HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, September 8, 2021

SEKTA YA AFYA KUIMARISHWA ZANZIBAR


Na Issa Mzee   Maelezo

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui, amesema Serikali ya Italy ina mpango wa kuisadia Zanzibar katika sekta ya afya ili kuimarisha huduma za afya nchini.

Alitoa kauli hiyo ofisini kwake Mnazi Mmoja, alipokutana na ujumbe kutoka Serikali ya Italy, uliofika Zanzibar kwa lengo la kutathmini namna bora ya kusaidia uimarishwaji wa huduma za afya nchini.

Alisema ujumbe huo kutoka Shirika la Italian Agency Development Cooperation, umelenga zaidi katika kusaidia huduma za uzazi, ili kuhakikisha afya bora ya mama na mtoto inaimarika nchini hasa wakati wa kujifungua.

Alieleza kuwa, shirika hilo linafanya kazi katika nchi za Afrika Mashariki, hivyo wameamuwa kufika Zanzibar ikiwa ni moja ya maeneo muhimu, ambayo yanahitaji huduma bora za afya katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mazrui aliwaeleza wageni hao kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ipo tayari kutoa ushirikino kwa washirika wote wa maendeleo, hasa katika sekta ya afya, ili ustawi mzuri wa jamii uweze kufikiwa kwa haraka.

Alisema kuwa, uimarishwaji na upatikanaji wa huduma bora za afya Zanzibar, ni chachu ya kuchochea wawekezaji duniani kuja kuwekeza nchini.

“Tunapokuwa na huduma bora za afya, hata wawekezaji watakuwa wengi kwani huduma bora za afya zinavuta uwekezaji na kuwaondolea hofu pale wanapopata tatizo la kiafya, hivyo ugeni huu utasaidia katika kufikia lengo la kuimarisha huduma bora za afya”, alisema Waziri.

Waziri Mazrui, alisema kutokana na idadi ya watu kuongezeka kila baada ya muda mfupi hasa katika maeneo ya mjini, ipo haja ya kujenga hospitali nyengine katika eneo la Mjini ili kupunguza msongamano katika hospitali ya Mnazi Mmoja, na kuwapa wepesi kina mama wanaofika hospitalini hapo kujifungua.

Aidha, Waziri huyo alitumia fursa hiyo kuipongeza serikali ya Italy, kwa kuunga mkono jitihada za kuimarisha sekta ya afya Zanzibar kwa maslahi ya wananchi wote.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Shirika la Italian Agency Development Cooperation, upande wa Afrika mashariki, Davide Bonechi,amesema zaidi ya dola 200 zinatarajiwa kutumika katika kuhakikisha mikakati ya kusaidia utoaji wa huduma bora Zanzibar inafanikiwa.

Alifafanuwa kuwa, shirika hilo lina mpango wa kuwapa mafunzo madaktari, kusaidia utoaji wa huduma bora za uzazi, pamoja na upatikanaji wa vifaa ili kuimrisha huduma za uzazi nchini.

Alisema kuwa, bado wanaendelea kufanya tathmini kwa kutembelea  vituo mbalimbali vya afya Zanzibar, katika vitengo vya uzazi ili kuona namna nzuri ya kusaidia huduma hizo.

Alisema kuwa mradi huo unaotarajiwa kufanyika kwa muda usiopungua miaka mitatu, utasaidia katika kuimarisha huduma bora za afya Zanzibar, hasa kwa akina mama wajawazito.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Fatuma Mrisho amesema Serikali ina mpango wa kupunguza msongamano kwa wagonjwa katika hospitali kuu ya Mnazi mmoja ili wananchi wapate huduma bora.

Alieleza kuwa, jitihada za kuimarisha vituo vya afya katika ngazi ya Wilaya na Mikoa unaendelea ili kuhakikisha huduma bora Mjii na Vijini zinapatikana.

Alieleza kuwa misaada ya vifaa tiba, ujenzi wa vituo vya afya pamoja na ujio wa wataalamu itasaidia katika kuwapatia wananchi huduma bora.


Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Fatma Mrisho (wapili kutoka kulia) akizungumza na Wajumbe kutoka shirika la Italian Agency Development Cooperation kuhusu Changamoto za Wizara ya Afya mara walipofika Ofisini kwake kwaajili ya Ziara yenye lengo la kutathmini namna bora ya kusaidia uimarishwaji wa huduma za Afya Zanzibar.

Mjumbe kutoa shirika la Italian Agency Development Cooperation Devide Bonechi akizungumzia lengo la ziara yao mara walipofika katika Ofisi ya Katibu  Mkuu Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto huko Mnazimmoja Zanzibar.


Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja Msafiri Marijani (katikati) akizungumza na Wajumbe kutoka shirika la Italian Agency Development Cooperation mara walipofanya ziara Hospitalini hapo yenye lengo la kutathmini namna bora ya kusaidia uimarishwaji wa huduma za Afya Zanzibar

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Nassor Ahemd Mazrui akizungumza na Wajumbe kutoka shirika la Italian Agency Development Cooperation mara walipofika Ofisini kwake huko Mnazimmoja Mjini Unguja kwaajili ya ziara yenye lengo la kutathmini namna bora ya kusaidia uimarishwaji wa huduma za Afya Zanzibar .


Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Nassor Ahemd Mazrui (kulia) akimkabidhi Mjumbe kutoka shirika la Italian Agency Development Cooperation Devide Bonechi kitabu maalum cha kumbukumbu za picha za picha za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar huko Ofisini Kwake Mnazimmoja Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad