HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 23, 2020

‘BARABARA YA RUANGWA - KIRANJERANJE KUWA YA LAMI’

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Serikali ya CCM imepanga kujenga barabara ya kutoka Ruangwa hadi Kiranjeranje kwa kiwango cha lami.

 

Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Oktoba 23, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa vijiji na kata mbalimbali za wilaya ya Ruangwa ambako alipita kumuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli na madiwani wote wa kata hizo.

 

Akizungumza na wakazi hao kwa nyakati tofauti, Mheshimiwa Majaliwa amesema barabara hiyo imo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM na tayari sh. bilioni 1.2 zimeshatolewa ili kufanya upembuzi yakinifu na usanifu. Barabara hiyo itawafanya wakazi hao wasilazimike kupitia Nanganga hadi Lindi wanapotaka kwenda Dar es Salaam.

 

"Barabara ya kutoka Ruangwa - Nanjilinji - Kiranjeranje ina urefu wa km.120. Barabara hii ukiangalia kwenye ilani yetu, utaikuta iko uk.75. Barabara nyingine ni ya kutoka Ngongo – Mandawa – Namichiga yenye urefu wa km 85 na hii ilipatiwa sh. milioni 800 na kazi ya upembuzi yakinifu imekwishakamilika, sasa kazi iliyobaki ni kutafuta fedha na kuanza ujenzi,” amesema.

 

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ambaye ni mbunge mteule wa jimbo la Ruangwa, amesema katika kipindi cha miaka mitano, wilaya hiyo imepokea zaidi ya sh. bilioni 100 kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

 

“Haijawahi kutokea. Tangu wilaya hii ianzishwe mwaka 1995, imekuwa ikipokea fedha za maendeleo kati ya sh. bilioni 3 hadi bilioni 4 tu. Lakini awamu hii tumepokea shilingi bilioni 49.5 kwa ajili ya kazi za maendeleo na hivi karibuni Mheshimiwa Dkt. Magufuli alitoa sh. bilioni 59 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Nanganga- Ruangwa kwa kiwango cha lami.”

 

Katika vijiji vyote alivyosimama na kazta za Mandawa, Chikundi, Namichiga na Mbekenyera, Mheshimiwa Majaliwa amewasihi wakazi hao kuwa ifikapo Jumatano ijayo wajitokeze kwa wingi na kupiga kura za ndiyo kwa Dkt. Magufuli na madiwani wa CCM.

 

“Sisi sote ni wana-Ruangwa na kikubwa tunachotaka ni maendeleo, na maendeleo hayachagui chama. Kwani tukijenga barabara, si tutatumia wote? Fanyeni maamuzi sahihi kwa kukichagua Chama cha Mapinduzi na kumpa kura nyingi Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,” amesisitiza.

 

Wakati huohuo, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa Ruangwa kwa kumpitisha bila kupingwa wakati akiwania ubunge wa jimbo hilo. Bado anaendelea na ziara yake kwenye jimbo la Ruangwa.

 

   

IMETOLEWA:

IJUMAA, OKTOBA 23, 2020.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad