HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 6, 2020

WAZIRI NDITIYE: SAFARI ZA TRENI ARUSHA – MOSHI KUANZA HIVI KARIBUNI

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amefanya ziara kukagua kazi ya ufufuaji wa reli kati ya Moshi hadi jijini Arusha kwa kutumia treni ya uhandisi ya Shirika la Reli Tanzania – TRC hivi karibuni Agosti 2020.

Lengo la ziara hiyo ni kuona maendeleo ya mradi wa ufuaji wa reli hiyo ambayo hivi karibuni itaanza kutoa huduma ya kusafirisha mizigo na abiria baada ya ufufuaji wake kukamilika kwa kiasi kikubwa. Katika ziara yake Naibu Waziri aliambatana na Maafisa kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini – LATRA, waandishi wa habari na maafisa kutoka TRC.

Sambamba na ukaguzi huo uliofanywa na Naibu Waziri, Shirika la Reli Tanzania hivi karibuni lilifanya ukaguzi wa kufanya tathmini ya ubora wa njia hiyo ya reli pamoja na kuendesha kampeni ya siku saba iliyoanza Agosti 3, 2020 ili kuongeza uelewa kwa wananchi wa Arusha, Moshi na Tanga kuhusu matumizi sahihi ya alama za usalama wa reli ili kuhakikisha reli na wananchi wanakuwa salama pindi treni zitakapoanza kutoa huduma.

Aidha katika ziara yake Naibu Waziri amewataka wananchi wote wanaofanya shughuli za kijamii na kiuchumi ikiwemo Kilimo na Biashara kandokando ya reli kuacha mara moja kwani kufanya hivyo kunahatarisha usalama wao na miundombinu ya reli, pia amelitaka Shirika la Reli Tanzania kushirikiana kikamilifu na viongozi wa Mikoa, Wilaya na Serikali za Mitaa katika kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu usalama wa reli na kuwa walinzi wa kwanza wa reli.

“Nimekagua njia iko vizuri, tunatarajia kuanza safari za treni kati ya Arusha na Moshi baada ya wiki mbili au tatu kutoka sasa, hivyo Shirika la Reli na viongozi wa mikoa hii wahakikishe wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu usalama wa reli” alisema Mhandisi Atashasta

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa uendeshaji wa huduma za reli TRC Ndugu Focus Makoye Sahani amesema kuwa Shirika la Reli litaendelea kushirikiana na viongozi wa maeneo husika wakati wa Kampeni hiyo ya uelewa katika kuhakikisha wananchi wanapata uelewa kuhusu usalama wa reli ili kudhibiti ajali za treni pindi huduma za treni zitakapoanza hivi karibuni kati ya Moshi na Arusha.

 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akizungiumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kufanya ziara kukagua kazi ya ufufuaji wa reli kati ya Moshi hadi jijini Arusha kwa kutumia treni ya uhandisi ya Shirika la Reli Tanzania – TRC hivi karibuni Agosti 2020.

Maandalizi ya  ufufuaji wa reli kati ya Moshi hadi jijini Arusha kwa kutumia treni ya uhandisi ya Shirika la Reli Tanzania – TRC hivi karibuni Agosti 2020.
 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad