiki ya tatu ya mwezi Aprili, 2022. Hata hivyo, maeneo ya
kusini mwa mkoa wa Morogoro mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili ya mwezi
Novemba, 2021 na kuisha wiki ya kwanza
ya mwezi Aprili, 2022.
Pwani ya kusini na maeneo ya kusini mwa nchi (Mikoa
ya Lindi, Mtwara na Ruvuma): Mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa
katika maeneo ya mikoa ya Lindi, Mtwara
na Ruvuma. Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili ya mwezi Novemba, 2021
katika mikoa ya Lindi na Mtwara na wiki
ya tatu ya mwezi Novemba, 2021 katika mkoa wa
Ruvuma. Mvua zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Machi, 2022
katika mkoa wa Ruvuma na wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2022 katika mikoa ya
Lindi na Mtwara.
Aidha, upo uwezekano wa kutokea kwa mgandamizo mdogo
wa hewa kaskazini mashariki mwa kisiwa cha Madagascar, hivyo kusababisha
kurejea kwa mvua katika baadhi ya maeneo
mwishoni mwa mwezi, Aprili, 2022.
TMA inawashauri wakulima kupanda mazao na mbegu
zinazokomaa ndani ya muda mfupi na
zinazostahimili mvua chache kama vile mazao jamii ya mizizi na mazao ya
bustani huku wakishauriwa kutumia mbinu na teknolojia za kilimo himilivu za
kuhifadhi maji na unyevunyevu wa udongo.
“Wakulima wazingatie kupata ushauri kutoka kwa
maafisa ugani juu ya namna bora ya
kuendesha kilimo kwa usalama wa chakula na lishe huku mamlaka husika zikishauriwa
kutoa elimu na ushauri kwa wakulima juu ya njia bora na namna ya kutumia kiwango kidogo cha mvua
kinachotarajiwa pamoja na matumizi mazuri ya
akiba ya chakula kilichopo..
Aidha mamlaka imesema sekta za usafirishaji hususan
usafiri wa ardhini, anga na kwenye maji zinaweza kunufaika kutokana na vipindi vya ukavu vinavyoweza
kujitokeza.
Hata hivyo, mamlaka ya Hali ya Hewa I imewashauri wadau
kuwasiliana na Mamlaka ili kupata taarifa mahsusi za utabiri wa msimu ili kukidhi mahitaji maalum katika sekta zao.
No comments:
Post a Comment