HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, September 23, 2020

TUMIENI USULUHISHI KUMALIZA MASHAURI: JAJI MKUU

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwasili Mahakama ya wilaya ya Manyoni kuanza ziara ya siku tatu mkoani humo kukagua shughuli za Mahakama. 
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Manyoni katika ziara yake mkoani Singida. 
Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Manyoni wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipokuwa akizungumza nao alipowasili kwenye Mahakama hiyo kukagua kazi za utoaji Haki. Jaji Mkuu ameanza ziara ya siku tatu mkoani Singida. 

……………………………………………………………………….. 

Na Lydia Churi-Mahakama, Singida 

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Majaji na Mahakimu nchini kuongeza matumizi ya njia ya usuluhishi katika kusikiliza na kumaliza mashauri hususan mashauri yanayohusu Mirathi. 

Akizungumza na watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Manyoni mkoani Singida katika siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi mkoani humo Jaji Mkuu amesema mashauri yanayohusu Mirathi yana changamoto nyingi hivyo njia ya usuluhishi itasaidia kurahisisha usikilizwaji wa mashauri hayo. 

Amewataka Majaji na Mahakimu kusimamia kikamilifu kuhakikisha wale wanaofungua mashauri hayo mahakamani wanawasilisha taarifa za mirathi na wanafunga hesabu ili ile dhana ya kuwa msimamizi wa mirathi ndiye atakayefaidika na mirathi na ambayo ndiyo inayochochea migogoro inaondoka. 

“Tujaribu kutumia usuluhishi kwani njia hii pia itasaidia kupunguza mashauri mahakamani. Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawahimiza Majaji na Mahakimu kumaliza mashauri kwa njia usuluhishi”, alisema Jaji Mkuu. 

Jaji Mkuu amesema Majaji na Mahakimu wakiweza kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kutatua migogoro hiyo nje ya Mahakama itakuwa ni rahisi kuyashughulikia mashauri ya aina hiyo. 

Akizungumzia suala la maadili kwa watumishi wa Mahakama, Jaji Mkuu amewataka watumishi hao kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi na kufuata utaratibu kwani kwa kufanya hivyo watarejesha Imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama. 

Alisema watumishi wa Mahakama ya Tanzania wenye kada za uhudumu, watunza kumbukumbu, walinzi na wengineo ndiyo kioo cha Mahakama na endapo watafanya kazi weledi mtazamo dhidi ya Mahakama utakuwa chanya wakati wote. 

Kuhusu mabaraza ya Ardhi, Jaji Mkuu amesema azma ya serikali ya kuyarudisha mabaraza hayo mahakamani bado ipo hivyo amewataka watumishi wa Mahakama kujiandaa kuyapokea mabaraza hayo. 

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu amewataka Mahakimu kuwa makini katika kusimamia Sheria, Kanuni na taratibu na kuhakikisha mshtakiwa anapokamatwa anafikishwa mahakamani ndani ya saa 48. Jaji Mkuu pia amewataka Mahakimu hao kuwakumbusha viongozi husika kuzingatia Sheria kanuni na taratibu wanapowakamata watuhumiwa. 

Alisema lengo la ziara yake ni kuzielezea changamoto wanazokutana nazo Majaji wa Mahakama ya Rufani wanaposikiliza mashauri. Moja ya changamoto hizo ni mapungufu yanayojitokeza wakati wa kuwakamata watuhumiwa. Vikao vya Mahakama ya Rufani vilianza Septemba 14, Mahakama Kuu kanda ya Dodoma na vitamalizika Septemba 28, mwaka huu. 

Jaji Mkuu ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu katika Mkoa wa Singida ambapo atakagua shughuli mbalimbali za Mahakama.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad