HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, August 21, 2020

HATUNA UHABA WA CHANJO NCHINI- DKT. LEONARD SUBI

 

Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuwa, haina upungufu wa chanjo wa aina yeyote hivyo kuwataka wazazi/walezi kuwapeleka watoto wao kuwapatia chanjo katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi wakati alipotembelea ghala ya kuhifadhia chanjo iliyopo hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kukagua hali ya chanjo katika mkoa huo.

Dkt. Subi amesema kuwa, chanjo zote aina tisa ambazo zinakinga dhidi ya magonjwa kumi na tatu zipo kwenye ghala hilo“tulikua na upungufu wa aina mbili za chanjo nchini kati ya tisa ambazo tumekuwa tukizitoa lakini, sasa hivi chanjo zote zipo, kwani zimeshawasili hapa nchini na usambazaji unaendelea”, amesema Dtk. Subi

Hata hivyo Dkt. Subi amesema kuwa, upungufu huo wa chanjo ulitokea baada ya Dunia kukumbwa na janga la mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 ambapo anga zote zilifungwa kwani chanjo husafirishwa kwa mnyororo baridi, kwahiyo huitaji usafiri wa anga.

“Tunamshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kulifungua anga la Tanzania ambapo,  chanjo sasa zimeanza kuingia nchini na hadi sasa mikoa kumi na tatu(13) chanjo hizi zimeshapokelewa kati ya mikoa 26, na mikoa mingine kumi na tatu  ya Tanzania Bara usambazaji unaendelea kupitia Bohari ya Dawa (MSD)”.

Aidha, Dkt. Subi alisema kuwa, usambazaji wa chanjo hizo mbili ambazo wananchi walikua wanazikosa, umeshaanza na watazipata kwa uhakika, huku akielekeza bohari ya dawa nchini (MSD) kuhakikisha chanjo zote  zimefika katika mikoa iliyosalia ya Tanzania Bara ifikapo mwishoni mwa wiki hii.

“Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri wote nchini hakikisheni chanjo hizo mnazipeleka kwenye vituo vyetu  vya kutolea huduma za afya na muwajulishe wananchi kwamba chanjo zipo na zinapatikana bila malipo yeyote, wazazi na walezi pelekeni watoto wenu kupata chanjo katika mikoa yenu”Alisisitiza Dkt. Subi.

Kwa upande wa taarifa iliyotolewa na moja ya chombo cha habari hapa nchini kwa kukosekana kwa chanjo ya kuzuia kuhara (Rota) Dkt. Subi alifafanua kuwa, nchi ya Tanzania haijawahi kukosa chanjo hiyo,huku akiweka bayana kuwa, chanjo zilizopungua kwa mwezi mmoja na nusu ni chanjo ya Polio na Surua-Rubella hali iliyosababishwa na mlipuko wa Covid-19 Duniani, huku akisisitiza kuwa serikali imekua ikinunua chanjo hizo kutoka nchi za Ulaya na Asia.

Aliendelea kusema kuwa, Serikali inaendelea kutoa fedha za chanjo, na kuweka wazi kuwa hadi sasa  imetoa zaidi ya  shilingi bilioni 18 kwa ajili ya ununuzi wa chanjo  na kuifanya  Tanzania kuendelea kuwa katika kiwango cha juu cha utoaji wa chanjo kwa zaidi ya asilimia 98 kwa miaka sita mfululizo.

Hata hivyo, Dkt. Subi amesema kuwa, Tanzania haijawahi kupata mgonjwa wa kupooza tangu mwaka 1996, jambo linalotokana na  uwepo wa hali nzuri ya upatikanaji wa chanjo, huku akidai kuwa nchi ya Tanzania tayari imepata cheti cha utambuzi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2015.

 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad