HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, September 16, 2020

TANZANIA KUFIKISHA HEKTA MILIONI MOJA ZA UMWAGILIAJI IFIKAPO 2025 -KM KUSAYA

 


Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akizungumza na wahandisi wa umwagiliaji toka mikoa ya Tanzania bara leo mjini Morogoro. Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (kulia) akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Zana na Umwagiliaji Eng.Anna Mwangamilo (kushoto) wakati alipomaliza kufungua kikao kazi cha Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na wahandisi wa umwagiliaji toka mikoa ya Tanzania bara leo mjini Morogoro.

Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa katika picha ya pamoja na wahandisi wa umwagiliaji toka mikoa yote ya Tanzania bara leo alipofungua mkutano wa siku mbili kujadili namna watakavyoweza kuongeza eneo linalomwagiliwa toka hekta 694,715 za sasa hadi hekta 1,000,000 ifikapo mwaka 2025.

*********************************

Wahandishi wa umwagiliaji wa mikoa wameagizwa kujipanga kwa kasi kusimamia na kutekeleza agizo la Serikali ya Awamu ya Tano la kuhakikisha eneo la kilimo cha umwagiliaji linaongezeka toka hekta 694,715 hadi kufikia hekta milioni moja ifikapo mwaka 2025.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ametoa agizo hilo leo (16.09.2020) alipofungua kikao kazi cha Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Wahandisi wa umwagiliaji toka mikoa ya Tanzania Bara kilichofanyika mkoani Morogoro.

Kusaya amesema ni wakati muafaka kwa wahandisi wote wa umwagiliaji nchini kujikita katika kuweka mipango inayotekelezeka ili eneo la umwagiliaji linalolimwa sasa liongezeke na tija ipatikani kwa wakulima.

“Malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano katika Sekta ya Umwagiliaji ni kuhakikisha kuwa hekta 1,000,000 zinafikiwa katika kilimo cha umwagiliaji ifikapo mwaka 2025 hivyo leo hii mtaniambia je kasi tunayokwenda nayo inatosha?” alisema Kusaya.

Katika hotuba yake ya ufunguzi Katibu Mkuu alibainisha kuwa Wizara ya kilimo inataka Tume ya Umwagiliaji kujikita zaidi katika kutatua changamoto za miundombinu ili wakulima wazalishe mazao kwa wingi kuwezesha nchi kuwa na uhakika wa chakula.

Aliipongeza tume ya umwagiliaji kwa mafanikio ya kuongeza eneo ambapo katika kipindi cha mwaka 2015 hadi Septemba, 2020 Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imefanikiwa kujenga na kukarabati jumla ya skimu 179 za Umwagiliaji na hivyo kufanikiwa kuongeza eneo linalomwagiliwa kutoka hekta 461,000 mwaka 2015 hadi hekta 694,715 mwaka 2020.

Katibu Mkuu huyo aliongeza kusema tija ya uzalishaji imeongezeka katika skimu za umwagiliaji kutoka wastani wa tani 1.8 – 2.0 kwa hekta hadi kufikia wastani wa tani 4.0 – 5.0 kwa hekta kwa zao la mpunga na zao la mahindi uzalishaji umeongezeka kutoka tani 1.5 hadi tani 3.7- 5.0 kwa hekta.

“Lengo tunataka kilimo cha umwagiliaji kiwe endelevu na kumsaidia mkulima kuwa na kipato kikubwa kutokana na uwepo wa ardhi nzuri na mabonde yanayofaa kwa umwagiliaji na nchi kuwa na uhakika wa chakula ” alisisitiza Kusaya.

Kusaya aliwagiza pia wahandisi wa umwagiliaji wa mikoa na watumishi wote kuwa na utumishi wenye tija zaidi na matokeo makubwa, kufanya kazi kwa kuzingatia uzalendo, weledi, kujituma kwa bidii, kuwa wabunifu, kushirikiana kama timu moja katika kutekeleza majukumu ya Tume huku wakizingatia maadili ya utumishi wa Umma ambayo ndiyo Dira katika kuufikia Utumishi uliotukuka na kuitendea haki Kauli Mbiu ya Mhe Rais ya “HAPA KAZI TU”.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Eng.David Kaali alisema wamefanikiwa kuongeza uzalishai wa mpunga kupitia skimu za umwagiliaji kutoka tani 714,000 mwaka 2000 hadi kufikia tani 2,009,174 mwaka 2019 kutokana na miundombinu mingi kuboreshwa.

Aidha, aliongeza kusema tume imefanikiwa pia kujenga na kukarabati skimu 179 za umwagiliaji nchini na kuongeza uwezo wa mitambo kufikia 56 inayofanya kazi kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika mikoa yote.

Ili kufikia lengo la hekta milioni moja ifikapo mwaka 2025 Tume itaendeleza mabonde ya umwagiliaji yafuatayo bonde la mto Ruvuma hekta ( 26,000),mto Ruhuhu (3,700),mto Songwe (3,005), mto Rufiji (64,896), bonde la Luiche Kigoma (3,000) na bonde la Usangu- Mbeya ( 10,000) katika kipindi cha miaka mitano ijayo 2021-2025.

Mhandisi Kaali alisema ili mkakati huo wa kuongeza eneo la umwagiliaji ufanikiwe Tume itahitaji kiasi cha Shilingi Bilioni 986.8 ambapo serikali itachangia asilimia 41 na kiasi kingine kitatokana na vyama vya umwagiliaji,wadau na sekta binasfi kama ilivyoanishwa katika Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II)
Katika hatua nyingine Mhandisi Kaali ameiomba serikali kutoa kipaumbele kwa Tume kuweza kupata wataalam ili kupunguza tatizo ambapo mahitaji ni 646 waliopo ni 208 na kuwa na upungufu wa wataalam 438 kote nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad