HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 18, 2021

HALMASHAURI YA MADABA YAKAMILISHA JENGO LA UTAWALA

 

 Na Muhidin Amri,Madaba

MKURUGENZI wa Halmashauri ya wilaya Madaba mkoani Ruvuma Shafi Mpenda amesema, ujenzi wa jengo la utawala kwa ajili ya watumishi wa Halmashauri hiyo hadi sasa limekamilika kwa asilimia 99.

Mpenda amesema hayo jana wakati akizungumza na Habarileo ofisini kwake  na  kumshukuru Rais Dkt John Magufuli kwa  kutoa kiasi cha shilingi bilioni 3 kwa ajili  ujenzi wa jengo hilo ambalo kwa sasa limesaidia sana watumishi wa idara mbalimbali kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi mkubwa.

Alisema,walipokea fedha za mradi  kwa mafungo ambapo  mwaka 2016 walipokea shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga msingi na nguzo za kusimamisha kuta za jengo.

Mpenda alibainisha kuwa,ujenzi rasmi ulianza Mwezi Septemba 2017 baada ya kusaini mkataba na wakala wa majengo Tanzania(TBA) wa shilingi milioni 493 na shilingi milioni 7 zilitumika kwa ajili ya kufanya vipimo vya udongo kwenye eneo la mradi.

Alisema,  Halmashauri  kupitia mapato yake ya ndani ilihusika kulipa fidia ya shilingi milioni 6.78 kwa wananchi waliokuwa wamiliki halali wa eneo  lililotumika kujenga jengo.

Hata hivyo, Serikali iliendelea kutoa fedha  na kufikiwa kiasi cha shilingi bilioni 3 ambazo mpaka sasa Halmashauri imeshazipokea na kutumia shilingi bilioni 2.9  na kubakiwa milioni 85.

Aidha alisema, Mwezi Mei 2020 Halmashauri ililazimika kuvunja mkataba na Tba kutokana na changamoto zilizojitokeza ikiwemo kusua sua kwa ujenzi wa mradi huo ambapo TBA ilijenga Boma tu, hivyo Halmashauri iliomba  kibali Tamisemi kwa ajili ya kumalizia ujenzi kwa kutumia mafundi wa ndani(force account)kwa kuamini kwamba utaratibu huo utasaidia kukamilisha mradi.

Kwa mujibu wa Mpenda,baada ya kuomba kibali cha Katibu Mkuu Tamisemi na Halmashauri iliendelea kujenga jengo hilo kwa mfumo wa force Akaunti ambao kimsingi umefanikisha  kumaliza jengo hilo  haraka na idara zote zimeshahamia.

Alisema,walilazimika kuhamia mapema hasa baada ya kupokea watumishi wengi na  jengo walililokuwa wanalitumia ni dogo,na hata usalama wa nyaraka za serikali na usalama wa watumishi ulikuwa mdogo hivyo kushindwa kutekeleza baadhi ya majukumu.


Alisema,  ni faraja kubwa  kuona sasa watumishi wanachapa kazi ya kuwahudumia wananchi  wa jimbo la Madaba na maeneo mengine ya nchi  licha ya kutokamilika kwa asilimia 100 ambapo kazi ndogo ndogo zilizobaki  zinafanyika wakati wakitumishi wakiwa katika jengo hilo  na kazi zilizobaki ni  kufunga milango, na marekebisho kwa maeneo ya nje kabla ya fundi kurudia kupaka rangi  ya mwisho.

Alisema, fedha zilizobaki wameamua kujenga kibanda cha mlinzi  aweze kufanya kazi katika mazingira mazuri,kujenga kantini ili  kuwasaidia watumishi kupata huduma ya chakula karibu na kuokoa muda wa kazi wa mwajiri ili watumishi wasipate sababu ya kwenda umbali mrefu na kuchelewa kurudi kuchapa kazi.

Alisema,  kukamilika kwa jengo hilo kunakwenda kuchochea morali ya watumishi kufanya kazi kama ilivyo dhamira ya serikali ya awamu ya tano na watumishi kuchochea mahudhurio kazini  tofauti na siku za ambapo jengo lililotumika lilikuwa dogo na kuvunja hali ya uwajibikaji kwa watumishi.

Pia alisema, sasa kumekuwa na usiri mkubwa kwa watumishi pale anapotekeleza majukumu yake  sambamba na kusaidia mtumishi kuona ufahari kuitanga vyema Halmashauri na Serikali  ya awamu ya tano kwani jengo hilo lina huduma zote muhimu.

Mpenda alieleza kuwa, jengo hilo limebadilisha taswira  na kuongeza  thamani ya eneo hilo na  sasa wananchi wanaweza kujenga nyumba kwa ajili ya kupangisha watumishi watakopenda  kuishi karibu na ofisi.

Amewataka wananchi kutumia fursa ya kuwepo kwa jengo hilo kujenga nyumba za kisasa,kujenga Hoteli,kumbi za sterehe na miradi mingine ya kuwaingizia kipato kwa sababu Serikali imeshasogeza fursa katika meoneo yao.

Sehemu ya Jengo la Utawala la Halmashauri ya wilaya Madaba mkoani Ruvuma likiwa limekamilika kwa asilimia 99 na limeanza kutumika kwa watumishi wa Halmashauri hiyo kutekeleza majukumu yao ya kila siku.Jengo hilo limegharimu zaidi ya shilingi bilioni 3 linakusudia kuboresha mazingira ya kufanyia kazi watumishi. Picha na Muhidin Amr

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad