CHANJO YA UVIKO19 HAISABABISHI UGUMBA WALA KUPUNGUZA NGUVU ZA KIUME-DK MFINANGA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, September 28, 2021

CHANJO YA UVIKO19 HAISABABISHI UGUMBA WALA KUPUNGUZA NGUVU ZA KIUME-DK MFINANGA

Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha

KUNDI la wanawake limeaswa kujitokeza kupata chanjo ya Uviko 19 pamoja na kuondoa imani potofu ya kuwa chanjo hiyo inatia ugumba ama kuleta madhara ya uzazi.

Aidha chanjo hiyo, haiingiliani na dawa nyingine kama za magonjwa ya TB au VVU, mgonjwa mwenye magonjwa hayo atachanjwa na kuendelea na dozi yake.

Rai hiyo imetolewa, wakati wa mafunzo ya umuhimu wa chanjo ya Uviko 19 kwa hiari ,yaliyoshirikisha makundi mbalimbali ikiwemo viongozi wa dini, watendaji, viongozi na idara katika wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani, Dk Juma Mfinanga bingwa wa magonjwa ya mlipuko na dharura Muhimbili, alieleza wanaume wanajitokeza kwa wingi kuliko wanawake.

Aliitaka jamii kuachana na uzushi wa mitandaoni, vijiweni kuwa chanjo hiyo ina madhara katika uzazi ,ugumba na kupunguza nguvu za kiume.
Mfinanga alieleza chanjo hiyo ni salama ,huku akiwaomba wananchi wajitokeze makundi yote kupata chanjo na endapo kama kuna mtu ana mashaka ama maswali awaone wataalamu wa afya ili kupata majibu sahihi.

Akijibu suala la waliochanja kuendelea kuvaa barakoa alifafanua, hadi litakapofikiwa kundi kubwa lenye asilimia 60 ndipo wataweza kuacha kuvaa barakoa hivyo wanavaa ili kujilinda na maambukizi madogo madogo .

Nae mkuu wa wilaya ya Kibaha, Sara Msafiri alisema, mwanzo wakati zinagawiwa chanjo hizo mikoani kulikuwa na vituo 27 baada ya tathmini vikaongezwa na kufikia 54 na sasa inatarajiwa kuongezwa 275.

Msafiri alisema, hadi sasa katika mkoa wa Pwani wameshachanjwa watu zaidi ya 15,000 ,hivyo amehimiza wananchi waendelee kujitokeza japo ifikie asilimia 60 .

Mratibu wa chanjo Halmashauri ya Kibaha ,Hadija Tellack alisema ,awali walipokea chanjo 7,000 ambapo halmashauri ya Kibaha ilipatiwa chanjo 2,000 na Mji wa Kibaha 5,000.
"Hadi sasa waliochanjwa halmashauri ya Kibaha ni 1,251 sawa na asilimia 63,mji wa Kibaha ni 3,532 sawa na asilimia 71"

Tellack alielezea ,kwasasa zipo chanjo zilizobakia stoo na katika vituo lengwa halmashauri ya Kibaha zimebaki 685 na Mji Kibaha ni 1,390.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad