WAZIRI AAGIZA MKANDARASI WA REA AKATWE MSHAHARA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 13, 2020

WAZIRI AAGIZA MKANDARASI WA REA AKATWE MSHAHARA

 

Veronica Simba – Dodoma
WAZIRI wa Nishati Dkt Medard Kalemani, ameagiza Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza, mkoani Dodoma akatwe asilimia 10 ya malipo yake kutokana na kuchelewa kukamilisha kazi hiyo.

Alitoa maagizo hayo, Agosti 12, 2020 baada ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi huo katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Chemba.

Akiwa amefuatana na Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga, Waziri Kalemani aliutaka Uongozi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kukata kiasi hicho cha malipo ya Mkandarasi husika, ambaye ni Kampuni ya A2Z Infra Engineering Limited, kuanzia Juni 30, 2020 muda ambao alipaswa kukamilisha Mradi.

Sambamba na agizo hilo, Waziri pia alimtaka Mkandarasi huyo kukamilisha kazi ya kuunganisha umeme katika vijiji vyote 66 vilivyobakia kabla ya Septemba 15 mwaka huu, huku akisisitiza kuwa, hakutakuwa na nyongeza ya muda wala msamaha.

“Asipomaliza ndani ya wakati huo, mchukulieni hatua za kisheria na kimkataba. Maeneo yatakayobaki, fanyeni ninyi TANESCO kwa pesa hiyo.”

Katika kuhakikisha kazi hiyo inatekelezwa, Waziri alimwelekeza Mkuu wa Wilaya kushikilia hati za kusafiria za Wakandarasi husika na kuhakikisha hawatoki nje ya Mkoa wa Dodoma, hadi watakapokamilisha kazi hiyo.

Aidha, alimwagiza Mkandarasi huyo kuongeza vibarua na magenge, ili aweze kukamilisha kazi kwa wakati.

Vilevile, alimtaka kuondoa mara moja nguzo zote zilizorundikwa chini na kuzisimika, kuvvuta nyaya na kuwaunganishia umeme wananchi.

“Kiu ya wananchi ni kuona umeme unawaka katika nyumba zao. Hawependezewi kuona nguzo zikiwa zimerundikana chini, nanyi mkipitapita pasipo kuwawashia umeme,” alisisitiza Waziri.

Dkt Kalemani alitoa wito kwa Wakandarasi wote nchini, wanaoendelea kutekeleza Miradi ya REA III, kuhakikisha wanakamilisha ifikapo Septemba 15, 2020.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya alimshukuru Waziri kwa kufuatilia utekelezaji wa Mradi husika huku akiweka wazi kuwa hana imani na Mkandarasi huyo kutokana na kutotekeleza majukumu yake ipasavyo.

Aliahidi kufanyia kazi maelekezo yote ya Waziri katika kumsimamia Mkandarasi ili kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo na hivyo wananchi wapate huduma ya umeme kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Katika Taarifa yake kwa Waziri, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Frank Chambua alieleza kuwa, kati ya vijiji 581 vya Mkoa huo, vijiji 393 vimeshapata umeme ambavyo ni sawa na asilimia 67.47 ya vijiji vyote.

 Mkuu wa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, Simon Odunga (wa pili-kushoto) akizungumza jambo, wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa pili-kulia) wilayani humo, kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Agosti 12, 2020.
 Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kulia), akitoa maelekezo kwa Wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza, mkoani Dodoma, Kampuni ya A2Z Infra Engineering Limited (kushoto) kuhakikisha wanakamilisha kazi hiyo kabla ya Septemba 15, mwaka huu, alipokuwa katika ziara ya kazi wilayani Chemba, Agosti 12, 2020. Kulia kwa Waziri ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Simon Odunga.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, wakiwa katika ziara kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, wilayani Chemba, Mkoa wa Dodoma, Agosti 12, 2020.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad