HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 10, 2021

WIZARA YA UJENZI NA JWTZ ZAAHIDI KUKUZA USHIRIKIANO

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, ameliomba Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kuendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara yake katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayosimamiwa na Wizara hiyo nchini.

Akizungumza katika kikao cha kufahamiana na kubadilishana uzoefu na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ),
Luteni Jenerali  Methew Edward Mkingile, Dkt. Chamuriho, amesema kuwa licha ya Wizara kutumia wataalam mbalimbali katika miradi ya Ujenzi, bado inahitaji ushirikiano na  wataalam kutoka katika Jeshi hilo.

“Nakupongeza kwa uteuzi uliopata, naamini kuwa uteuzi huu utakuwa chachu ya kuendeleza ushirikiano tuliokuwa nao na kusaidia katika mwendelezo wa utekelezaji wa miradi inayosimamiwa na Wizara”, amesema Waziri Dkt. Chamuriho.

Aidha, Dkt. Chamuriho amesisitiza kuwa kutumia wataalam shirikishi kutoka katika Jeshi hilo imekuwa ni msaada mkubwa katika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha na kukamilika kwa wakati.

Kwa upande wake, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Methew Edward Mkingile, ameipongeza Wizara hiyo kwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Jeshi hilo na kuwaamini katika kutekeleza miradi ya Wizara.

“Sisi tupo tayari na bado tutaendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara na Taasisi za Serikali kama Sheria inavyotutaka, lengo ni kuhakikisha malengo na maendeleo ya nchi yanafikiwa”, amesisitiza Luteni Jenerali Mkingile.

Uongozi wa Wizara umekutana na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Methew Edward Mkingile, ikiwa ni siku kadhaa mara baada ya uteuzi wake ambapo pamoja na mambo mengine ziara hii ilikuwa na lengo la kuendeleza na kukuza ushirikiano baina ya Taasisi hizo.  

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho (wa kwanza kushoto), akijadiliana jambo na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Methew Edward Mkingile (wa pili kushoto), pamoja na baadhi ya viongozi wa Wizara katika kikao cha kufahamiana na kubadilishana uzoefu kilichofanyika ofisi za Wizara Mtumba, jijini Dodoma.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, akiwa katika picha ya pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Methew Edward Mkingile, mara baada ya kumaliza kikao cha kufahamiana na kubadilishana uzoefu katika ofisi za Wizara Mtumba, jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho (katikati), akifafanua jambo kwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Methew Edward Mkingile (Kushoto), na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Joseph Malongo, mara baada ya kumaliza kikao cha kufahamiana na kubadilishana uzoefu,  katika ofisi za Wizara Mtumba, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Joseph Malongo, akitambulisha baadhi ya viongozi wa Wizara hiyo kwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Methew Edward Mkingile, alipowasili Wizarani hapo Mtumba, jijini Dodoma.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad