SimBanking yatajwa kuwa mkombozi huduma za kibenki - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, April 12, 2021

SimBanking yatajwa kuwa mkombozi huduma za kibenki

Ujumuishi wa huduma za fedha unasaidia kuongeza matumizi ya mifumo rasmi ya kifedha na kuchochea shughuli za kiuchumi. Maendeleo ya kiteknolojia yamesaidia taasisi za fedha kubuni mifumo jumishi ya utoaji huduma ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kufikia lengo la kusogeza huduma za kifedha kwa watu wengi hususan waliopo vijijini. 
 
Pamoja na kupunguza gharama za miamala, huduma jumuishi za fedha zinafungua milango ya fursa zinazoweza kuleta mapinduzi katika jamii. Taasisi za fedha zimekuwa nyenzo muhimu kuwezesha hilo kwa kubuni njia mbadala za kufikisha huduma kwa wananchi. 
 
Benki ya CRDB ilianzisha huduma ya SimBanking mwaka 2011 kwa lengo la kurahisha upatikanaji wa huduma na kuwawezesha wateja kufanya miamala yao ya kifedha popote walipo kupitia simu za mkononi, kwa kupiga *150*03#. Mwaka 2016, Benki ya CRDB ilianzisha huduma ya SimBanking App kupitia simu janja (smartphones) ili kuendana na mahitaji ya wateja ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na ukuaji wa teknolojia.
 
Wachambuzi wa masuala ya fedha wanasema kwa miaka yote iliyokuwa sokoni, SimBanking imekuwa njia ya huduma za kifedha inayotegemewa zaidi katika soko. Kwa sasa Benki ya CRDB inatekeleza mpango wa miaka mitano (2018-2022) ambao umejikita katika kutoa huduma za kidigitali kwa lengo la kuendana na mabadiliko ya mahitaji ya wateja wao. Utekelezaji wa mpango huu unachangia kuongeza nguvu katika jitihada za Serikali kutimiza Dira ya Maendeleo ya 2025 kwani kupitia huduma za kidigitali Benki ya CRDB itaweza kujumuisha Watanzania wengi zaidi.
 
Hivi karibuni Benki ya CRDB ilizindua huduma ya SimBanking App iliyoboreshwa zaidi inayowawezesha wateja kufungua akaunti ya Benki ya CRDB kwa kutumia simu bila ya kwenda kwenye tawi kwa kutumia kitambulisho cha NIDA na alama za vidole tu.
 
Maboresho hayo ya huduma ya ‘SimBanking’ yamekuwa kivutio kikubwa kwa Watanzania ambapo ndani ya mwezi mmoja wateja zaidi ya 2,000 wamefanikiwa kufungua akaunti kupitia simu zao, huku miamala zaidi ya milioni 2.5 ikifanyika ndani ya kipindi hicho.
 
“Ubunifu huu waliokuja nao Benki ya CRDB ni wakupongezwa sana, mwanzoni nilikuwa na shaka inawezekanaje lakini nilipo pakua SimBanking App katika simu yangu niliweza kufungua akaunti kwa hatua chache tu,” anasema Juma Mlala mjasiriamali wa Gairo, Dodoma. Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Abdulmajid Nsekela, anasema Benki ya CRDB imejidhatiti kuwawezesha watanzania wengi zaidi kupata huduma za fedha kupitia mifumo ya kidijitali ikiwamo SimBanking.
 
Awali kabla ya ujio wa huduma ya SimBanking, Watanzania wanaoishi vijijini walikuwa wanalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za kifedha.  “SimBanking App imekuwa na msaada mkubwa kwa Watanzania hususani wanaoishi vijijini kwa kuwa kwa sasa huduma za kifedha zinapatikana viganjani mwao kupitia app hiyo,” alisema Nsekela. 
 
David Machumu, mwalimu ambaye ana akaunti ya CRDB katika wilaya ya Malinyi, mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa wanufaika wa SimBanking. Akitoa ushuhuda wanamna ambavyo SimBanking imesaidia kuboresha maisha yake, Machumu, amesema miaka ya nyuma kabla ya kujiunga na SimBanking ilikuwa inamlazimu kila mwisho wa mwezi kusafiri mpaka wilaya ya Ifakara, umbali wa kilometa 108 kuangalia kama ameingiziwa mshahara wake kwenye akaunti. 
 
“Kabla ya SimBanking ilikuwa inatugharimu sana linapokuja suala la pesa na muda,” alisema Machumu. Kupitia SimBanking Machumu kwa sasa hana haja ya kusafiri umbali mrefu kwa kuwa anaweza akatumia simu yake ya kiganjani kuangalia kama ameingiziwa mshahara wake na pale anapohitaji pesa taslimu hufanya miamala kwa CRDB Wakala waliopo wilayani humo. 
 
Huduma ya SimBanking imesaidia sana kubadilisha mtazamo wa Watanzania wengi juu ya upatikanaji wa huduma za kibenki kwani hivi sasa takribani asilimia 95 ya huduma hupatikana kiganjani. 
 
Akielezea huduma zinazopatikana kupitia SimBanking, Nsekela amedadavua kuwa mbali na kuwawezesha wateja kufungua akaunti wenyewe, SimBanking sasa hivi inatoa wigo mpana wa huduma za benki hiyo ikiwamo kuomba mkopo, kulipa bima, kuhamisha pesa, kulipia manunuzi, pamoja na huduma ya kutoa fedha kupitia matawi, CRDB Wakala na ATMs. 
 
Sanjari na huduma hizo, mteja pia anaweza kufanya malipo ya kodi za Serikali kwenda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), malipo ya bandarani kwenda mlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) pamoja na bili za umeme na maji. 
 
“Uwepo wa huduma zote muhimu za kibenki kupitia SimBanking, unaifanya kuwa benki kiganjani na ndio maana tunasema ‘Benki ni SimBanking’,” ameongezea Nsekela huku akibainisha kuwa kipaumbele cha Benki ya CRDB ni kutoa huduma bora na zinazopatikana kwa urahisi. Wakati wa uzundizi wa maboresho ya SimBanking, Waziri wa Mawasiliano na Teknoljia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile alionyesha matumaini makubwa kwa huduma hiyo kuchangia katika ajenda ya nchi ya kuongeza ujumuishi wa kifedha. 
 
Ndungulile aliitaka Benki ya CRDB kuendelea kutoa elimu kwa Watanzania juu ya faida ya mfumo huu wa SimBanking katika kurahisisha upatikanaji wa huduma, huku akiwahamasisha wananchi kujiunga na kuanza kufurahia huduma hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad