Na Hassan Mabuye, Mbeya
WAZIRI
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amezindua
mpango wa kitaifa wa kuwakopesha wananchi fedha za kufanya urasimishaji
wa maeneo yao kwa kipindi cha miaka miwili.
Waziri
Lukuvi ameyasema hayo katika kata ya Igawa wilayani Mbarali mkoa wa
Mbeya wakati akizindua Mpango wa maalumu wa kukopesha wananchi gharama
ya kupanga, kupima na kupewa hati kwa kushirikiana na Benki ya NMB.
Lukuvi
amesema mpango huu ni wa nchi nzima ambao umeanzia hapa Mbarali kwa
kuwamilikisha wananchi zaidi ya 52,000 kwa kuwa mazoezi mengi ya
urasimishaji yameshindwa kufanikiwa kwa sababu baadhi ya wananchi
wameshindwa kupata fedha kwa mkupuo kugharimia shilingi 150,000 za
upimaji na umilikishaji.
“nimeamua
kuanzisha mpango huu kwa kushirikiana na NMB ambao watawakopesha fedha
za kupanga, kupima na kuandaa hati ambazo Benki italipa 100% kwa mkupuo
kisha nyinyi mtalipa taratibu na kwa awamu kwa muda wa miezi 24 yaani
miaka miwili” Amesema Waziri Lukuvi.
“baadhi
ya wananchi wamekwamisha kazi hii ya urasimishaji katika maeneo mengi
kwa kuwa wachache ndio wameweza kupata fedha za kugharimia upangaji,
upimaji na umilikishaji kwa wakati. Sasa NMB leo hapa Mbarali wamekuja
kuwakopesha wananchi gharama zote. Na ninataka zoezi kama hili lifanyike
nchi nzima na wengine waige kwa kuafuata utaratibu huu" Ameongeza
Waziri Lukuvi.
Amesema
pia 90% ya wananchi wa Mbarali walikuwa hawakopesheki kwa sababu ya
ardhi yao ilikuwa haijapangwa wala kupimwa. Lakini kwa mpango huu pia
watakuwa na haki ya kukopeshwa na benki yoyote hapa nchini kwa kuwa
watakuwa na dhamana inayotambulika kisheria ambayo ni hatimiliki ya
ardhi.
Naye
Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Benki ya NMB Bwana Benedicto Baragomwa
amewataka wananchi kuchangamkia fursa hii kufanya urasimishaji kupitia
Benki ya NMB ambayo itafanya zoezi hili kwa kutumia matawi yake yote 226
nchi nzima kujipatia mkopo huu na kujiwezesha kiuchumi.
Kwa
upande Mwingine Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Bibi Mary Makondo amewahakikishia wananchi kwamba Wizara yake
itasimamia kikamilifu mpango huu ambao wananchi watapewa hatimiliki za
ardhi za miaka 99 na watamilikishwa kisheria.
No comments:
Post a Comment