*Ni baada ya Serikali kujenga mradi mkubwa wa sh Bil. 40
MJUMBE
wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa amesema changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama
wilayani Simanjiro kuwa historia baada ya Serikali kujenga mradi mkubwa
wa maji kutoka Mto Ruvu hadi Orkesumet wenye thamani ya sh bilioni 40.
“Mradi
huu umefikia asilimia 89 za utekelezaji na unatarajiwa kuanza kufanya
kazi mwishoni mwa mwezi huu wa Septemba 2020 au mapema Oktoba 2020. Pia
Serikali imetekeleza miradi mingine ya maji ikiwemo ya uchimbaji ya
mabwawa ya kunyweshea mifugo ambayo tayari inatoa huduma kwa wananchi.”
Ameyasema
hayo leo (Ijumaa, Septemba 4, 2020) alipohutubia mkutano wa kampeni
uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Orkesumet wilayani
Simanjiro mkoani Manyara wakati akimuombea kura Rais Dkt. John Pombe
Magufuli na mgombea ubunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole
Sendeka na wagombea udiwani.
Amesema
miradi mingine inayotekelezwa katika wilaya hiyo ni pamoja na uchimbaji
wa visima virefu vya maji 18 katika maeneo ya Kitwai, Msitu waTembo,
Mirerani, Londrekes, Loibosoit, Kityangare Namalulu, Terrat, Olbili,
Nadonjukin na Okutu. Ukarabati wa visima 13 umefanyika kikamilifu
hatimaye vituo vya kuchotea maji vimefikia 95.
“Ujenzi
wa bwawa la Narakauo kwa ajili ya matumizi ya mifugo na wananchi wa
vijiji vya karibu yake unaendelea kupitia Wizara ya Mifugo kwa gharama
ya sh. 413,865,700 sawa na asilimia 36.”
Waziri
Mkuu amesema mradi huo utakuwa mkombozi mkubwa kwa wafugaji wa ukanda
wote wa Simanjiro ya juu. Pia Serikali imetumia sh. 412,724,300
kutekeleza mradi wa maji kutoka Nomokon hadi Narakauo ambao pia
utasaidia kupunguza uhaba wa maji kwa wafugaji wa Kata nzima ya
Loibosiret.
Amesema
licha ya utekelezaji wa miradi ya maji pia, Serikali imetenga shilingi
milioni 500 kwa ajili kuboresha barabara za mjini katika Halmashauri ya
wilaya hiyo na zile za makao makuu ya wilaya (Orkesumet) ambazo
zinaendelea kuwekewa lami. “WanaSimanjiro endeleeni kukiamini Chama
chenu Cha Mapinduzi kwa kuchagua wagombea wote wa CCM ili mpate
maendeleo zaidi.”
Akizungumzia
kuhusu nishati ya umeme, Mheshimiwa Majaliwa amesema kati ya vijiji 56
vya wilaya ya Simanjiro vijiji 38 tayari vimepata umeme na vijiji 18
visivyokuwa na umeme vitapatiwa nishati hiyo, hivyo amewataka wananchi
hao waendelee kuwa na subira na kuiamini Serikali yao.
Amesema
Rais Dkt. Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme
tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza
kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na wilaya ya Simanjiro.
Gharama za kuunganishiwa umeme huo zimepungua kutoka sh 177,000 hadi sh.
27,000.
Waziri
Mkuu ameongeza kwa kusema wananchi hawatowajibika tena katika kulipia
gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwa sababu
tayari gharama hizo zote zimeshabebwa na Serikali.
Mheshimiwa
Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaomba wakazi wa wilaya ya Simanjiro
mkoani Manyara na Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao
wamchague Rais Dkt John Pombe Magufuli ili aendeleze kazi ya kuwaletea
maendeleo katika maeneo yao ambayo tayari ameshaianza.
No comments:
Post a Comment