HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 21, 2021

MKOA WA RUVUMA WAPOKEA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 12 ZA COVID-19

  Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Julius Mtatiro, akiongea jambo jana katika kikao kazi cha maendeleo juu ya fedha za Covid-19 kilichofanyika jana katika Ukumbi wa Manispaa ya Songea .

Baadhi ya Wataalam mbalimbali wa Halmashauri za Wilaya wakifuatilia Hotuba ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge(hayupo pichani)wakati wa kikao kazi za kupitia taarifa za maendeleo ya fedha za Covid-19 katika Ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya za mkoa wa Ruvuma wakimsikiliza Mkuu wa mkoa wa Ruvuma katika kikao kazi za kujadili na kupitia taarifa za maendeleo ya fedha za Covid-19 katika Ukumbi wa Manispaa ya Songea

Na Muhidin Amri, Songea
MKOA wa Ruvuma umepokea jumla ya Sh. bilioni 12.7 sawa na asilimia 2.4 ya Sh. bilioni 635.68 ambazo Ofisi ya Rais Tamisemi imeidhimishiwa kwa ajili ya uboreshaji wa sekya ya Afya,Elimu na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, amesema hayo wakati akifungua kikao kazi cha maandalizi ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya COVID-19 kilichofanyika mjini Songea.

Amesema,matumizi ya fedha hizo yameelekezwa kwenye maeneo ya vipaumbele yanayogusa wananchi moja kwa moja ili kuwaondolea kero katika kuzifikia na kuzipata huduma za afya,elimu na uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa COVID-19.

Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kutokana na jitihada zaze za kupambana na ugonjwa wa COVID-19 zilizowezesha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata mkopo wenye masharti nafuu kutoka Shirika la fedha la Kimataifa(IMF).

Amesema, fedha hizo ni kwa ajili ya kampeni ya Maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya COVID-19 lengo likiwa kufufua uchumi katika sekta zilizopata athari hasi za kiuchumi kutokana na ugonjwa huo.

Amesema, katika utekelezaji wa mpango huo sekta ya Elimu imetengewa Sh.bilioni 10.32 sawa na asilimia 81.3 ya fedha zilizoidhinidhwa katika mkoa huo.

Amebainisha kuwa, sekta ya Elimu ya msingi fedha zilizotengwa ni Sh. bilioni 1.36 ambazo zitatumika kujenga vyumba 52 vya madarasa katika shule shikizi na mabweni 4 katika shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Aidha,kwa upande wa elimu ya Sekondari mkoa wa Ruvuma umetengewa Sh.bilioni 8.96 kwa ajili ya kujenga vyumba 448 vya madarasa kwa ajili ya kujiandaa kupokea wanafunzi wa kidato cha watakaojiunga Mwezi Januari mwakani.

Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa,ujenzi wa idadi ya vyumba hivyo vya madarasa unatokana na mahitaji kulingana na idadi ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na elimu ya Sekondari katika muhula wa masomo 2022 ambapo ameagiza madarasa hayo kukamilika ifikapo Desemba 2021.

Kwa upande wa huduma za afya ya msingi Jenerali Ibuge amesema,mkoa umetengea jumla ya Sh.bilioni 2.38 ambapo vipaumbele vitakavyotekelezwa kupitia fedha hizo ni kuanzisha huduma za dharura,kujenga jengo la huduma za wagonjwa mahututi na kununua mitambo miwili ya huduma za mionzi(machine za X Ray).

Katika hatua nyingine Ibuge amesema, Serikali itajenga nyumba sita zenye uwezo wa kuchukua familia 3 za watumishi wa afya na hivyo kuwezesha familia 18 za watumishi wa afya kupata makazi ya uhakika katika maeneo yaliyopo pembezoni.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala msaidizi mipango na uratibu Jumanne Mwankhoo amesema, fedha hizo zimegawanywa katika Halmashauri zote nane za mkoa wa Ruvuma.

Mwankhoo amezitaja Halmashauri hizo ni Halmashauri ya wilaya Tunduru iliyopata Sh. bilioni 2.990, Namtumbo Sh bilioni 1.810 Songea Sh.bilioni 1.390,Manispaa ya Songea Sh.milioni 660 Madaba Sh.bilioni 1.150.

Amezitaja Halmashauri nyingine ni Mbinga iliyopata Sh.bilioni 1.950,Halmashauri ya Mji Mbinga milioni 860 na Halmashauri ya Nyasa imepata Sh. bilioni 1.890.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad