RAIS MAGUFULI AZINDUA JENGO LA MAHAKAMA KUU KANDA YA KIGOMA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, September 19, 2020

RAIS MAGUFULI AZINDUA JENGO LA MAHAKAMA KUU KANDA YA KIGOMA

 

 Na Said Mwishehe, Michuzi TV -Kigoma 


RAIS Dk.John Magufuli amezindua rasmi jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma na kwamba kuzinduliwa kwa jengo hilo kutasaidia kuondoa changamoto ya kucheleweshwa kesi kwa wananchi wa Mkoa huo. 

Dk.Magufuli amesema hayo leo Septemba 19, 2020 wakati wa uzinduzi wa jengo hilo ambao umeshuhudiwa na Rais wa Burundi Evarist Ndayishimiye , ambapo amesema kabla ya kuzinduliwa kwa jengo hilo wananchi wa Kigoma walikuwa wakifuata huduma ya Mahakama Kuu mkoani Tabora, hivyo kulisababisha hata haki zao kuchelewa kutolewa. 

Hata hivyo amesema kuwa kuzinduliwa kwa mahakama hiyo ni sehemu ya mkakati wa kujengwa kwa Mahakama , nyingine katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kusogeza huduma za kimahakama karibu na wananchi.Pia amesema katika kipindi cha miaka mitano Serikali imeendelea kuuimarisha muhimili wa Mahakama kwa kuongeza idadi ya majaji hadi kufikia 50, mahakimu 938. 

Wakati huo huo Rais Magufuli ametoa rai kwa Mahakama kuhakikisha wanatunza miundombinu ya jengo hilo ambalo limejengwa kisasa na kwamba mahakama hiyo itumike katika kutoa haki badala ya kuipindisha haki kwasababu za rushwa."Miundombinu iliyojengwa itumike kuimarisha utoaji haki, haitakuwa sahihi iwapo watu watanyimwa haki zao kwasababu ya rushwa.Wananchi wa Kigoma waitumie hiyo Mahakama katka kutafuta haki zao." 

Kwa upande wake Rais wa Burundi Evarist Ndayishimiye amesema amekubali kufungua jengo hilo kwani ni heshima kubwa kwake. 

Awali Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Hamis Jumaa amesema kuwa kukamilika kwa Mahakama hiyo kunakwenda kurahisisha upatikanaji wa huduma za kimahakama kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma ambapo awali walikuwa wanafuata huduma hiyo Mkoa wa Tabora. 

Amesema uzinduzi wa Mahakama hiyo unakwenda sambamba na ule wa ujenzi wa jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Musoma ambalo nalo lililishakamilika na kuzinduliwa. 

"Jengo hili linabeba mambo matatu muhimu, tulikotoka, tuliko na tunakokwenda katika safari ya utoaji wa huduma za haki nchini na hasa Kigoma kwani haikuwa kazi rahisi na hata historia ya mambo ya Mahakama inaeleza vizuri,"amesema. 

Hata hivyo amesema jengo hilo pia litatumika kwa ajili ya Mahakama ya Rufaa na kwamba wanatamani siku moja nchi yote kuwa na majengo ya aina hiyo kwa mikoa ambayo imesalia. 

Hata hivyo amesema juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuboresha sekta ya usafiri wa barabara, reli, usafiri wa anga, umeme na mambo mengine yamekuwa chachu katika kuchochea haki kupatikana kwa wakati sahihi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Burundi Mheshimiwa Evariste Ndayishimiye wakifungua kwa pamoja jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma leo tarehe 19 Septemba 2020. PICHA NA IKULU

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad