HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, September 14, 2021

WAZEE WATAKIWA KUPATA HUDUMA ZA MATIBABU-NAIBU WAZIRI AFYA

 

Wahudumu maalum kwa Wazee katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Bukoba Mkoani Kagera wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis alipofanya ziara Hospitalini hapo kukagua huduma zinazotolewa kwa Wazee.

Mmoja wa Wazee wasiojiweza katika Makazi ya Kiilima, Mkoani Kagera akipokea zawadi ya Mchele kutoka kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis alipotembelea makazi hayo kuona jinsi utoaji wa huduma kwa wazee unavyoendelea.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akimjulia hali mtoto aliyejeruhiwa kwenye ajali ya Basi Mkoani Kagera na anaendelea na Matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Bukoba, Mkoani Kagera.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akisaini kitabu cha wageni cha Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera alipowasili Mkoani hapo kwa ziara ya kikazi. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo Brigedia Jenerali Charles Mbuge.
Baadhi ya Wazee wa makazi ya Wazee wasiojiweza Kiilima wakimsikiliza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (hayuko pichani) alipofanya ziara katika makao hayo yaliyoko nje kidogo ya Manispaa ya Bukoba, Kagera.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW

Na Mwandishi Wetu, Bukoba
SERIKALI imesema haitavumilia sababu zinazokwamisha Wazee kupata huduma ya matibabu kama ilivyo katika miongozo na maelekezo ya viongozi kuhusu huduma kwa Wazee nchini.

Naibu Waziri wa Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amesema hayo mjini Bukoba Mkoani Kagera katika ziara yake Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kagera kukagua ya utoaji wa huduma kwa wazee, wanawake na watoto.

Amesema kuwa maelezo kuhusu baadhi ya dawa kutotolewa kwa wazee kutokana na maelekezo ya Bima ya Afya yanahitaji kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu ili waweze kupata huduma kama ilivyoelekezwa.

“Nimeambiwa kwamba baadhi ya dawa hazipatikani kwa wazee kwa maelekezo kadhaa kulingana na viwango na uwezo wa hospitali tusingependa kusikia baadhi ya wazee wanakosa dawa kwa sababu yoyote.” alisema

Aidha, Mhe. Mwanaidi amemuelekeza Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera kuwasilisha taarifa ya upatikanaji wa dawa Wizarani ili kuhakikisha wazee na makundi mengine ya kipaumbele yanapata huduma stahiki.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mwanaidi alitembelea wodi ya watoto, wajawazito na wazazi na kupata maelezo ya huduma zinazotolewa hospitalini hapo.

Aidha, amewapongeza watoa huduma katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuongeza kwamba kazi hiyo ni ya wito hivyo waendelee kujitoa na kufanya kazi kwa moyo.

Wakati huo huo, Naibu Waziri Mwanaidi ametembelea Makazi ya Wazee wasiojiweza Kiilima nje kidogo ya Manispaa ya Bukoba na kuiagiza Wizara kuendelea kutoa huduma kwa wazee hao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad