HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, April 2, 2021

Benki ya CRDB yaibuka Kinara Tuzo za Afrika Mashariki za Umahili wa Uandaaji Taarifa za Fedha za FiRe

Benki ya CRDB imetajwa kuwa mshindi katika tuzo za FiRe kwa upande wa Tanzania kutokana na uandaaji wa taarifa bora za matokeo ya kifedha kwa mwaka wa fedha 2020.  
 
Katika tuzo zilizofanyika tarehe 26 Machi 2021 kupitia mitandao, Benki ya CRDB pia ilitajwa kuwa mshindi wa tatu Afrika Mashariki kwa uandaaji taarifa za fedha ambapo mshindi wa kwanza ilikuwa ni Benki ya KCB na kufuatiwa na kampuni ya SCB zote za Kenya.
 

“Tuzo hizi zinadhihirisha jitihada kubwa ambazo Benki inazifanya katika kuboresha kuimarisha ripoti zetu, ili kuongeza uwazi na uwajibikaji. Sasa hivi tunatumia mfumo wa Ripoti Jumuishi ambazo zinagusa sehemu kubwa ya taarifa za biashara yetu kwa faida ya wadau wetu wote,” alisema Afisa Mkuu wa Fedha Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo akielezea sababu zilizopelekea benki hiyo kushinda tuzo hizo.
 
Aidha, Nshekanabo alisema Benki ya CRDB imefanya uwekezaji mkubwa katika mifumo ya kidijitali ikiwa ni pamoja na kuboresha mifumo ya ukusanyaji na uandaaji wa taarifa. Benki ya CRDB pia imeuunganisha mfumo wake wa utoaji taarifa za fedha na mfumo wa kimataifa wa kuandaa taarifa za fedha (IFRS), na hivyo kupelekea kuwa bora zaidi katika utoaji wa taarifa za fedha.
 
FiRe ni tuzo mashuhuri zaidi Afrika Mashariki kwa ripoti za kifedha. Tuzo ya FiRe hizi zinakusudia kukuza utoaji wa taarifa kwa njia ya kuongeza uwajibikaji, uwazi, na uadilifu. Nshekanabo alisema kuwepo kwa tuzo hizi kumesaidia kuhamasisha taasisi na mashirika ndani ya Afrika Mashariki kufuata mfumo unaofaa wa utoaji wa taarifa za kifedha.
 
Tuzo za Fire zinaandaliwa kila mwaka na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji (CMA) Kenya kwa kushirikiana na Taasisi ya Wahasibu wa Umma a Kenya (ICPAK), Soko la Hisa Nairobi (NSE) na Bodi ya Viwango vya Uhasibu wa Sekta ya Umma (PSASB) Kenya.
 
 Tuzo hii inazidi kuzihirisha ubora wa taarifa za fedha za Benki ya CRDB ikizingatiwa kuwa mwishoni mwa mwaka jana 2020, Benki ya CRDB ilitunikiwa tuzo ya taasisi ya fedha iliyoongoza kwa kuwasilisha Taarifa ya Fedha bora kwa mwaka 2018/2019 kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad