HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 8, 2021

VYUO VILIVYO CHINI YA WIZARA YA FEDHA VYAAGIZWA KUONGEZA TAFITI

 


Na. Peter Haule, WFM, Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamadi Yussuf Masauni, amekiagiza Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) kufanya tafiti zitakazo ibua vyanzo vipya vya mapato na kodi ili kuisaidia Serikali katika kutekeleza mipango ya maendeleo kwa watanzania.

Agizo hilo limetolewa jijini Dar es Salaam alipotembelea Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya vyuo hivyo katika mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea taasisi zote zilizo chini ya wizara hiyo.

Mhandisi Masauni alisema kuwa Vyuo hivyo vimekuwa vikifanya vizuri katika mambo ya taaluma kwa kuongeza Kozi mbalimbali, idadi ya wanafunzi licha ya changamoto ya miundombinu na ufaulu lakini suala la utafiti linatakiwa pia kupewa msukumo wa ziada.

“Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2021/22 imepokelewa vizuri na wabunge na wananchi kwa ujumla hususani katika mabadiliko ya kodi na vyanzo vya mapato, lakini jambo hili linaweza kuwa endelevu kwa kufanya tafiti zaidi ili kuweza kuwa na kodi na vyanzo vipya vya mapato ambavyo si kero kwa mwananchi’’, alieleza Mhandisi Masauni.

Mhandisi Masauni amevitaka Vyuo hivyo kuendelea kufanya tafiti pia katika eneo la ununuzi na ugavi na kutoa ushauri kwa Serikali ili kuongeza nguvu katika usimamizi wa fedha za miradi kwa kuwa fedha nyingi hutengwa kwa ajili ya maeneo hayo.

Amezihakikishia Menejimeti za Vyuo hivyo kuwa Wizara ya Fedha na Mipango itashirikiana navyo kufanikisha tafiti zitakazoongeza tija kwenye uchumi na maendeleo ya    nchi.

Mhandisi Masauni alisema kuwa Vyuo hivyo vinawataalamu wabobezi katika masuala ya usimamaizi wa fedha na bima, masuala ya ugavi na ununuzi hivyo wanaweza kuwa washauri wazuri katika nyanja hizo kwa Wizara ya Fedha na Mipango iliyopewa dhamana ya kusimamia uchumi wa nchi na Serikali kwa ujumla ili kuweza kupiga hatua za maendeleo.

Alisema kuwa suala la ushauri elekezi unaotokana na tafiti una tija si tu kwa mapato ya Serikali lakini pia kwa vyuo, hivyo ni vema Vyuo hivyo vikaongeza jitihada za kuongeza tafiti na ushauri kwa Serikali kwa kuwa kuna uhitaji mkubwa.

Aidha amevitaka Vyuo hivyo kutoa mafunzo ya muda mfupi hususani kwa watumishi wa umma wanaofanya kazi kwenye taasisi zinazofanana na fani zilizopo katika Vyuo hivyo ili kuwaongezea uwezo lakini pia kukuza kipato cha chuo.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA), Dkt. Momole Kasambala, alisema kuwa, katika mwaka wa fedha 2019/20 hadi sasa taasisi imefanikiwa kuboresha miundombinu ya utafiti, ushauri wa kitaalamu na machapisho.

Dkt. Momole alisema kuwa TIA imefanikiwa kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu mbinu za ukusanyaji mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa Halmashauri tano hadi kufikia, Juni 2021.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Prof. Tadeo Satta, amesema kuwa idadi ya tafiti imeongezeka na sasa wameingia katika hatua ya uandishi wa vitabu na pia suala la mafunzo kwa watumishi wa umma litafanyiwa kazi ili kuongeza tija katika utendaji kazi kwa waTumishi wa umma.

Wakuu wa Vyuo hivyo wamemshukuru Naibu Waziri Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, kwa kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ili kuona majukumu yanatekelezwa kwa ufanisi.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Masauni, anaendelea na ziara ya kutembelea taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni(Mb) akiiagiza Menejimenti ya Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) kuhakikisha wanafanya tafiti na kuja na vyanzo vipya vya mapato na kodi zisizo na usumbufu kwa wananchi, alipotembelea Chuo hicho kilicho chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkuu wa Chuo hicho. Dkt. Momole Kasambala.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb), akikabidhiwa kitabu na Mkuu Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA), Dkt. Momole Kasambala, baada ya kufanya mkutano na Menejimenti ya Chuo, katika ziara yake ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es Salaam.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA)anayeshughulikia fedha, Dkt. Hassanal Isaya, akieleza nia ya Chuo hicho ya kufanya tafiti katika vyanzo vya mapato na kodi, lakini pia kuzishauri  Halmashauri kuhusu masuala ya Fedha,  wakati wa Mkutao wa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb) na Menejimenti ya Chuo hicho, jijini Dar es Salaam.

1 comment:

  1. Awesome and interesting article. Great things you've always shared with us. Thanks. Just continue composing this type of post.

    ReplyDelete

Post Bottom Ad