HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, July 27, 2021

Benki ya CRDB yaingia mkataba wa makubaliano na Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Kuwezesha ulipaji wa gharama za kutoa mizigo bandarini kwa riba nafuu

Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts akibadilishana mkataba na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini (JWT), Mchungaji Silva Kiondo wakati wa hafla ya kutia sahihi mkataba wa makubaliono utakaowawezesha wafanyabiashara kupata mkopo wa kulipa gharama za kutoa mizigo bandarani kwa riba nafuu. Wengine pichani ni Mkuu wa Kitengo cha Biashara Benki ya CRDB, Toyi Ruvumbangu (Kushoto) na Mkurugenzi wa Mawasiliano JWT, Stephen Chamle.
 
========     ========= 
 
Dar es Salaam 27 Julai 2021 – Ikiendeleza jitihada zake za kumuwezesha mfanyabiashara nchini, leo, Benki ya CRDB imesaini mkataba wa makubaliano na Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) kuwezesha kulipia gharama za kutoa mzigo bandarini. 

Akizungumza katika hafla hiyo ya utiaji saini mkataba wa makubaliano, Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts alisema ushirikiano huo utawawezesha wafanyabiashara kulipia gharama za kutoa mizigo bandarini kwa mkopo (Post Import Financing Solution) na kuondokana na changamoto za uchelewshaji wa mizigo ambazo huongeza gharama.
Dkt. Witts alisema huduma hiyo ni sehemu ya jitihada zinazofanywa na Benki ya CRDB kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu katika kuboresha mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara nchini. Alisema ili kutoa unafuu zaidi kwa wafanyabiashara Benki hiyo imepunguza riba katika huduma hiyo ambapo wateja watakuwa wakitozwa asilimia 16 kulinganisha na asilimia 18 inayotozwa katika mikopo ya kawaida. 

Katika makubaliano hayo Benki ya CRDB itakuwa ikisaidia kulipa gharama za kutoa mizigo bandarini na wafanyabiashara kulipa katika kipindi cha miezi mitatu. Akielezea taratibu za upatikanaji wa huduma hiyo, Dkt. Witts alisema huduma hiyo itatolewa kwa wafanyabiashara ambao ni wanachama wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania. 

“Mkopo huu hutolewa kulingana na kiwango cha gharama za malipo ya mzigo uliopo bandarini ambapo mfanyabiashara anaweza kulipia gharama za kodi ya forodha, gharama za bandari na wakala wa meli kwa wakati na bila kuchelewa,” aliongezea Dkt. Witts ambapo alifafanua kuwa riba hiyo inaweza kupungua zaidi kutokana na mwitikio na uaminifu utakao kuwa ukionyeshwa na wafanyabiashara.
Mkopo huo wa gharama za tozo/ kodi ya mizigo iliyoagizwa kutoka nje inatolewa kwa masharti nafuu bila ulazima wa kuwa na dhamana ya mali isiyohamishika na hutolewa kwa riba nafuu ambapo mteja atapata fedha kwa muda mfupi usiozidi siku saba pindi atakapowasilisha ombi la mkopo.

Aidha, malipo ya kodi na gharama za kodi na bandari zitalipwa moja kwa moja kwenye taasisi husika ikiwamo TRA, TPA au Wakala wa meli. Dkt. Witts alisema wamefanya hivyo ili kusaidia na kurahisisha ulipaji kodi kwa wakati. 

“Dhumuni letu ni kuleta urahisi kwa wafanyabiashara kupata bidhaa/ mizigo yao pindi wanapoagiza kutoka nje. Lakini vilevile huduma hii itasaidia jitihada za Serikali kukusanya kodi kwa wakati na kuboresha uchumi wa nchi kwa kuhakikisha wafanyabiashara wote wanalipa kodi katika muda uliowekwa kama ambavyo serikali imekua ikisisitiza” alisema Dkt. Witts.

Dkt. Witts aliongezea kuwa huduma hiyo itakwenda kutoa nafuu kwa wafanyabiashara kipindi hiki cha corona ambapo biasahara nyingi zimepata changamoto. Alisema Benki ya CRDB imejidhatiti kuhakikisha inawafikia wafanyabiashara wengi zaidi kupitia huduma hiyo. 

 “…ni matumaini yangu kuwa utaratibu huu wa mikopo ya kutoa mzigo bandarini utekwenda kuwa ni suluhisho kubwa kwa kila mfanyabiashara kwani inaenda kuleta unafuu wa gharama za bandari zinazotokana na kuchelewa kulipia gharama za uingizaji wa bidhaa,” alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Nchini, Mchungaji Silva Kiondo aliishukuru Benki ya CRDB kwa kutambua umuhimu wa wafanyabiashara kupitia jumuiya hiyo na kubuni huduma hiyo ambayo itakwenda kuondoa changamoto nyingi wakati wa uingizaji wa bidhaa nchini.

“Tunajivunia kwa Jumuiya yetu kufikia mafanikio haya, malengo yetu ni kuona wanachama wetu wanafanya biashara zao bila usumbufu wa aina yoyote. Nitoe wito sasa kwa wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa nje kutumia fursa hii kuboresha biashara zao,” alisema Mchungaji Kiondo huku akisema jumuiya hiyo imejipanga kukamilisha na kuhakikisha inawahudumia kikamilifu wafanyabishara ili wawe na uhakika na biashara zao.
Jumuiya hiyo pia iliipongeza Serikali kwa kuendelea kuisisitiza Wizara ya fedha na mipango kupitia TRA iweke mazingira wezeshi na rafiki yenye hamasa katika uendeshaji biashara na uwekezaji utakaoleta upanuaji wa wigo wa kodi nchini. 




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad