Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) Dkt.
Abdul-Razaq Badru (katikati) akizungumza na waandishi wa vyombo vya
Habari kuhusu kufunguliwa kwa dirisha la msimu wa masomo kwa mwaka
2020/21. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano HESLB, Omega Ngole.
TZS 464 bilioni zatengwa kwa wanufaika 145,000
Na Ismail Ngayonga - HESLB (0717 084252),
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo (Jumanne,
Julai 21, 2020) imetangaza kuanza kupokea maombi ya mikopo kwa njia ya
mtandao kwa mwaka wa masomo 2020/2021 kuanzia leo hadi Agosti 31, 2020.
Akizungumza na wanahabari katika ofisi za HESLB zilizopo eneo la
TAZARA jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq
Badru amesema waombaji wote wa mkopo wanashauriwa kusoma na kuuzingatia
‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa 2020-2021’ unaopatikana katika tovuti ya
HESLB (www.heslb.go.tz).
“Mwombaji anaweza kuingia kwenye mfumo wetu kupitia tovuti yetu ambayo ni www.heslb.go.tz na atapata maelekezo ya kutosha ya kuingia katika mfumo wa OLAS – Online Loan Application System,” amesema Badru.
Kuhusu bajeti ya fedha za mikopo, Badru amesema Serikali imetenga TZS
464 bilioni kwa mwaka 2020/2021 ambazo zinatarajia kuwanufaisha jumla
ya wanafunzi 145,000. Kati yao 54,000, watakua ni mwaka wa kwanza na
wengine 91,000 ni wanaoendelea na masomo.
Bajeti ya mikopo kwa 2020-2021
“Bajeti hii ya TZS 464 bilioni kwa 2020/2021 imeongezeka kutoka TZS
450 bilioni mwaka 2019/2020 ambazo zinawanufaisha jumla ya wanafunzi
132,119,” amesema Badru wakati akifafanua swali la mwanahabari aliyetaka
kujua iwapo kuna ongezeko la bajeti.
Katika mkutano huo, Badru pia amezungumzia wanafunzi wahitaji wa
mkopo waliomaliza kidato cha sita na wanatarajia kujiunga kambi za Jeshi
la Kujenga Taifa (JKT) na kusema utaratibu wa kuwafikia unaandaliwa.
“Tunafahamu kuwa kuna wanafunzi waliomaliza kidato cha sita
wanaotarajia kujiunga na kambi 18 za Jeshi la Kujenga Taifa kuanzia
mwezi Agosti, 2020, tunakamilisha utaratibu kwa kushauriana na Makao
Makuu ya JKT ili kuwawezesha kuwezeshwa wakati huo,” amesema.
Malipo ya robo ya nne ya fedha za chakula na malazi
Akitoa ufafanuzi kuhusu malipo ya robo ya nne ya fedha za chakula na
malazi kwa wanafunzi waliopo vyuoni hivi sasa, Badru amesema HESLB
inakamilisha malipo hayo kwa wanafunzi 132,119 ambao wananufaika hivi
sasa.
“Tumeanza kulipa na tunakamilisha malipo hayo ambayo hulipwa kwa
mwanafunzi mnufaika moja kwa moja ili kumuwezesha kumudu gharama za
chakula na malazi katika siku zote anazokuwa chuoni kama tunavyoelezwa
na chuo husika,” amesema Badru na kuongeza:
“Ufafanuzi huu tunautoa kwa kuwa tumepokea maoni kuwa baadhi ya
wateja wetu ambao ni wanafunzi hawajaelewa vizuri utaratibu huu wa
malipo haya na ada za mafunzo ambazo hulipwa mara mbili kwa mwaka,”
amefafanua.
Mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kuomba
Akizungumza katika mkutano huo, Afisa Mikopo Mwandamizi wa HESLB
Josephat Bwathondi amewakumbusha waombaji kuhakikisha wanafuata
maelekezo ikiwemo kutumia namba moja ya kidato cha nne katika kuomba
mkopo na kuomba udahili chuoni.
Kwa mujibu wa Bwathondi, uzoefu wa uchambuzi wa maombi ya mikopo
umeonesha kuwa baadhi ya waombaji hukosea kwa kuambatisha nyaraka
zisizotambulika na hivyo kukosa mkopo na kushindwa kutimiza ndoto zao.
No comments:
Post a Comment