HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 27, 2021

CHANJO YA UVIKO-19 HAINA MADHARA KWA WAJAWAZITO


Na Joseph Lyimo
WANAWAKE wajawazito na wanaonyonyesha wametakiwa kupata chanjo ya Uviko-19 ili kuimarisha kinga za mwili za mama na mtoto kwani hazina madhara kwao.

Wanawake wajawazito ni miongoni mwa watu waliopo kwenye hatari pia kwani wanaweza kupata maambukizo ya Uviko-19 na kuathirika hivyo wanapaswa wapate chanjo ya Uviko-19.


Kaimu mganga mkuu wa halmashauri ya mji wa Babati Dkt Emmanuel Mkonyi ameyasema hayo wakati akielezea umuhimu wa chanjo ya Uviko-19 kwa wanawake wajawazito.


Dkt Mkonyi amesema mwanamke mjamzito akipata janga la Uviko-19 mimba inaweza kuharibika hivyo ni vyema kupata chanjo hiyo ya Uviko-19.


Amewatoa hofu wajawazito na wanawake wanaonyonyesha pamoja na makundi mengine katika jamii kuhusu chanjo ya Uviko-19 akiwataka kutoogopa kupata chanjo kwa kuhofia kiumbe aliyepo tumboni pamoja na maziwa ya mtoto.


"Wanawake wenye ujauzito na akina mama wote wanaonyonyesha wajitokeze kwa ajili ya kuchanja kwa kuwa chanjo hii ni salama na haina madhara yoyote kwa mama mjamzito wala anayenyonyesha," amesema Dkt Mkonyi.


Amesema mjamzito akijifungua anapokuwa ananyonyesha kinga ya mwili zina tabia ya kushuka kutokana na mahitaji ya mwili kuongezeka, kwa hiyo ni vyema wakapata chanjo ili kujikinga na Uviko-19.


Mjamzito mkazi wa Nangara Mjini Babati, Mary Ombay amesema elimu ya wajawazito kupatiwa chanjo ya Uviko-19 inapaswa kutolewa kwani baadhi ya wajawazito wanahofu kupata chanjo.


Ombay amesema awali alikuwa anaogopa kwenda kupata chanjo kwa kuwa alihofia maisha yake na ya mwanaye aliyetumboni.




"Kwa sasa nimepata elimu hii ya chanjo na madaktali wametushauri kupata chanjo ya Uviko-19 ni bora zaidi kuliko kutopata kwa sababu sisi wajawazito muda mwingi tunakuwa dhaifu ,kupata chanjo hii kutanihakikishia usalama wangu na wa mtoto wangu aliye tumboni," amesema.



Mkazi wa Mtaa wa Maisaka, Mariam Hassan amewashukuru wataalam wa afya kwa kupita mtaa kwa mtaa mjini Babati na kuwajengea uwezo juu ya chanjo ya Uviko-19.


"Tunashukuru sana kwani watu wengi hawana uelewa juu ya chanjo na wengine hawana sababu ya msingi ya kukwepa chanjo wala namna sahihi ya kujikinga hivyo elimu iendelee kutolewa," amesema.


Mkazi wa Mtaa wa Miomboni Abdalah Hamis amesema elimu ya wajawazito kupatiwa chanjo hata yeye imemnufaisha kwani awali mke wake ambaye ni mjamzito aliambiwa na majirani asichanje ila kupitia elimu hiyo atachanja.


"Madaktari wanapita mitaani kutupa elimu ya chanjo tunamshukuru kwani watu wengi wanaogopa kupata chanjo na wengine wanakwepa bila sababu ya msingi jambo hili linatufanya tuwe hatarini kupata maambukizi ya Uviko-19," amesema.


Amesema kutokana na elimu hiyo pia wamejifunza usipopata chanjo na endapo ukipata maambukizi unakuwa hatarini zaidi, hivyo ni vyema kila mtu akapata chanjo ya Uviko-19.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad