HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, December 23, 2020

WAJASIRIAMALI WATAKIWA KUWEKEZA KWENYE DHAMANA ZA SERIKALI


WAJASIRIAMALI na wadau wa maendeleo wametakiwa kuwekeza kwenye dhamana za serikalini ili wapate faida wao wenyewe na serikali kwa ujumla kuliko kutegemea miradi mingine ikiwemo nyumba za kupangisha.

Pamoja na kupata faida binafsi pindi wakiwekeza kwenye dhamana hizo, serikali pia itanufaika kwa kutumia fedha hizo za uwekezaji katika kujenga na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwa jamii.

Kamishna msimamizi wa madeni wa Wizara ya Fedha na Mipango, Lekinyi Mollel ameyasema hayo jijini Arusha, wakati akizungumza na wadau mbalimbali wa ujasiriamali kwenye semina ya kuwajengea uwezo. 

Mollel amesema pamoja na kuwekeza katika dhamana za serikali fedha za wajasiriamali hao hazitakuwa kwenye viashiria hatarishi.

Amesema huu ni wakati muafaka kwa wajasiriamali, wenye viwanda, wafugaji, wakulima, wadau wa madini na sekta nyingine kuwekeza kwa wingi kwenye dhamana za serikali.

Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha, Richard Kwitega amesema wananchi wanaponunua dhamana hizo za serikali hupata faida baada ya vipindi mbalimbali ikiwemo miezi sita na mwaka mmoja.

Kwitega amesema dhamana hizo za serikali ni rafiki kwani mwekezaji ana uhuru wa kuuza dhamana sake muda wowote akihitaji kufanya hivyo.

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja amesema uanzishwaji wa minada ya dhamana za serikali ni mkakati wa kuendeleza masoko ya fedha nchini.

Mwaipaja amesema dhamana za serikali zimegawanyika katika makundi mawili ya dhamana za muda mfupi isiyozidi mwaka mmoja na hatifungani zinazotumiwa na serikali za miaka miwili hadi 20.

Katibu mkuu wa wafanyabiashara wa madini, Noel Olevaroya amesema atakuwa balozi mzuri kwa wachimbaji madini na wafugaji katika kufikisha elimu ya uwekezaji wa dhamana za serikali.

"Sisi wafanyabiashara wa madini tuna uwezo wa kuwekeza katika dhamana hizo na pia wafugaji tuna mifugo mingi hivyo ili kufuga kitaalamu tutaifikisha elimu hii kwao," amesema Olevaroya.

Mjasiriamali Theresia Onesmo amesema kupitia elimu hiyo ya uwekezaji kwenye dhamana za serikali ataachana na mpango wa kujenga nyumba za kupangisha na kuwekeza kwenye dhamana za serikali.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega akifungua semina ya kuwajengea uwezo wajasiriamali juu ya namna ya kuwekeza kwenye dhamana za Serikali.
Mjasiriamali wa jijini Arusha, John Mollel akizungumza kwenye semina ya Wizara ya Fedha na Mipango ya namna ya kuwekeza kwenye dhamana za Serikali.
Kamishna msaidizi wa madeni Wizara ya Fedha na Mipango, Lekinyi Mollel akizungumza na wadau wa maendeleo jijini Arusha, juu ya kuwekeza kwenye dhamana za Serikali.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad