HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, February 5, 2021

GePG YAPAISHA MAPATO TANAPA NA MAMLAKA YA MAJI JIJI LA ARUSHA

 

 

Afisa Mwandamizi wa Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Afande Boniphase Maliki, akieleza kuwa Shirika lilikua na Akaunti 100 na baada ya kujiunga na Mfumo wa Makusanyo ya malipo ya Serikali (GePG), imebaki na akaunti 8, wakati Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini walipotembelea Shirika hilo, jijini Arusha.

Afande Juma Kuji, (wa pili kulia) akiwa na maafande wengine wakisikiliza kwa makini maswali ya Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini kuhusu Mfumo wa GePG ulivyosaidia katika makusanyo.

Mkuu wa Usajili wa Wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Arusha, Dkt. Baraka Kichonge (wa kwanza kushoto), akiwa kwenye mkutano na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini waliofika katika Chuo hicho kuangalia mafanikio ya Mfumo wa GePG, jijini Arusha.

Mkuu wa Usajili wa Wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Arusha, Dkt. Baraka Kichonge, akiipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, kwa kuanzisha Mfumo wa Malipo ya Serikali kwa njia ya Kielektroniki (GePG), ambao umeongeza makusanyo na kurahisisha utendaji wa kazi.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja, akielezea jambo, walipotembelea Chuo cha Ufundi Arusha, kuangalia namna Mfumo wa Malipo ya Serikali kwa njia ya Kielektroniki (GePG) unavyofanya kazi, wakati wa ziara ya Wahariri wa Vyombo vya Habari katika Chuo hicho.

Mkuu wa Kitengo cha Tehama wa Mamlaka ya Maji jijini Arusha Bw. Tito Ndaki akielezea kuongezeka kwa mapato ya mwezi kutoka Sh. bilioni 1.2 hadi bilioni 1.6 baada ya kuanza kwa matumizi ya Mfumo wa Malipo ya Serikali kwa njia ya Kielektroniki (GePG).

Mtaalamu wa Uchumi wa Wizara ya Fedha na Mipango. Bi. Neema  Maregeli akifafanua jambo, katika ziara ya Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini katika  Chuo cha Ufundi Arusha.

(Picha na Ramadhani Kissimba, WFM, Arusha

…………………………………………………………………………………….

Na. Ramadhani Kissimba na Peter Haule, WFM, Arusha

Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imefanikiwa kuongeza mapato maradufu baada ya kuanzisha matumizi ya mfumo wa kukusanya mapato ya Serikali (GePG), ambapo mpaka sasa taasisi zaidi ya 670 zimekwishajiunga katika mfumo huo.

Hayo yamebainishwa leo baada ya ziara iliyofanywa na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini walipotembelea Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) na Mamalaka ya Maji Safi na Maji Taka mkoa wa Arusha, (AUWASA).

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Afande Juma Mussa Nasoro Kuji Kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa, (TANAPA) amesema tangu kuanzishwa kwa mfumo wa makusanyo wa pesa za serikali, shirika hilo limeokoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo zilikuwa zikitumika kuwalipa watoa huduma kutoka benki mbalimbali. Afande Kuji alisema TANAPA ilikuwa ikilipa asilimia moja ya mapato yote wanayokusanya kwa mabenki hayo, ambazo ni kati ya shilingi bilioni moja hadi bilioni tatu kwa mwaka. Na sasa hakuna malipo yoyote yanayofanyika kwa benki hizo kutokana na matumizi ya mfumo wa GePG.

Akizungumzia mafanikio ya TANAPA baada ya kuunganishwa na mfumo wa GePG, Mkuu wa Kitengo cha Tehama Afande Boniphase Mariki alisema kuwa kabla shirika hilo halijaanza kutumia mfumo huo kila geti la hifadhi lilikuwa na akaunti yake hivyo kusababisha shirika hilo kuwa na akaunti zinazokaribia mia moja (100), jambo ambalo lilikuwa linachelewesha kupata taarifa za makusanyo na ufanyaji wa usuluhishi wa kifedha (Bank reconciliation).

Afande Maliki aliongeza kuwa baada ya kujiunga na GePG kwa sasa shirika lina akaunti nane (8) tu ambazo akaunti nne (4) ni za sarafu ya Shilingi na akaunti nne (4) ni za sarafu ya Dola, jambo linalowezesha shirika kutatua changamoto nyingi za makusanyo kwa kuwa makusanyo yote yanasimamiwa na mfumo wa GePG. 

Aidha akiwakaribisha wahariri na watumishi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Afande Kuji alisema TANAPA walianza na hifadhi moja ya Serengeti mwaka 1959 na mpaka sasa wana hifadhi 22 nchini kote.

Katika ziara hiyo wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini pia walipata fursa ya kutembelea katika chuo cha Ufundi Arusha na Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Mkoani Arusha ambapo walipata taarifa jinsi mfumo wa GePG ulivyosaidia kurahisisha makusanyo kwa Taasisi hizo na kupunguza usumbufu kwa wateja.

Akizungumzia mafanikio hayo Mkuu wa Kitengo cha Tehama wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Mkoani Arusha, Bw. Ndaki Titto alieleza kuwa baada ya kujiunga na mfumo huo katika mwaka wa fedha 2017/18 shirika hilo limefanikiwa kuongeza mapato yake kutoka shilingi bilioni 1.2 hadi bilioni 1.6 kwa mwezi.

Bw. Titto amesema kuwa mbali na shirika kuongeza mapato yake, pia wateja wamefaidika kwa kiasi kikubwa kwa sababu mfumo wa GePG umeruhusu kufanya malipo kupitia njia mbalimbali zikiwemo mitandao ya simu hivyo kupunguza usumbufu kwa wateja wake. Bw. Ndaki amesema kuwa pamoja na mafanikio hayo kuna changamoto wanazokumbana nazo kupitia mfumo huo wa GePG ikiwemo changamoto ya mtandao.

‘’Changamoto ninayoiona kwa upande wa GePG ni utegemezi zaidi kwa upande wa mtandao, maana bila ya mtandao huwezi kuona mapato na changamoto nyingine ni elimu kwa wananchi, ambapo wananchi wengi hawana uelewa kuhusu matumizi ya namba ya malipo (control number) kuwa unaweza kulipia katika benki yoyote’’ aliongeza Bw. Titto.

Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa chuo cha Ufundi Arusha, Mkuu wa Usajili wa wanafunzi Dk. Baraka Kichonge amesema kuwa mfumo wa ukusanyaji mapato ya serikali (GePG) umekuwa mkombozi wa matumizi ya fedha za umma kwa kuwa mfumo huo umeweka uwazi katika makusanyo na hivyo kuongeza uadilifu katika matumizi ya fedha za Umma.

Aidha Dk. Kichonge amewaomba wahariri hao kufanya ziara ya mkakati katika chuo hicho ili kujionea teknolojia kubwa inayotumika katika ufundishaji chuoni hapo na kuzifikisha taarifa hizo kwa wananchi ili waweze kuwekeza katika teknolojia kupitia vijana wao watakaowapeleka kupata mafunzo katika chuo hicho.

Kwa Upande wa Wizara, Afisa Tehama Mwandamizi anayesimamia Mfumo wa GePG Bw. Basil S. Baligumya alisema katika semina ya siku mbili kwa wahariri Wizara imepata zaidi ya kujifunza kuhusu ufanyaji kazi wa mfumo wa GePG. Bw. Basil aliongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa sapoti kwa taasisi zake kuhakikisha kwamba changamoto zozote za mifumo zinatatuliwa kwa wakati.

‘’Sisi kama Wizara tupo tayari kuendelea kuwapa sapoti na tunashukuru kwa ushirikiano wenu pia na tunaendelea kuwatia moyo ile mifumo yenu inayochakata bili muendelee kuiboresha ili tuendelee kutoa huduma kwa namna ambayo ni rahisi kwa watu wanaolipia huduma zetu” alisema Bw. Basili.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad