HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 8, 2020

NAIBU WAZIRI WA NISHATI AWAONYA WAKANDARASI WANAOSUSUA


Hafsa Omar-Katavi

Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema Serikali haitasita kusitisha mkataba  wa Mkandarasi yoyote ambae ataonekana kusuasua katika kutekeleza majukumu yake na kwenda kinyume na mkataba waliokubaliana nao.
Ameyasema hayo, Julai 7,2020, wakati alipokuwa akizungumza wa wananchi wa kijiji cha Kenswa Nsimbo, kata ya Katumba,Wilaya ya Mpanda,Mkoani Katavi, kabla ya kuwasha umeme kwenye kijiji hicho.
Naibu Waziri aliyasema hayo,baada ya kutoridhishwa na kasi ya usambazaji umeme na kampuni ya China Railway Construction Electrification Bureau Group Co Ltd( CRCEBG) iliyopewa kazi ya usambazaji umeme  Mkoani humo.
Aidha, alisema  Serikali tayari imesitisha mkataba wa mkandarasi wa mradi wa REA mkoani Mwanza, kwasababu hakuweza kutekeleza majukumu yake kama mkataba unavyoeleza, na kusema kuwa hawatasita kusitisha mkataba wa Mkandarasi wa mkoa huo endapo atashindwa kubadilika katika utendaji wake wa kazi.
“Bado kasi ya mkandarasi haijaturidhisha, kwasasa tumeamua kutengua mikataba kwa wakandarasi wasioendana na kasi yetu, leo tutakaa nao kupitia mpango kazi wao na tutakubaliana kwa mara ya mwisho na mkandarasi huyo,na asipobadilika tutatengua mkataba wake tumpe mwengine,”alisema.
Alifafanua kuwa, wakandarasi wote nchini wanayafahamu vizuri maeneo yao ambayo waliomba kufanyia kazi na nakuzifahamu  changamoto za maeneo hayo, na kuwataka wakandarasi hao kuacha kutoa sababu  kuwa miundombinu inawakwamisha kutekeleza  kazi zao kwa wakati.
Alieleza kuwa, Serikali haipo tayari kurudishwa nyuma katika juhudi zake za usambazaji umeme nchini,ambapo wanatarajia ifikapo mwisho wa mwezi wa Julai jumla ya vijiji 10,446 vitakuwa tayari vimesambaziwa umeme na kuwataka wakandarasi wote wa miradi ya REA kufanya kazi kwa bidii ili kufanikisha lengo hilo.
Hata hivyo, Mgalu aliwatoa wa hofu wananchi wa Mkoa  huo kwa kuwambia kuwa mradi wa REA III mzunguko wa pili ambao unatarajiwa kuanza Septemba mwaka huu kuwa vijiji vyote vya mkoa huo vitapata umeme.
“Naomba kuwahakikishia kuwa Katavi kazi inaendelea na vijiji  vilivyosalia vitaingia kwenye mradi wa REA III mzunguko wa pili ni mradi ambao utaifanya Katavi yote kuwa na umeme kwahiyo naomba mkae mkao wa kupokea mradi huo wa umeme,”alisema Mgalu.
Aliongeza kuwa, Serikali imetenga zaidi ya bilioni mia moja kwaajili ya mradi wa ujazilizi,mradi ambao utapeleka  umeme kwenye vitongoji vyote nchini ambapo tayari mkandarasi ameshapatikana  na mradi huo unatarajiwa kuanza mwezi Agosti mwaka huu.
Aidha, alisema Serikali itaendelea kusambaza umeme kwa kasi kubwa kwasababu inafahamu kuwa mahitaji ya huduma hiyo yanaongezeka siku hadi siku na kwa kasi kubwa na Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa kila mtanzania anapata huduma hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mlele Bi Rachel Kasanda amesema jumla ya vijiji 44 vimeunganishiwa umeme mkoani humo ambapo amesema idadi hiyo ni ndogo kulinganisha na mahitaji ya watu wengi wanaohitaji huduma, na kumtaka mkandarasi kuongeza kasi ya usambazaji wa huduma hiyo.
Pia, ameishukuru Serikali kwa juhudi zake za kuunganisha Mkoa wa Katavi kwenye gridi ya Taifa hatua ambayo itaiondoa Katavi kuondokana na mfumo wa kutumia umeme wa mafuta ambao una gharama kubwa kwenye uendeshaji wake ambapo zaidi ya milioni 21 zinatumika kwa siku moja ambayo sawa na milioni 648 kwa mwezi.
Katika ziara yake hiyo Mkoani humo, Naibu Waziri pia ametembelea kituo cha kupokelea umeme wa gridi ya Taifa kilichopa katika kijiji cha Kampuni na kuwataka wakandarasi wa mradi huo kufanya kazi kasi kubwa ili kumaliza kujenga mradi kwa wakati uliopangwa pia aliwasha umeme katika zahati ya kijiji cha Tambaza Kenswa Nsimbo,Kata ya Katumba, wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu(katikati) akiwasili kwenye mkutano wa hadhara uliyofanyika katika kijiji Kenswa Katumba kilichopo katika kata ya Katumba, Wilaya ya Mpanda, Mkoani Katavi, Julai 7,2020.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akizungumza na wananchi wa  kijiji Kenswa Katumba kilichopo katika kata ya Katumba, Wilaya ya Mpanda, Mkoani Katavi, kabla ya kuwasha umeme kwenye kijiji hicho, Julai 7,2020.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu,(mwenye nguo ya njano) akikata utepe kuashiria kuasha umeme kwenye zahati ya kijiji cha Tambaza Kenswa Nsimbo, kata ya Katumba,wilaya ya Mpanda, Mkoani Katavi,Julai 7,2020, kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mlele Bi Rachel Kasanda.
Wananchi wa kijiji cha Kenswa Katumba kilichopo katika kata ya Katumba, Wilaya ya Mpanda, Mkoani Katavi, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu(hayupo pichani) kabla ya kuwasha umeme kwenye kijiji hicho, Julai 7,2020.



Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu,(mwenye nguo ya njano) akiwa pamoja na viongozi mbalimbali wa mkoani Katavi wakikagua ujenzi wa kituo cha kupokelea umeme wa gridi ya Taifa Mpanda, kilichopo katika kijiji cha Kampuni, wilaya ya Mpanda, Mkoani Katavi, 




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad