Hospitali ya Kairuki yapima afya bure kumuenzi Mwanzilishi wake - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, February 5, 2021

Hospitali ya Kairuki yapima afya bure kumuenzi Mwanzilishi wake

 

Mwanafunzi wa mwaka wa tano wa udaktari katika Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Hubert Kairuki (HKMU),  Mayila Mbuki akimpima shinikizo la damu, Zubeda Saidi kwenye kambi ya siku nne ya kupima bure afya kwenye kituo kipya cha mabasi ya mikoani Mbezi Luis, iliyoandaliwa na hospitali ya Kairuki Mikocheni kwaajili ya kumuenzi mwasisi wa hospitali hiyo Profesa Hubert Kairuki.
2: Mtaalamu wa macho wa Manispaa ya Ubungo Dar es Salaam, Dk. Bernadeta Twinomukama akimpima macho mmoja wa wananchi waliofika kwenye kambi ya siku nne iliyoandaliwa na hospitali ya Kairuki Mikocheni kwaajili ya kumuenzi mwanzilishi wa hospitali hiyo, Profesa Hubert Kairuki.
 Joyce Riwa ambaye ni mtaalamu wa macho katika Manispaa ya Ubungo Dar es Salaam akimfanyia vipimo vya macho mmoja wa wananchi waliofika kwenye kambi ya kupima afya bure iliyoandaliwa na hospitali ya Kairuki Mikocheni kwaajili ya kumuenzi mwanzilishi wa hospitali hiyo, Profesa Hubert Kairuki aliyefariki mwaka 1999.

Na Mwandishi Wetu
MAMIA ya wananchi wamejitokeza kwa wingi kupima afya bure kwenye kambi maalum inayoendeshwa na hospitali ya Kairuki Mikocheni kwa kushirikiana na Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Kambi hiyo iliyoanza Jumatano, wiki hii katika kituo cha mabasi Mbezi Luis jijini Dar es Salaam, inatarajiwa kufungwa Ijumaa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo,  Kisare Makori.

Baadhi ya huduma zinazotolewa kwenye kambi hiyo ya siku nne ni upimaji wa macho, sukari, shinikizo la damu, elimu ya lishe bora, dalili za awali za saratani ya matiti, kuchangia damu na elimu ya umuhimu wa bima ya afya.

 Mwanabinti Hamis ambaye ni mmoja wa waliopata huduma ya upimaji wa sukari na shinikizo la damu, ameishukuru hospitali ya Kairuki kwa kutoa huduma hiyo bure na kushauri utaratibu huo uwe endelevu.

Amesema wananchi wengi wanashindwa kwenda kupima afya zao na kupata elimu kuhusu namna ya kujikinga na maradhi ya kuambukiza kwa kuwa wengi wao hawana uwezo wa kugharamia vipimo kwenye hospitali.

“Nimepima sukari iko juu na kabla ya hapa sikuwa najua kwasababu sikuwahi kupima ila niliposikia Kairuki wanapima bure ndipo nikawahi mapema na kweli nimehudumiwa pamoja na vipimo vya presha ambayo wamesema iko kawaida,” alisema

Kwa upande wake,  Mohamed Issa mkazi wa Kimara aliyepimwa saratani ya matiti aliwataka wanaume wajitokeze kwa wingi kupima ugonjwa huo na kuachana na dhana iliyojengeka miongoni mwao kuwa ugonjwa huo huwapata wanawake pekee.

“Nimepima nimeambiwa niko vizuri hivyo ni vyema ukapima afya yako kujua kama uko salama, ukipima na ikagunduika kwamba uko salama haikugharimu kitu kuliko ukadhani uko salama kumbe saratani ya matiti inakutafuna kidogo kidogo na huduma yenyewe hapa ni bure,” alisema

Naye, Kaimu Meneja Uhusiano na Masoko wa hospitali hiyo ya Kairuki, Arafa Juba amesema kambi hiyo hufanyika kila mwaka kwa ajili ya kumuenzi mwanzilishi wa hospitali hiyo, hayati Profesa Hubert Kairuki na kusema mbali na kupimwa, wananchi wanaofika kwenye kambi hiyo wamekuwa wakipata ushauri wa kitabibu kutoka kwa madaktari wa hospitali hiyo wa namna ya kwenda kutibu maradhi yanayowasumbua.

“Tunawapima pia wenye uoni hafifu na kwa wale wanaohitaji miwani tunawapa miwani bure. Pia tumefanikiwa kuhamasisha wananchi wengi wajiunge na bima ya afya iliyoboreshwa (CHF), “amesema Arafa.

Alisema hayati Profesa Kairuki aliyefariki Februari 6 mwaka 1,999, licha ya kuwa mwanzilishi wa hospitali hiyo ni mwanzilishi pia wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU) na Shule Kuu ya Uuguzi ya Kairuki na pia Profesa Kairuki ni mwanzilishi wa Mtandao wa Shirika la Afya na Elimu (KHEN), ambapo pia umeanzisha kiwanda  cha kutengeneza dawa, Kairuki Pharmaceuticals Industry kilichoko Zegereni Kibaha.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad