HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 6, 2020

NANENANE DODOMA KUANZISHA MAONESHO YA KIMATAIFA YA UTALII WA MIFUGO

Mwakilishi wa Wakuu wa Mikoa ya Singida na Dodoma  kwenye  Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati, ambaye  pia ni  Mkuu ya Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi  Athuman Mukunda akijaribu  kuendesha Trekta kwenye maonesho hayo  leo, aliye pembeni yake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel,  walio chini  mwenye miwani ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Anjelina Lutambi na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Injinia Jackson Masaka wakishuhudia tukio hilo. Picha na John Mapepele
Mfugaji wa Mifugo Juma Seleman kutoka  Mpwapwa akipitisha Ng’ombe wake  Mashindano maalum ya Paredi ya mifugo iliyofanyika kwenye maonesho ya nanenane kanda ya kati kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma. Picha na John Mapepele
Viongozi kutoka Mkoa wa Dodoma na Singida  pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa  mashindano maalum ya Paredi ya mifugo iliyofanyika kwenye maonesho ya nanenane kanda ya kati kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma. Picha na John Mapepele
Wawakilishi wa Wakuu wa Mikoa ya Singida na Dodoma  kwenye  Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati,ambaye ni  Mkuu ya Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi  Athuman Mukunda(mwenye kilemba) akimuuliza maswali muoneshaji wa kampuni la uzalishaji wa chakula cha mifugo ya Harsho Group, Juma Ally (mwenye Tisheti ya Njano) Kulia ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Anjelina Lutambi. Picha na John Mapepele

Na John mapepele, Dodoma

Wakuu wa Mikoa ya Dodoma na Singida wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii  kuyafanya mashindano maalum ya Paredi ya Mifugo yanayofanyika kila mwaka kwenye  kanda ya kati kwenye viwanja vya Nzuguni  jijini Dodoma kuwa Maonesho ya Kimataifa  ya utalii wa mifugo ili kuongeza pato la taifa na kuleta hamasa kwa wananchi kushiriki.

Katika hotuba iliyotolewa kwenye Paredi la Mifugo leo na Mkuu ya Wilaya ya Bahi Mwanahamisi  Athuman Mukunda kwa niaba ya Wakuu hao wa Mikoa, amesema Tanzania imebarikiwa kuwa nchi ya pili  kwa kuwa na mifugo mingi barani Afrika  hiyo uanzishaji uboreshaji wa Paredi  la mifugo utasaidia  kuinua uchumi wa taifa kwa kuongeza  kipato kutoka kwa watalii  kupitia mifugo.

Ameongeza kuwa jiografia ya Dodoma kuwa katika ya nchi na  hali ya hewa nzuri ya majira ya mwezi Agosti katika eneo la Nzuguni  linafanya watalii wengi kuja kutembelea maonesho hayo.

“Ndugu zangu  niwaambie ukweli  katika nchi yetu miongoni mwa Wizara mama ambazo ni nguzo na tegemeo wa maisha ya wananchi wake na ambayo inaweza kuongeza mapato ya Serikali ni  Wizara ya Mifugo na Uvuvi”  alisisitiza Mhe. Mukunda

Amesema mifugo na uvuvi ni dhahabu inayotembea ambayo kama  itatunzwa  kwa kuzingatia ushauri na utaalam  utaongeza tija na kulifanya taifa lisonge  mbele  kiuchumi.

Hata hivyo amesema changamoto inayosababisha kutokuwa na mageuzi ya haraka kwenye Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi nchini ni kukosekana kwa wataalam kwenye  ngazi za chini kwa wananchi ambapo amesisitiza kuwa  kuna umuhimu Wizara husika kushusha wataalam hadi kwenye ngazi za vijiji  badala yahali ilivyo sasa ambapo wataalam  wapo kwenye ngazi za juu jambo ambalo linafanya utalaamu usiwafikie wananchi kama ilivyokusudiwa.

Aidha ameongeza kuwa kuna haja ya Wizara husika kuboresha ushirikiano katika utekelezaji  na utoaji wa maelekezo ambapo amesema  kumekuwa na ushahidi kuwa sehemu ambazo wizara zimeshirikiana kikamilifu na Halmashauri husika kumekuwa na matokeo chanya.

 Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Anjelina Lutambi amepongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye Sekta mbalimbali hapa nchini ikiwa ni pamoja na Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambapo ameelekeza  Halmashauri za Mkoa wa Singida kutenga maeneo  kwa ajili ya kulima malisho ya  mifugo na ameishukuru Wizara ya Mifugo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Ikungi kuanzisha shamba darasa  bora la malisho ya mifugo ambalo ni la mfano hapa nchini.

“Ukiona Mheshimiwa, Rais Dkt. John Magufuli anawekeza kwenye miradi kama ule wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere Rufiji, Reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Makutupola ya Singida lengo ni kujenga uchumi jumuishi” ameongeza Dkt. Lutambi

Amesema Mkoa wa Singida umendelea kupiga hatua katika kutekeleza   miradi mbalimbali ambapo amesema licha ya kufanya mapinduzi makubwa kwenye zao la Korosho   pia wamesimamia  vizuri sekta nyingine  kama vile  sekta ya madini ambapo muelekeo wa sekta ya madini ni kuwafanya wananchi wamiliki raslimali hii kwa kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi. Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina amesema  Serikali  ya awamu ya Tano imefanya mageuzi makubwa  kwenye sekta ya mifugo ambapo  viwanda vingi vya nyama  vimeanzishwa, kuboresha kwa miundombinu ya mifugo kama majosho na kuimarisha  minada, kuzuia utoroshaji wa  mifugo kwenda nchi jirani na  kuanza  kutengeneza  chanjo za mifugo ambapo hadi sasa chanjo sita zimekamilika na  nyingine saba zinatarajia kukamilika katika kipindi  kifupi kijacho na kufanya  chanjo  dhidi ya magonjwa 13 za kipaombele kukamilika.

Aidha, amesema Wizara  ya Mifugo tayari imeshatangaza  rasmi tarehe 13/5/2020  bei elekezi za chanjo za wanyama dhidi ya magonjwa 13 ya kipaombele  kwa mujibu wa Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 za Mwaka  2020 kifungu cha 3(2)(g) na Kanuni za Chanjo na Uchanjaji Na 180 za Mwaka 2020 Kifungu cha 14(b) na (c)  ambapo bei ya dukani nay a kuchanjia kwa dozi  haitazidi  viwango vilivyoainishwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad