HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 12, 2021

TANZANIA YAPONGEZWA KUFANIKISHA MAONESHO YA UTALII UKANDA WA AFRIKA MASHARIKI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro wakifungua na kuweka jiwe la msingi la kwanza la maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki, leo Jijini Arusha. Na Mwandishi Wetu, Arusha

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepongezwa kwa kufanikisha maonsho ya kwanza ya kitaifa ya kikanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Jijini Arusha kuanzia tarehe 9 – 11 yaliyolenga kutangaza vivutio na fursa mbalimbali za utalii ndani ya Jumuiya hiyo.

Pongezi hizo zimetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na baadhi ya Mawaziri wa Utalii wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati wa kufunga maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki leo jijini Arusha.

“Nawapongeza kwa kufanikisha maonesho haya ni imani yangu kuwa kupitia maonesho haya nchi zetu za ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimepata fursa ya kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii pamoja na kujadili njia mbalimbali za kukabiliana changamoto zinazoikabili sekta ya Utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki,” Amesema Dkt. Mwinyi

“Natoa wito kupitia maonesho haya ambayo yatakuwa yanafanyika kila mwaka kwa mzunguko kwa kila nchi mwanachama……..jitihada zaidi zinahitajika katika kutangaza vivutio vya utalii katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na kuboresha sera zetu za utalii,” ameongeza Dkt. Mwinyi

Dkt. Mwinyi pia ameitaka Kamati Maalumu ya Kikanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya ziara Zanzibar na kujionea fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya utalii pamoja na zile za biashara na uwekezaji.

Awali Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema kupitia maonesho haya ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki yamekuwa na mafanikio makubwa ambapo zaidi ya waoneshaji 100 kutoka mataifa mbalimbali duniani wameshiriki, kati yao 41 wakitoka mataifa mbalimbali na nchi 25 zikishiriki ikiwa ni pamoja na sita za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Nae Waziri wa Uhifadhi wa Wanyamapori na Utalii kutoka Sudan ya Kusini Mhe. Luteni Jenerali Rizik Zakaria Hassan ameipongeza Tanzania kwa kufanikisha maonesho ambayo yemeweza kuvitangaza vivutio mbalimbali vya utalii ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki ambayo pia yametoa fursa ya kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya utalii.

“Maonesho haya yemekuwa na manufaa makubwa sana kwa kutuweka sekta ya utalii ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki ……….binafsi nawapongeza sana Tanzania kwa kulifanikisha jambo hili muhimu kwetu, naamini kupitia maonesho haya tutazidi kuimarika ziadi kama jumuiya kwa maendeleo yetu sote,” Amesema Luteni Jenerali Hassan.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Forodha na Biashara Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bwn. Keneth Bagamuhunda ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Peter Mathuki, amesema maonesho yalilenga kutoa fursa kwa kila nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii ili kuifahamisha Afrika na Dunia kuwa ndani ya Afrika Mashariki kuna vivutio vya utalii.

“Tutaendelea na maonesho haya kwa kila mwaka lengo likiwa ni kutangaza utalii na kuhakikisha soko la utalii ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki linakuwa kila mwaka,” Amesema Bwn. Bagamuhanda.

Kwa upande wake, Waziri wa Utalii na Malikale wa Zanzibar, Mhe. Leila Mohamed Mussa (Mb) amesema Afrika kwa sasa inatakiwa fursa za utalii na biashara ili kuweza kuziongezea Serikali zetu mapato.

“Afrika Mashariki inayo mambo mengi ya kutoa katika bara la Afrika na Duniani kwa ujumla hasa katika sekta ya utalii kwa kuwa tumejaliwa vivutio mbalimbali vya utalii,” amesema Bibi Leila Mohamed Mussa.

Oktoba 09, 2021 maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki yalizinduliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki jijini Arusha.

Kufanyika kwa maonesho hayo kunatokana na kuzinduliwa hivi karibuni mpango wa pamoja kutangaza utalii katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki uliozinduliwa rasmi na Mawaziri wa Maliasili na Utalii wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Maonesho hayo yalihudhuriwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania (Mwenyeji), Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akihutubia washiriki wa maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki, leo Jijini Arusha.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akipata maelezo wakati alipotembelea banda la Rwanda katika maonesho ya kwanza ya Kikanda ya Utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki leo Jijini Arusha.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akikaribishwa na Balozi wa Kenya nchini Tanzania katika banda la Kenya wakati alipokuwa akitembelea mabanda mbalimbali katika maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki, leo Jijini Arusha.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Mkewe Mhe. Mama Mariam Mwinyi na viongozi mbalimbali katika banda la Zanzibar leo Jijini Arusha.
Kikundi cha ngoma kutoka Makumira Arusha kikitumbuiza wakati wa maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki leo Jijini Arusha.
Kikundi cha ngoma kutoka Sudan Kusini kikitumbuiza wakati wa maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki leo Jijini Arusha.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali mara baada ya kufunga maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki leo Jijini Arusha.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad