Brigedia Jenerali Ibuge akagua mpaka wa Tanzania na Msumbiji - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 1, 2021

Brigedia Jenerali Ibuge akagua mpaka wa Tanzania na Msumbiji

 MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amefanya ziara yake ya kwanza tangu ateuliwe kuwa Mkuu wa Mkoa kwa kukagua eneo la Mkenda lililopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji kupitia wilaya ya Songea.

Brigedia Jenerali Ibuge amekagua daraja la Mkenda Mto Ruvuma linalotenganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji, amezungumza na askari wa Msumbiji waliopo mpakani,ametembelea kivuko cha Mitomoni,kupitia Mto Ruvuma,amekagua soko la kimataifa la Mkenda na kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Mkenda.

Akizungumza na watumishi wa Idara za uhamiaji,Mamlaka ya Mapato Tanzania,polisi na Usalama waliopo eneo la Mkenda,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amelitaja lengo la serikali kuwaweka watumishi hao mpakani ni kusimamia maslahi ya taifa.

 Amewataka watumishi hao kila mmoja katika Idara yake kushirikiana na kufanya kazi kwa tija na ufanisi kwa maslahi ya watanzania.

“Sasa hili la ushirikiano nataka kusisitiza,mpo mbele ya mpaka wetu ,kumbukeni kuna changamoto kubwa ya ugaidi inayotukabili kwenye mpaka wetu na Msumbiji ,huu sio wakati wa kuchukulia vitu poa’’,alisisitiza Brigedia Jenerali Ibuge.

Hata hivyo amewatahadharisha watumishi hao wasipokuwa na muunganiko wanapobaini watuhumiwa wakiwemo wahamiaji haramu, biashara zinazotia mashaka na vitendo vya rushwa wanaweza kuharibu mfumo mzima wa Mkoa na Taifa kwa ujumla kutokana na uzembe na ujinga wa mtumishi mmoja.

Kuhusu watumishi wa TRA waliopo mpakani,RC Ibuge amesema licha ya ukweli kuwa mapato ni muhimu kwa maendeleo ya nchi,hata hivyo ametaka ushirikiano wa kuangalia mazingira ya kiforodha yaangaliwe kiulinzi na usalama kwa kudumisha mawasiliano na vyombo vingine vya usalama.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa ametoa pole na kuwafariji wananchi wa kijiji cha Mkenda kutokana na vifo vilivyotokea katika ajali ya majini kwenye mto Ruvuma hivi karibuni.  

Hata hivyo ametoa rai kwa Mwenyekiti wa kijiji cha Mkenda na wananchi kwa ujumla kushirikiana na vyombo vya usalama vilivyopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji ili  kujilinda kwa ajili ya usalama wa wananchi na Taifa kwa ujumla. 

Awali akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Kituo cha Uhamiaji Mkenda,Mratibu Msaidizi wa Uhamiaji Upendo Kikudo amesema kituo hicho kinafanya kazi kwa ushirkiano na Idara nne ambazo ni  Uhamiaji,Polisi,TRA na Usalama wa Taifa.

Amezitaja changamoto zinazokikabili kituo hicho ni ukubwa wa mpaka kutokana na jiografia ya eneo lililozungukwa na Mto Ruvuma na misitu,hali ya machafuko inayoendelea nchini Msumbiji,uwepo wa vipenyo vingi vilivyo rasmi na visivyo rasmi,mawasiliano,miundombinu ya barabara,huduma za afya na ukosefu wa nishati ya umeme.


Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akikagua kivuko cha mto Ruvuma eneo la Mitomoni wilayani Songea

Wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiwa ameongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa na wilaya ya Songea,kukagua daraja la Mkenda Mto Ruvuma wilayani Songea ambalo linatenganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji


Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akipata maelezo ofisi ya uhamiaji eneo la mpakani upande wa pili wa nchiMsumbiji.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad