HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, August 17, 2021

WAZIRI MKENDA ATUA BABATI/AITAKA NFRA KUFANYIA KAZI CHANGAMOTO KABLA YA KUKABIDHIWA MRADI WA VIHENGE VYA KISASA NA MAGHALA

 


 

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akikagua ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa vya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja Wilaya ya Babati Mkoani Manyara leo tarehe 16 Agosti 2021. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akikagua ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa vya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja Wilaya ya Babati Mkoani Manyara leo tarehe 16 Agosti 2021. 
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akipata maelezo ya ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa vya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja Wilaya ya Babati Mkoani Manyara leo tarehe 16 Agosti 2021. 
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akikagua mitambo ya kusafisha nafaka kwenye ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa vya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja Wilaya ya Babati Mkoani Manyara leo tarehe 16 Agosti 2021. 

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Manyara

Serikali imebainisha kuwa kuchelewa kukamilika kwa ujenzi wa Vihenge vya Kisasa na Maghala kumetokana na tatizo la mgogoro wa mwingiliano wa viwanja kati ya Shirika la umeme (TANESCO) na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

Mgogoro huo ulipelekea mkandarasi kusimama na baadaye kuongezewa muda wa mkataba wa kutekeleza mradi mpaka tarehe 13 Septemba 2021.

Akizungumza mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya siku moja Wilaya ya Babati Mkoani Manyara leo tarehe 16 Agosti 2021 Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa pamoja na mradi huo kukamilika kwa asilimia 99.8 kama inavyotajwa lakini bado NFRA inapaswa kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali kabla ya kukabidhiwa mradi huo.

Waziri Mkenda amebainisha kuwa changamoto hizo ni pamoja na kupewa elimu ya namna gani vihenge hivyo vitaweza kufanyiwa usafi kwani kwa sasa hakuna uwezekano wa kufanya usafi jambo ambalo ni hatari kwa uhifadhi wa nafaka zinazonunuliwa na kuhifadhiwa na serikali.

Pia ameitaka NFRA kuhakikisha kuwa inasimamia utekelezaji wa uwezekano wa njia sahihi ya kutibu nafaka inayohifadhiwa kwenye Vihenge hivyo vya kisasa (Fumigation) kwani eneo hilo ni muhimu zaidi kwa ajili ya uhifadhi.

Ujenzi wa Vihenge vya Kisasa na Maghala kanda ya Arusha inayojumuisha mikoa ya Arusha na Manyara katika kituo cha Babati unatekelezwa na kampuni ya Unia Sp.zo.o kutoka nchini Poland kwa kushirikiana na kampuni ya wazawa ya Elerai Construction Company Ltd kwa gharama ya Dola za Kimarekani Milioni 8.08 ambazo ni sawa na Bilioni 18.67 za kitanzania.

Kwa ujumla sehemu kubwa ya mradi imechukuliwa na ujenzi wa vihenge ambao ni zaidi ya asilimia 60 ya mkataba. 

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa sasa una maghala 34 yenye uwezo wa kuhifadhi nafaka Tani 251,000 katika kanda zake nane za kimakakati.

Hivyo serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi huo ambao ni maalumu kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kuhifadhi kwa jumla ya Tani 250,000 wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 55 ambazo ni sawa na Bilioni 126.5 ambapo mradi huo utakapokamilika utaongeza uwezo wa kuhifadhi wa NFRA kutoka Tani 251,000 za sasa hadi kufikia Tani 501,000.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad