WAFANYAKAZI WANNE WA STAMIGOLD KIZIMBANI KWA MATUMIZI MABAYA YA OFISI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, February 19, 2021

WAFANYAKAZI WANNE WA STAMIGOLD KIZIMBANI KWA MATUMIZI MABAYA YA OFISI

 

Na Mwandishi wetu, Globu ya Jamii.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera
imewafikisha katika mahakama ya Wilaya ya Biharamulo watuhumiwa wanne ambao ni watumishi wa Kampuni ya Uchimbaji wa Madini  STAMIGOLD kwa makosa ya kujihusisha na vitendo dhidi ya Rushwa na matumizi mabaya ya ofisi.


Katika taarifa iliyosainiwa na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Kagera, John Joseph imesema watu hao wametumia vibaya ofisi chini ya kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupamba na na Rushwa, namba 11 ya mwaka 2007 na wamefunguliwa Shauri la jinai lenye namba CC 12/2021.


Taarifa hiyo inaeleza kuwa Watuhumiwa waliofikishwa mahakamani ni 
aliyekuwa Meneja Mkuu (General Manager) wa Mgodi wa STAMIGOLD Co Ltd katika kipindi cha mwaka 2016/2017, Dennis Joseph Sebugwao ambaye, Afisa Manunuzi wa kampuni STAMIGOLD Co Ltd katika kipindi cha mwaka 2016/2017, Bwire Kanyaranyara Eliaseph na aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi cha Mgodi wa STAMIGOLD Co Ltd kwa kipindi cha mwaka 2016/2017, Sadick Soud Kasuhya, aliye kuwa Mkuu wa Idara ya Fedha wa Kampuni ya STAMIGOLD Co Ltd, Clara Aaron Mwaikambo.

"Uchunguzi wa TAKUKURU mkoa wa Kagera umeweza kuthibitisha kuwa katika kipindi cha kuanzia 30/06/2016 hadi 31/12/2017 kwa nyakati tofauti wakiwa watumishi wa Kampuni ya STAMIGOLD CO. LTD ambayo ni Kampuni tanzu ya kampuni STAMICO (STATE MINING CORPORATION) yenye Makao Makuu yake katika Wilaya ya Biharamulo katika Mkoa wa Kagera walitumia vibaya nafasi zao na kusababisha Kampuni ya SUPERCORE kujipatia manufaa." Imeeleza taarifa hiyo.

Watuhumiwa wote kwa pamoja wakiwa waajiriwa wa Kampuni ya STAMIGOLD kwa nafasi tofauti tofauti katika kipindi cha 30/06/2016 hadi 31/12/2017 walitumia vibaya nafasi zao na hivyo kupelekea kuingiwa kwa Mktababa baina ya STAMIGOLD CO LTD na kampuni ya SUPERCORE wenye thamani ya shilingi bilioni nne milioni mia sita ishirini na mbili elfu laki nne ( Shs 4,622,400,000/=) badala ya shilingi bilioni tatu milioni mia nne elfu tisini na sita elfu (Shs 3,496,000,000/=) na hivyo kupelekea kampuni ya SUPERCORE kujipatia manufaa ya jumla ya shilingi bilioni moja milioni mia moja ishirini na sita laki nne (Shs 1,126,400,000/=)

Baada ya shauri hilo kufunguliwa, Mshitakiwa mmoja ambaye ni Clara Mwaikambo aliweza kupata dhamana na watuhumiwa wengine watatu waliobaki siku hiyo hawakuweza kutimiza masharti ya Dhamana. Hata hivyo washitakiwa wawili ambao ni Dennis Joseph Sebugwao na Bwire Kanyaranyara Eliaseph walifanikiwa kupata dhamana siku ya tarehe 16/02/2021 na Mshitakiwa Sadick Soud Kasuhya bado hajaweza kukidhi masharti ya dhamana hadi leo.

"Ikumbukwe kuwa maandiko matakatifu kutoka katika Vitabu vitakatifu hasa BIBILIA na QURAN yametamka bayana kuwa Rushwa ni dhambi, na yamekataza mtu yeyote kujihusisha na vitendo vya Rushwa kwa njia yoyote, hivyo kujihusisha na vitendo dhidi ya Rushwa ni kwenda kinyume na Makatazo ya Mwenyezi Mungu na ni kuharibu uhusiano baina yako ya Mwenyezi Mungu." Imeeleza taarifa hiyo.

Ni wajibu wa kila Mtanzania kuchukua hatua kila anapoona kuna dalili ya vitendo vya rushwa kufanyika na ni vyema kila mmoja wetu kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi zilizowekwa kwa maslahi mapana ya Taifa. Hivyo nitoe wito kwa Wananchi wote wa mkoa wa Kagera kuchukua hatua mahususi pale wanapoona kuna dalili au ukiukwaji wa sheria zetu za nchi au kuna viashiria vya uwepo wa vitendo vya rushwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad