MAWAZIRI WA FEDHA TANZANIA BARA NA ZANZIBAR KUTATUA CHANGAMOTO ZA MIRADI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, August 4, 2021

MAWAZIRI WA FEDHA TANZANIA BARA NA ZANZIBAR KUTATUA CHANGAMOTO ZA MIRADI

 

Na. Saidina Msangi na Sandra Charles, WFM, Dodoma

Waziri wa Fedha na Mipango wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, wamekubaliana kutatua changamoto za utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kufanya kazi kwa kushirikiana ili kukuza uchumi wa Taifa.

Mawaziri hao wamekutana jijini Dodoma katika kikao kazi kilicholenga kuangalia masuala yaliyokuwa na changamoto wakati wa bunge la bajeti na Sheria ya Bajeti pamoja na masuala yanayohusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Dkt. Nchemba alisema kuwa kikao hicho kimekuwa cha mafanikio ambapo mengi yamefikia hatua nzuri na kuongeza wigo wa ushirikishwaji hasa katika kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mipya ya kipaumbele iliyoko katika Bajeti Kuu ya Serikali.

“Katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo tunaangalia uwezeshaji na utekelezaji wa miradi inayoendelea na miradi mipya, na mengi tuliyojadili tumefikia hatua nzuri,” alisema Dkt. Nchemba.

Waziri Nchemba aliwaagiza wataalamu wa pande zote kuendelea kufanyia kazi maeneo ya changamoto yaliyosalia ikiwemo uboreshaji wa Sheria ya Usajili wa Vyombo vya Moto.

“Niwasihi msiishie kwenye Sheria ya Vyombo vya Moto ila muangalie na waendeshaji wa vyombo vya moto haipendezi mtu kuwa na leseni mbili wakati nchi ni moja”, alisisitiza Dkt. Nchemba.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, alisema kuwa kikao kati yake na mwenzake Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba kimetoa njia ya namna ya kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo hususani za miradi.

Alisema kuwa wamejadili namna ya kufanikisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati iliyopo upande wa Zanzibar, jambo ambalo lina tija kwa wananchi wa Zanzibar.

“Hili ni jambo muhimu tunashukuru uwepo wa kikao hiki ambacho kinatoa mwanga wa namna miradi ya kimkakati Zanzibar itatekelezwa na uwezeshaji wake,” alisema Mhe. Jamal Kassim Ali.

Aidha ameushukuru uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango upande wa bara kwa kikao hicho na kueleza kuwa kikao hicho ni vema kikawepo angalau kila baada ya miezi miwili ili kuona mambo mapya yatakayoibuka yanatatuliwa na kufanya ufuatiliaji wa makubaliano yaliyopita jambo ambalo lililidhiwa na pande zote.

Waziri wa Fedha na Mipango wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia), akipeana mkono na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, baada ya kumalizika kwa mkutano kati yao ulioangazia masuala ya fedha na utekelezaji wa miradi, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, wakiongoza mkutano ulioangazia masuala ya fedha na utekelezaji wa miradi, jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza jambo wakati wa kikao kati yake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali (kushoto), jijini Dodoma.
Wajumbe wa Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali (hawapo pichani), wakiteta jambo, baada ya kumalizika kwa Mkutano huo, jijini Dodoma.
Afisa Habari wa Wizara ya Fedha na Mipango. Bi. Saidina Msangi na Msaidizi wa Waziri wa Fedha na Mipango, Bw. Moris Linuma, wakiangalia nyaraka, wakati wa Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali (hawapo pichani), jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa pili kulia) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali (wa pili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja, baada ya kumalizika kwa Mkutano kati yao, jijini Dodoma.

(Picha na Peter Haule, WFM, Dodoma)No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad