Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi Hati ya
Ardhi aliyekuwa Waziri wa Ujenzi ambaye sasa ni Mbunge wa Jimbo la
Katavi Isack Kamwelwe akiwa katika ziara yake ya kikazi kukagua utendaji
kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Tanga tarehe 7 Januari 2021.
Kushoto ni Meya wa Jiji la Tanga Abdulrahman Shiloow.

Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimsikiliza Mkuu wa
Mkoa wa Tanga Martine Shigela (Kushoto) na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi
ambaye sasa ni Mbunge wa Katavi Isack Kamwelwe alipowasili kwa ziara ya
siku moja katika mkoa wa Tanga kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi
tarehe 7 Januari 2021. Wa pili kulia ni Mkuu wa wilaya ya Tanga Thobias
Mwilapwa.

Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza katika
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kabla ya kuzungumza na watendaji wa sekta
ya ardhi kwenye mkoa huo na kugawa hati za ardhi kwa wakazi wa jiji la
Tanga akiwa katika ziara yake ya kikazi tarehe 7 Januari 2021. Aliye kaa
mbele ni Mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shigela.
…………………………………………………………………….
Na Munir Shemweta, WANMM TANGA
Naibu Waziri wa Ardhi
Dkt Angeline Mabula amewataka watendaji wa sekta ya ardhi nchini
kufanya utafiti sababu zinazowafanya wamiliki wa ardhi kushindwa
kujitokeza kuchukua hati za ardhi zilizokamilika.
Dkt Mabula alitoa
kauli hiyo leo tarehe 7 Januari 2021 katika ukumbi wa Halmashauri ya
jiji la Tanga wakati akigawa Hati za Ardhi kwa wakazi wa Jiji hilo akiwa
katika ziara yake ya siku moja katika mkoa huo kukagua utendaji kazi wa
sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia
kodi ya pango la ardhi.
Dkt Mabula alisema,
ni lazima watendaji wa sekta ya ardhi nchini kuanza kujiuliza tatizo
liko wapi mpaka wamiliki wa ardhi ambao hati zao zimekamilika
wanashindwa kujitokeza kuzichukua hati zao katika ofisi za Wasajili wa
Hati Wasaidizi kwenye Ofisi za Ardhi za Mikoa.
Kwa mujibu wa Naibu
Waziri Mabula, kati ya wamiliki wa ardhi 80 waliotaarifiwa kwenda
kuchukua hati zao zilizokamilika katika Halmashauri ya jiji la Tanga ni
wamiliki 8 tu waliojitokeza kuzichukua jambo alilolieleza kuwa siyo
sahihi.
Aliwataka watendaji
wa sekta ya ardhi kuwahimiza wamiliki wa ardhi wakati wa kuandaliwa hati
kwenda kuchukua hati kwa wakati sambamba na kuwakumbusha masharti ya
umiliki kama vile viwango wanavyotakiwa kulipa kama kodi ya pango la
ardhi pamoja na kuendeleza kiwanja ndani ya miaka 3.
“Ukichukua Hati
unaongeza thamani ya eneo lako maana usipochukua kunakuwa na masharti
mengi wakati wa kutaka kuuza, eneo la milioni 20 unaweza kuliuza kwa
milioni 5 huku anayelinunua anaweza kuliuza hata kwa milioni 200 ”
alisema Dkt Mabula.
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula aliongeza kwa kusema, kwa sasa
Watendaji wa Wizara yake wanafanya kazi kama mchwa ili kuhakikisha
mambo wanayopanga yanafanyika kwa mafanikio makubwa.
Mmoja wa wananchi
waliopatiwa Hati na Naibu Waziri Dkt Mabula mkoani Tanga ni aliyekuwa
Waziri wa Ujenzi ambaye sasa ni Mbunge wa Jimbo la Katavi Mhandisi Isack
Kamwele ambaye aliipongeza Wizara ya Ardhi kwa utaratibu iliyouanzisha
ya kuwapigia simu wamiliki wa ardhi ambao hati zao zimekamilika.
“Mimi nilipigiwa simu
na ofisi ya Ardhi mkoa kuelezwa kuwa hati yangu iko tayari, uamuzi wa
kupigiwa simu ni utaratibu mzuri na hii sasa ni dunia ya kwanza na
tukiendelea na utaratibu huu basi malalamiko yatapungua sana ila naomba
muongeze kasi katika utoaji vibali vya ujenzi” Alisema Mhandisi Kamwele.
No comments:
Post a Comment