WANAWAKE MUNDARARA WAFAIDIKA NA MADINI YA RUBY - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 13, 2020

WANAWAKE MUNDARARA WAFAIDIKA NA MADINI YA RUBY

 

WANAWAKE wa jamii ya wafugaji wa Kata ya Mundarara Wilayani Longido wamenufaika kiuchumi baada ya kujihusisha na shughuli za uchenjuaji mchanga wa madini ya Ruby. 

Wakizungumza wakati wakipatiwa elimu ya afya na usalama kwa wachekechaji iliyotolewa na shirika la Haki Madini, wanawake hao walidai kuwa maisha yao yamebadilika kiuchumi kupitia madini hayo ya Ruby wanayaopata baada ya kuchekecha mchanga. 

Mmoja kati ya wachekechaji hao Martha Ngada alisema kupitia uchekechaji huo amefanikisha kuwasomesha watoto wake saba akishirikiana na mumewe. 

Ngada alisema hivi sasa wameondokana na utegemezi kwa kubadili maisha yao kiuchumi kupitia mchanga wa madini ya Ruby wanayochenjua mgodini.

"Pia nimefanikiwa kuwanunua mbuzi watano ambao ninaendelea kuwafuga na kujipatia maziwa ambayo nakunywa na kuyauza." alisema.

Mchekechaji mwingine Leah Lazaro alisema shida ndogo ndogo ameondokana nazo hivi sasa kupitia kazi yao ya kuchenjua mchanga wa madini ya Ruby.

Lazaro alisema wanawake wengine wanapaswa kubadilika kwa kufanya kazi halali ya kujipatia kipato kuliko kujihusisha na vitendo visivyo na maadili au kuomba mitaani. 

Ofisa miradi wa shirika la Haki Madini, Emmanuel Mbise alisema katika elimu waliyotoa pia wametoa barakoa kwa wanawake hao ili waweze kujikinga na vumbi. 

Mbise alisema wamewapa elimu wanawake hao wasifanye kazi ya kuchekecha mchanga wakiwa na watoto wao kwani watawasababishia maradhi ya vifua. 

Ofisa ustawi wa jamii wa halmashauri ya wilaya ya Longido, Atuganile Chisunga alisema wanawake wengi wa eneo la Mundarara wamejiunga na shughuli za uchenjuaji mchanga baada ya kubaini kuna kipato. 

Ofisa jinsia na uchimbaji wa shirika la Haki Madini, Joyce Ndakaru alisema hivi sasa jamii ya wafugaji wanawake wanaimudu kazi hiyo kutokana na kutotumia nguvu kubwa. 

"Kupitia mradi wa afya na usalama unaotekelezwa kwenye vijiji vinne vya eneo hili tunatambua juhudi kubwa zinazofanywa na wanawake katika kujishughulisha," alisema. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad