HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 29, 2021

Bodi ya wakurugenzi TANESCO yaagiza kuongezeka kasi ya ujenzi wa mradi wa umeme wa RUHUDJI


Na Amiri Kilagalila,Njombe

Bodi ya wakurugenzi wa shirika la umeme Tanzania TANESCO imewaagiza wataalamu kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi wa umeme  kwa kutumia maporomoko ya maji ya mto Ruhudji uliopo kijiji cha Itipula wilayani Njombe.

Agizo hilo limetolewa na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa TANESCO  Dkt.Alexander Kyaluzi wakati bodi hiyo ilipotembelea na kuona mahali utakapojengwa mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 358.

"Wataalamu wa mradi huu waende kasi zaidi kwasababu huu mradi unategemewa sana na viongozi wetu wameshauzungumza mara nyingi kwa hiyo tungependa utekelezwe kwa muda mfupi iwezekanvyo,kwa hiyo tungeomba wataalamu wetu kila hatua waifikie kwa haraka zaidi"alisema Dkt.Alexander Kyaluzi
 
Aidha Dkt.Kyaluzi amesema lengo la bodi hiyo kutembelea katika mradi muhimu na tegemeo kwa tofauti ni pamoja na kuutambua zaidi ili kuelewa namna unavyotekelezwa pamoja na bajeti zake.

"Lengo letu ilikuwa ni kuja kuona changamoto zake za kufika hapa site kwasababu wakati mwingine bodi mtaletewa taarifa ya kupitisha fedha halafu mnasema hizi hela ni nyingi sana.Kwa hiyo ziara  imetusaidia kupata taarifa ili wakati tunapitisha makadirio basi tunakuwa na kumbu kumbu"alisema Dkt,Kyaluzi

Kwa upande wake mhandisi Toto Zedekia msimamizi wa muda wa mradi huo licha ya kupokea maelekezo ya bodi ya wakurugenzi wa TANESCO,amesema mradi huo muhimu unaotarajiwa kujengwa kwa miezi 36 utakuwa ni miongoni mwa miradi muhimu nchini kwa kuwa maji ya mto huo hayakauki mwaka mzima.

"Mwaka 1998 ndipo ulipofanyika upembuzi yakinifu kwa hiyo kutokana na study ya mradi huu tumejihakikishia kwamba kuna maji ya kutosha kwasababu tunapima maji kila wakati na tumejiridhisha yapo wakati wote wa mwaka"alisema Toto Zedekia

Vile vile amesema licha ya kuchelewa kwa mradi huo lakini wanatarajia kufanya kazi kwa kasi na kwa sasa wamekuwa wakisubiri bajeti ili mradi huo uweze kuanza.

Baadhi ya wananchi wanaozunguka mradi huo akiwemo Ibrahim Kilasi wamesema wapo tayari kuendelea kutunza mto huo na mito mingine midogo inayoingiza maji katika mto ruhudji ili kuwezesha  umeme utakaozalishwa katika mradi huo kuwa wa kudumu kwa kuwa utakuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa Njombe na taifa kwa ujumla.
Moja ya eneo la mradi wa umeme wa maji ya mto Ruhudji sehemu ambayo itajengwa bwawa kubwa likionekana kwa umbali wakati bodi ya wakurugenzi ilipofika na kujionea eneo la mradi huo.
Dkt.Alexander Kyaluzi  mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi TANESCO akitoa maagizo kwa wataalamu wa mradi ili kuongeza kasi ya ujenzi huku akieleza pia faida za bodi hiyo kutembelea katika eneo la mradi.
Bodi ya wakurugenzi wa TANESCO wakiwa katika picha ya pamoja na mkuu wa mkoa wa Njombe Marwa Rubirya walipofika mkoani Njombe kwa lengo la kutembelea miradi ya umeme inayojengwa mkoni humo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad