HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, September 23, 2020

Mkongo wa Mawasiliano Zanzibar waunganishwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

 

 

Dkt Zainabu Chaula Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano(Sekta ya Mawasiliano) na  Dkt Mustafa Aboud Jumbe, Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wakishuhudia hafla ya utiaji saini wa Mkataba wa Uendeshaji wa Mkongo kati ya TTCL Corporation na ZICTIA baada ya kufanikisha kuunganisha Mkongo wa Zanzibar kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasilianoa, katika Ukumbi wa Ofisi za Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, visiwani Zanzibar. 

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation Waziri Kindamba (Kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Uendeshaji Mkongo Zanzibar- ZICTIA Mhandisi,Shukuru Awadh Suleiman(Kulia) wakisaini mkataba wa uendeshaji baada ya kufanikisha kuunganisha Mkongo wa Zanzibar kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasilianoa, katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Ofisi za Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, visiwani Zanzibar.

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation Waziri Kindamba (Kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Uendeshaji Mkongo Zanzibar- ZICTIA Mhandisi,Shukuru Awadh Suleiman wakibadilishana nyaraka baada ya kuingia makubaliano ya  uendeshaji wa Mkongo katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Ofisi za Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, visiwani Zanzibar. 

    Dkt Mustafa Aboud Jumbe, Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji (Kulia) akimpa mkono wa pongezi Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation Waziri Kindamba(Kushoto) kwa kufanikisha kuunganisha Mkongo wa Zanzibar kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawailiano.

 ========  ======= ========

Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL Corporation limetiliana saini ya mkataba wa uendeshaji baada ya kufanikisha kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Mkongo wa Mawasiliano wa Zanzibar katika hafla iliyofanyika katika Ofisi za Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, visiwani Zanzibar

 

Tukio hilo utiaji saini lilishuhudiwa na Dkt Zainabu Chaula Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano(Sekta ya Mawasiliano) na  Dkt Mustafa Aboud Jumbe, Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji.

 

Makubalino hayo yameingiwa rasmi kati ya Shirika la Mawasiliano Tanzania kupitia Mkurugenzi Mkuu Waziri Kindamba na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Uendeshaji Mkongo Zanzibar- ZICTIA Mhandisi,Shukuru Awadh Suleiman.

 

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation         Waziri Kindamba amesema tumekamilisha zote muhimu za kitaalamu na kiufundi kwa pande zote mbili ya Tanzania Bara na Zanzibar hii inatokana na kufanikisha majaribio yaliyofanywa miezi kadhaa iliyopita ya kuunganisha Mkongo wa Taifa Mawasiliano (NICTBB)  na Mkongo wa Zanzibar kupitia vituo vya Tanga - Pemba na Dar es salaam - Unguja.

 

“Kufanikisha kuunganisha Mkongo Taifa na huu wa Zanzibar,ni fursa pekee kwa watoa huduma mbalimbali za kijamii, uwekezaji, kibiashara na kiuchumi kwa pande zote mbili kufikia masoko au wateja wao kwa urahisi, haraka zaidi na kwa gharama nafuu” ameongeza Mkurugenzi Mkuu TTCL

 

Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu Waziri Kindamba aliongeza kuwa kuunganishwa kwa Mkongo wa Taifa, na huu wa Zanzibar ni fursa kwa watoa huduma mbalimbali kisiwani Zanzibar kuweza kuyafikia masoko ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kwa urahisi na haraka zaidi.  Vilevile kwa watoa huduma mbalimbali wa Tanzania Bara na nchi za Jirani kuweza kuyafikia masoko ya Zanzibar kwa urahisi, haraka na gharama nafuu zaidi.

 

Naye, Mtendaji Mkuu wa ZICTIA, Mhandisi, Shukuru Awadh Suleiman amesema kuwa kusaini kwa Mkataba huu imetokana na ushirikiano mkubwa ya kiutendaji kati ya Taasisi hizi mbili, kuunganishwa kwa Mkongo wa Taifa na huu wa Zanzibar utaleta mageuzi makubwa katika matumizi ya mawasiliano sambamba na kukuza uchumi wa Taifa letu.  

 

Katibu Mkuu  Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,(Sekta ya Mawasiliano) Dkt Zainabu Chaula amezitaka taasisi hizi mbili TTCL na ZICTIA kuhakikisha vyema wanasimamia na kulinda miundombinu hiyo Mkongo ya mawasiliano ili huduma za mawasiliano zipatikane muda wote.

 

“Ni wazi kuwa uwepo wa Mkongo wa Zanzibar ambao umeunganishwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unaenda kufungua fursa kwa wawekezaji na watoa huduma mbalimbali ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kwa sababu kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano tumefanikisha kuunganisha nchi za Afrika Mashariki na kati ikiwemo Rwanda, Burundi, Kenya, Congo, Zambia, Malawi na Uganda” ameongeza Katibu Mkuu Mawasiliano Dkt Zanaibu Chaula

 

Aidha, Katibu Mkuu Mawasiliano Dkt Chaula ameongeza kuwa ufunguzi wa njia ya Mawasiliano ya Mkongo kati ya Tanzania Bara na Zanzibar utakuwa na manufaa makubwa kwa Taifa letu ambapo itaongeza kasi ya matumizi ya huduma za data na intaneti sambamba na huduma nyingine za kijamii na kiuchumi.

 

Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Dkt Mustafa Aboud Jumbe amesema kuwa Mkongo wa Zanzibar umefanikisha kuunganisha Mikoa na wilaya zote za Ugunja na Pemba. Awali kulikuwa na changamoto ya mawasiliano kati ya Unguja na Pemba kutokana na kutumia teknolojia ya Mawimbi ya Radio (Radio Link), kupitia Mkongo wa Zanzibar na  Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano visiwa vya Unguja na Pemba vitakuwa vimeunganishwa kwenye miundombinu ya mawasiliano.

 

Katibu Mkuu Jumbe ameongeza kuwa  kuunganisha Mkongo wa Taifa na Mkongo wa Zanzibar utaimarisha mawasiliano ya ndani kati ya Unguja na Pemba sambamba na kufanikisha kuunganisha Visiwa hivyo na mikoa ya Tanzania Bara pamoja na nchi za jirani.

 

 Aidha, Dkt Jumbe amezitaka taasisi hizi mbili TTCL na ZICTA kuhakikisha inalinda na kuhifadhi miundombinu hii ya mawasiliano ili iweze kuleta teja kwa wananchi sambamba na kuhakikisha gharama za mawasiliano ili wananchi waweze kunufaika na huduma za mawasiliano nchini.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad