HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, August 22, 2020

WATIANIA 176 KIBAMBA... WASEMA WAMEJIPANGA


Makada wa CCM ambao walitiania ya kuomba ridhaa ya kuomba kueliwa na Chama chao kugombea ubunge jimbo la Kibamba wakionesha ishara ya kidole gumba kama ishara ya umoja na mshikano baada ya mwenzao Issa Mtemvu jina lake kupitishwa kupeperusha bendera kwa nafasi ya ubunge.

Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MAKADA wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wapatao 176 waliotiania kuomba ridhaa ya kugombea ubunge katika Jimbo la Kibamba jijini Dar es Salaam wameanzisha umoja wao ili kumuunga mkono Issa Jumanne Mtemvu aliyepitishwa na Chama chao kugombea ubunge katika jimbo hilo.

Wamesema Umoja huo utakuwa chachu ya kufanikisha mgombea wao kushinda kwa kishindo na jimbo la Kibamba kurudi kwenye mikono ya CCM baada ya kuwa upinzani kwa muda mrefu huku mmoja ya watia nia George Mosha akitoa Sh.200,000 ili kumpa Mtemvu akachukulie fomu ya ubunge Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC).

Mwenyekiti wa Umoja huo wa Watia 176 Jimbo la Kibamba Dk.Mkumbo Mitula amesema wao ndio walikuwa wengi kuliko maeneo mengine na sasa wote kwa umoja wao wanaunga mkono uamuzi wa Chama chao kupitia jina la Mtemvu kugombea ubunge Kibamba.

"Mnafahamu jinsi ambavyo Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Magufuli ambavyo amefanya mambo makubwa katika nchi yetu, watu wengi tumejitokeza kwasababu ya hamasa iliyotokana na utendaji wake, ndio maana watia nia mwaka huu wamekuwa wengi kuliko wakati wowote ule,"amesema Dk.Mitula.

Hivyo amesema katika kufanikisha ushindi kwa mgombea wao tayari wameunda kamati tano ambazo zitakisaidia Chama chao wakati wa kampeni.Kamati hizo ni Mipango,usafiri na lojistiki,habari, kampeni na kamati ya propaganda.

"Tunafahamu Chama ndicho kinachokamata mambo yote ya kampeni , hivyo tutasubiri ratiba ya Chama na kisha nasi kuangalia namna ambavyo tutaendelea na majukumu yetu ambayo tumejiwekea Umoja wa watia nia 176 Kibamba.

"Na katika hili hatuko peke yetu kwani hata wale ambao walitia nia Ubungo wapato 111 nao tumeungana nao na kitu kimoja lengo letu ni kuhakikisha Kibamba na Ubungo zote zinakuwa kwenye mikono ya CCM.Sisi watia nia baada ya jina la mmoja wetu kupitishwa tulisema hawa watia nia wote ni hazina na kuamua tuwe timu moja ya kufanikisha ushindi.

"Leo tunavunja rasmi makundi yetu , sisi wenyewe kwa hiyari yetu, hatujalazimishwa na mtu , tumeamua kuvunja makundi wenyewe kwa maslahi ya Chama.Kitu kingine ambacho napenda kukisema ni kwamba katika watia nia 176 tulijua mmoja atapita na azimio letu ni kumuunga mkono kwa hali na kwa mali,"amesema.

Ameongeza hivyo wameamua leo kukusanyika kwa ajili ya kuwathibitishia watanzania wote kwamba wana mapenzi mema na Chama na wameamua kuvunja makundi kwa ajili ya kumuunga mkono mwenzao Issa Jumanne Mtemvu katika Jimbo la Kibamba.

Dk.Mitula amesema wao wako na Chama chao, wako kwa ajili ya kufanya kazi, wameshikana na hakuna mmeguko na kwamba wanamtia moyo Mwenyekiti wao na viongozi wengine wa kitaifa kuwa mchakato uliofanyika uko sahihi na wao wameridhika.

"Tuliotia nia Kibamba tuko watu wenye taaluma mbalimbali ambazo sasa tunakwenda kuziunganisha na kufanya kazi moja tu ya kuhakikisha tunashinda na kuirudisha Kibamba kwenye mikono ya CCM.Maneno haya yaende na tunawatangazia Watanzania umoja huu ni mfano.

"Tunaomba na wengine ambao waligombea kwa maana ya kutia nia lakini mmoja akateuliwa kupeperusha bendera Chama wafanye kama tulivyofanya sisi, tumeungana na mioyo yetu ni safi kabisa,"amesema Dk.Mitula.

Kwa upande wake George Mosha ambaye ni miongoni mwa watia nia katika Jimbo la Kibamba ambaye ameamua kutoa fedha Sh.200,000 na kumkabidhi aliyepitishwa na Chama hicho kupeperusha bendera , amesema sababu za kutoa fedha hizo ni kutokana na kufuhishwa na jinsi mchakato ulivyokwenda hadi kupatikana kwa jina la Mtemvu

Wakati huo huo Anuar Sanga ambaye ni miongoni mwa walitia nia jimbo la Kibamba amesisitiza kwa sasa wao wamekuwa kitu kimoja na lengo lao ni kuhakikisha mgombea wao anashinda kwa zaidi ya asilimia 100."Pamoja na ule wingi wetu wakati tulipotia nia hivi sasa sisi ni kitu kimoja."


Umoja wa watia nia 176 katika Jimbo la Kibamba jijini Dar es Salaam wakiongozwa na Mwenyekiti wa Umoja huo Dk.Mkumbo Mitula (katikati) wakiwa wamenyoosha mikono juu kama ishara ya kuuthibitisha umoja wenye lengo la kumuunga mkono Issa Mtemvu ambaye jina lake limepitishwa kugombea ubunge.



Mwenyekiti wa Umoja wa watia nia 176 katika Jimbo la Kibamba Dk.Mkumbo Mitula (katikati) akifafanua jambo kuhusu sababu za kuwa na Umoja huo ambao lengo lake kuu ni kufanikisha ushindi kwa mwenzao ambaye jina lake limepitishwa na CCM kugombea ubunge.
Mwenyekiti wa Kamati ya Habari katika Umoja wa Watiania 176 jimbo la Kibamba Anuar Sanga akifafanua jambo kuhusu Umoja huo jinsi walivyojipanga kufanikisha ushindi wa mgombea wao wa ubunge.
Katibu wa Umoja wa Watiania 176 katika Jimbo la Kibamba Wakili Precious Ahmad Hassan (wa pili kulia) akizungumza kilichowasukuma kuanzisha Umoja huo ambao sasa umekuwa kitu kimoja kufanikisha ushindi wa CCM jimbo la Kibamba ambapo pamoja na mambo mengine amesema wamejipanga kwa hali na mali.
Mmoja ya watiania hao George Mosha aliyesimama nyuma wa tatu kushoto) akieleza sababu zilizomsukuma kuamua kutoa Sh.200,000 kwa ajili ya kumuwezesha mgombea ubunge wa jimbo hilo Issa Mtemvu kwenda kuchukua fomu ya ubunge NEC.


Watiania hao wakiangalia hash tag inayosema Kibamba ya Kijani ambayo wataitumia katika kipindi cha kampeni cha kusaka ushindi wa jimbo hilo pindi kampeni zitakapoanza rasmi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad