Mgombea Ubunge wa jimbo la Songea mjini kwa tiketi ya Chadema Aden Mayalla wa pili kushoto akiwa na baadhi ya viongozi wa Chama hicho mkoa wa Ruvuma na Kanda ya Mbeya wakiwa katika maandamano ya hiari mara baada ya kumaliza mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya soko kuu mjini Songea jana. Picha na Muhidin Amri
Na Muhidin Amri, Songea
MGOMBEA Ubunge wa jimbo la Songea mjini kwa tiketi ya Chadema Aden
Mayalla amesema,kukosekana kwa soko la uhakika la kuuzia mazao
yanayozalishwa kwa wingi katika jimbo hilo kumetokana na kutowajibika
kwa baadhi ya viongozi waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi.
Hivyo, amewaomba wanachi wa jimbo hilo wamchague awe mbunge ili aweze
kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa soka la
kuuzia mazao ya wakulima ambayo sasa yanauzwa kwa bei ndogo licha ya
gharama kubwa za uzalishaji.
Mayalla amesema hayo jana katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika
viwanja vya soko kuu mjini Songea, na amewataka wananchi wa Songea
kuhakikisha wanakipigia kura nyingi Chadema ili kukiondoa Chama cha
Mapinduzi madarakani mabcho kwa muda mrefu kimeshindwa kuisimamia
Serikali.
Mayalla amesema, endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo ataanza
na utatuzi wa kero zinazowakabili wananchi wa Songea kwa muda mrefu hasa
suala la soko la mazao,maji mindombinu ya barabara na kuondoa fedha ya
malipo ya kadi ya mgonjwa kabla ya kuonana na Daktari.
Alisema, mkoa wa Ruvuma umebarikiwa kuwa na ardhi nzuri inayofaa kwa
kilimo cha mazao mbalimbali kama korosho,kahawa,mahindi na ufuta, hata
hivyo bado wananchi wake ni maskini ikilinganisha na mikoa mingine hapa
nchini.
Aidha mgombea huyo amesema, iwapo atachaguliwa kuwa mbunge atahakikisha
anarudisha vyuo vyote vilivyofutwa na Serikali ya CCM ili kutoa fursa
kwa watoto wa jimbo la Songea na mkoa wa Ruvuma kupata nafasi ya
kujiunga na elimu ya juu ili nao waweze kufanya kazi za kuchangia
maendeleo katika mkoa huo.
“nawaomba sana wananchi wenzangu wa Songea mjini tarehe 28 Oktoba
mnichague mimi Mayalla niwe mbunge wenu na Mheshimiwa Tundu Lissu katika
nafasi ya Urais,Songea tumebaki nyuma kwa muda mrefu licha ya
rasilimali nyingi tulizonazo ikiwemo madin”alisema.
Mbali na changamoto ya soko la mazao Mayalla amesema, iwapo Chadema
itachaguliwa na kushika dola itahakikisha inajenga upya barabara ya
Njombe-Makambako kwa kiwango cha lami kwani muda wake umekwisha jambo
linalochangia ajali za mara kwa mara.
Kwa upande wake, kada wa Chadema kutoka mkoa wa Mbeya John Mwambigili
amesema, wananchi wa jimbo la Songea wanakabiliwa na changamoto nyingi
hali ilirudisha sana maendeleo na kutolea mfano kujengwa kwa kituo kipya
cha mabasi eneo la Shule ya Tanga umbali wa km 30 kutoka mjini.
Kwa mujibu wa Mwambigili,Manispaa ya Songea haijawatendea haki wananchi
kupeleka kituo hicho Shule ya Tanga kwani sio wote wenye uwezo wa
kulipia usafiri kutoka mjini hadi katika kituo hicho pale wanapohitaji
kusafiri.
Kwa hiyo, amewaomba wananchi kutorudia makosa kwa kumchagua mbunge
aliyemaiza muda wake Dkt Damas Ndumbaro badala yake kuhakikisha
wanamchagua Mgombea ubunge wa Chadema Aden Mayalla ambaye ni msikivu na
amekuwa akishiriki shughuli mbalimbali za kijamii na wananchi.
Alisema, haiwezekani na haingii akilini kuona mji wa Songea licha
ukongwe wake umebaki kama kambi ya wakimbizi kwa kukosa maendeleo
licha ya kuwa kituo kikuu cha kuuzia mazao na bidhaa mbalimbali na watu
kutoka wilaya nyingine za mkoa wa Ruvuma kama Mbinga,Namtumbo na
Tunduru.
Naye mwanachama mkongwe wa Chadema Joseph Fume, amewaomba wakazi wa
Songea kutorudia makosa ya kumrudisha tena Dkt Ndumbaro kwani katika
kipindi chake cha miaka mitano hakuna maendeleo yaliyopatikana katika
jimbo hilo.
Alisema,njia pekee ya kumuondoa madarakani ni kumnyima kura tarehe 28
Oktoba kwa kuwa ameshindwa kuliongoza jimbo hilo licha ya tabia yake
kung’ang’ania nafasi hiyo.
No comments:
Post a Comment