HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, July 12, 2020

SERIKALI YALIPA WAFANYAKAZI DARAJA LA KILOMBERO



Serikali imeendesha zoezi la malipo kwa waliokuwa wafanyakazi zaidi ya 250 wa kampuni ya kikandarasi ya China Railway 15 Group ambao walipunjwa mishahara yao wakati wa ujenzi wa daraja la Magufuli (Kilombero), mkoani Morogoro, mara baada ya uhakiki wa taarifa zao kukamilika.

Akizungumza wakati wa uendeshaji wa zoezi hilo, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro, Mwenyekiti wa timu ya uhakiki wa madai ya malipo hayo kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Hashim Kabanda, amesema kuwa zoezi lilikuwa na mafanikio makubwa kwani kila mfanyakazi aliyekuwa anastahili kulipwa amepata haki yake  kama ilivyohakikiwa na jopo la wataalamu hao kwa kushirikiana na wawakilishi wa mkandarasi huyo.

“Tunashukuru kwa kukamilisha zoezi hili kwani haikuwa kazi rahisi kama ambavyo watu wanafikiri, changamoto zilikuwa nyingi zikiambatana na lawama ambazo baadae zilitafutiwa ufumbuzi na hatimaye madai ya wafanyakazi hawa tumeyamaliza leo”, amesema Mhandisi Kabanda.

Aidha, Kabanda ametaja changamoto mbalimbali walizokutana nazo ikiwemo baadhi ya majina kujirudia na mengine kukosewa ambapo awali orodha iliyowasilishwa kwa Kamishna wa kazi ilikuwa na idadi ya wadai 269 na  mara baada ya uhakiki huo idadi ilipungua hadi kufikia 252 ambao kati yao wadai 242 walijitokeza na kulipwa na waliobaki hawakujitokeza.

Sambamba na hilo, wakati zoezi hilo likiendelea liliibuka kundi jingine la wadai ikiwemo walinzi na wafanyakazi wengine ambao walilalamika kuwa nao walipunjwa mishahara yao na kampuni hiyo hali iliyopelekea Mwenyekiti huyo kuwasilisha madaia yao kwa  Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero ili yashughulikiwe kwa taratibu stahiki na hatimaye kupata haki zao. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Ismail Mlawa, amesema kuwa Serikali ipo kwa ajili ya wananchi, hivyo kundi jingine la walinzi ambalo limejitokeza nalo lifuate utaratibu kama waliofanya wenzao ili nao waweze kushughulikiwa madai yao na hatimaye kupata haki zao. 

"Sisi kama Serikali tupo kwa ajili ya wananchi, hakuna kulalamika, mnachotakiwa kufanya ni kufuata maelekezo mnayoambiwa ili msaidiwe kama ambavyo wenzenu wamefanya, na mimi naahidi kuwa sambamba  nanyi ili tujue hatma ya hili”, amesema Mkuu wa Wilaya.

Naye, Mwenyekiti wa wafanyakazi wa ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero Bw.  Alex Ndagaro, ameeleza kuwa mwaka 2013 waligundua kuwa walikuwa wanapunjwa mishahara yao ukilinganisha na viwango vya Serikali vilivyowekwa kwa malipo ya siku hivyo wakaamua kupeleka malalamiko yao Serikalini ili kupata stahili zao.

"Tunashukuru Serikali kwa jitihada zao zote za kukubali kuwasimamia wananchi wake na kwa kumbana mkandarasi alipe madai ya wafanyakazi wake, hii ni Serikali sikivu na ya wanyonge, hakika tunampongeza Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli na timu nzima ya Sekta ya Ujenzi", amesisitiza Mwenyekiti huyo.

Madai ya mapunjo ya mishahara ya wafanyakazi hao yaliibuka mnamo mwezi Mei 2015, baada ya Ofisi ya Kazi Mkoa wa Morogoro kupokea malalamiko ya Wafanyakazi   dhidi ya Mkandarasi huyo kupitia Ofisi ya Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Morogoro.
 Mwenyekiti wa Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Hashim Kabanda, akisisitiza jambo kwa waliokuwa wafanyakazi wa kampuni ya kikandarasi ya China Railway 15 Group, ambao walipunjwa mishahara yao wakati wa ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero (Magufuli), wilayani Kilombero, mkoani Morogoro.
 Mkuu wa Wialaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, Ismail Mlawa akizungumza na waliokuwa wafanyakazi wa kampuni ya kikandarasi ya China Railway 15 Group, ambao walipunjwa mishahara yao alipokuatana nao wilayani humo kwa ajili kuhakiki malipo yao ili wapate stahili zao.
 Waliokuwa wafanyakazi wa kampuni ya kikandarasi ya China Railway 15 Group, ambao walipunjwa mishahara yao wakati wa ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero (Magufuli), wakiwasiliza wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), waliofika wilayani hapo kwa ajili ya kuhakiki malipo ya wafanyakazi hao ili kulipwa stahili zao. 
 Wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), wakiwa na wawakilishi kutoka kampuni ya kikandarasi ya China Railway 15 Group, wakihakiki taarifa za malipo ya waliokuwa wafanyakazi wa kampuni hiyo, wilayani Kilombero mkoani Morogoro.

Wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), wakihakiki majina na malipo ya wafanyakazi ya waliokuwa wakiidai kampuni ya kikandarasi ya China Railway 15 Group, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad