HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, September 23, 2021

DKT.CHAMURIHO ATAJA MAFANIKO LUKUKI SEKTA YA YA UJENZI, UCHUKUZI

 Aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt.  Leonard Chamuriho, amesema  Wizara hiyo imeendelea kutekeleza kwa mafanikio Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka mitano (2021/22 - 2025/26) kwa kukamilisha miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa madaraja makubwa Tisa.

Akizungumza wakati wa kumkabidhi ofisi Waziri mpya wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa jijini Dodoma leo, Dkt. Chamuriho ameyataja madaraja yaliyokamilika kuwa ni daraja la Magufuli (Kilombero), Nyerere (Kigamboni -Dar es Salaam), Magara (Manyara), Kavuu (Katavi), Mlalakuwa (Dar es Salaam), Momba (Rukwa), Lukuledi (Lindi), Mara (Mara) na Sibiti mkoani Singida.

Aidha, Dkt. Chamuriho amesema daraja jipya la Selander, daraja la Msingi (Singida), daraja jipya la Wami,  Kitengule, Ruhuhu na Kigongo – Busisi, ujenzi wake unaendelea na uko katika hatua nzuri.

“Kuhusu usafiri wa anga, jumla ya ndege 11 zimenunuliwa na tayari mkataba wa ununuzi wa ndege nyingine mpya tano umeshafanyika”, amesisitiza.

Naye Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amemuomba aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho kuendelea kushirikiana na Wizara hiyo, ili kuwatumikia vyema watanzania.

Aidha, alimuelezea Dkt. Chamuriho kuwa ni kiongozi makini, mwenye utaalamu na ambaye amefanya mambo makubwa nchini kwa weledi ili kuhakikisha Watanzania wanapata miundombinu iliyo bora.

"Siwezi kuandika historia yangu bila kukutumia, tumetatua changamoto nyingi za Wizara hii hususani Sekta ya Uchukuzi tukiwa pamoja, hivyo nakuomba tuendelee kusaidiana kuwatumikia Watanzania," amesisitiza Prof. Mbarawa.

Makabidhiano hayo ya Ofisi yanafuatia mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan hivi karibuni. 

Aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho (kulia), akimkabidhi nyaraka za ofisi Waziri mpya Prof. Makame Mbarawa, katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mtumba, jijini Dodoma.
Aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, akitoa maelezo wakati akimkabidhi ofisi Waziri mpya Prof. Makame Mbarawa (kushoto), katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mtumba jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (wapili kulia), akiwa katika picha ya pamoja na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho ( wa pili kushoto), mara baada ya kukabidhiana ofisi. Kulia ni Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi, Bw. Gabriel Migire na kushoto ni Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Joseph Malongo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad