WANANCHI KATA YA WINO-MADABA WAJENGA BWENI LA WAVULANA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 18, 2021

WANANCHI KATA YA WINO-MADABA WAJENGA BWENI LA WAVULANA

 

 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya  ya Madaba mkoani Ruvuma Theofanes Mlelwa mwenye shati la kitenge akishiriki ujenzi wa Bweni la wavulana katika shule ya sekondari Wino linalojengwa kwa nguvu za wananchi  na kwa kushirikiana na Serikali ambayo imetoa kiasi cha shilingi milioni 80 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya viwandani,kushoto mkuu wa shule hiyo Benaya Mkumba.Picha na Muhidin Amri

……………………………………………………………………………….

Na Muhidin Amri,Madaba

KUTOKANA  na uhaba  mkubwa wa Mabweni unaowakabili wanafunzi wa  shule ya Sekondari Wino Halmashauri ya wilaya Madaba,Wananchi kata ya Wino  yenye vijiji vitatu vya Wino,Lilondo na Igwisenga  wameanza ujenzi wa Bweni  moja la wavulana  litakalokuwa na uwezo wa kuchukua watoto 80.

Kutokana na uhitaji mkubwa wa mabweni katika  shule hiyo  wanafunzi  hasa wa kiume kwa sasa wanalazimika kupanga vyumba uraini jambo lililochangia sana kushuka kwa taaluma na morali ya kujisomea kwa wanafunzi  .

Akizungumza  katika eneo la ujenzi Afisa Mtendaji wa  wa Serikali ya kijiji cha Wino Sholastika Mkanula amesema, wananchi wamehamasika kujitokeza kuchangia nguvu zao na vitu  mbalimbali  katika  ujenzi wa bweni  ili  kupunguza  tatizo la sehemu ya kulala  wanafunzi  wa kiume.

Alisema, katika  ujenzi wa bweni la wavulana wananchi kupitia mitaa yao kila mmoja amehamasika kwa kuleta mawe,matofali na mchanga kwa ajili ya ujenzi huo .

Hata hivyo,amewaomba wadau wengine wa maendeleo  kutoka maeneo mbalimbali kuwaunga mkono kwa kuchangia ujenzi bweni hilo ambalo mara litakapokamilika litachangia  sana kurudisha morali ya kujisomea na kupanda taaluma  kwa wanafunzi na shule kwa jumla .

Alisema,kitendo  cha wananchi wake kujitokeza kushiriki kwa hali na  mali ujenzi huo kimemtia moyo na kuhaidi kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho Hezron Mwageni amesema,mradi huo ulianza tangu mwezi 8 ambapo wananchi walitakiwa kuchangia nguvu zao kwa kuchimbi msingi,kuleta mawe,matofali na mchanga jambo ambalo wamelitekeleza kwa kiwango kikubwa.

Alisema, wananchi  wameamua kuunga mkono juhudi za Serikali ili kuhakikisha watoto wa kiume katika shule hiyo nao wanakuwa na mazingira mazuri na salama ya kuishi na kuwataka wananchi ambao bado hawajachangia wanafanya hivyo ili kuwezesha watoto wao kuishi katika mazingira mazuri na kutimiza ndoto zao.

Mkuu wa shule hiyo Benaya Mkumba amesema,  kwa sasa shule ya Sekondari Wino ina uhitaji wa mabweni 4 kwa ajili ya wavulana  na yaliyopo 4 ambayo yanatumika kwa wasichana,  kwa hiyo  kujengwa kwa bweni hilo kunakwenda  kupunguza mahitaji ya mabweni kwa wanafunzi wa kiume .

Alisema, katika ujenzi huo Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 80 kwa ajili ya kununua vifaa vya viwandani  na mara litakapokamilika  litasaidia  kuinua  taaluma na kujenga nidhamu ya wanafunzi wenyewe hasa ikizingatia kuwa vijana wengi wa kiume wanaishi nje ya eneo la shule.

Alisema, jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 lakini kutokana na uhitaji mkubwa wa sehemu ya kulala, kuna uwezekano mkubwa idadi hiyo itaongezeka na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kuunga mkono jitihada za wananchi na serikali kwa jumla.

Naye AfisaMtendaji wa kata  ya Wino Hans Pope, ameishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 80 ambazo zitatumika kununua vifaa vya viwandani, ambapo alisema bweni litakapokamilika litaleta tija kubwa ya kupunguza tatizo la malazi kwa wanafunzi wa kiume.

Amewataka Watanzani, kuhakikisha wanashirikiana na Serikali yao katika ujenzi wa miradi na shughuli  mbalimbali  za maendeleo ili  kumaliza baadhi ya kero za muda mrefu, badala ya kuichia Serikali kufanya kila jambo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Madaba Shafi Mpenda alisema,  baadhi ya shule za sekondari ikiwemo Wino  zinakabiliwa na upungufu  wa mabweni,hata hivyo mkakati uliopo ni kuhakikisha  shule zote za sekondari kuna mabweni ya kutosha.

Kwa mujibu wa Mpenda,changamoto kubwa ni ukosefu wa fedha na kuwaomba wadau mbalimbali wakiwemo wazazi na jamii kwa jumla kujitolea kusaidia katika kuwezesha mpango wa kuimarisha na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kujifundishia.

Amempongeza diwani wa kata ya Wino  na Mwenyekiti wa Halmashauri  hiyoTheofenasi Mlelwa kwa ushiriki na kufuatilia kwa karibu ujenzi wa bweni hilo.No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad