HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 12, 2020

WAZIRI KAREMANI ATOA SIKU 10 KWA EWURA KUPITIA BEI ZA MAFUTA KATIKA MAGHALA

Kamishna wa Maendeleo Petroli wa Wizara ya Nishati, Adam Zuber( kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa pamoja nchini( PBPA) erasto samwel( katikati) walimsikiliza Waziri wa Nishari, Dkt. Medard Kalemani,( hayupo pichani) akizungumza baada ya kufanya ziara katika ghala ya kuhifadhi na Kupokea mafuta Kampuni ya GBP mkoani Tanga, Mei 10,2020.
 Waziri wa Nishari, Dkt. Medard Kalemani (wa pili kulia mbele) akipita kukagua mazingira ya ghala la kuhifadhi na kupokea mafuta la kampuni ya GBP, alipofanya ziara katika eneo hilo mkoani Tanga, Mei 10, 2020.
 Baadhi ya mapipa makubwa ya kuhifadhia mafuta katika ghala la kuhifadhi na kupokea mafuta la kampuni ya GBP mkoani Tanga, Waziri wa Nishari, Dkt. Medard Kalemani, alifanya ziara katika eneo hilo, Mei 10, 2020.
 Muonekano wa eneo kitakapojengwa kifaa cha kupimia mafuta (Flow Meter) kutoka katika meli hadi katika maghala ya kuhifadhi na kupokea mafuta katika bandari ya Tanga, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, alifanya ziara katika eneo hilo, Mei 10, 2020.
Waziri wa Nishari, Dkt. Medard Kalemani, (katikati) akiwasha umeme katika moja ya Ofisi za Serikali ya Kijiji katika Kijiji cha Mbuyuni Kata ya Mapatano wilayani Mkinga, mkoani Tanga, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini katika wilaya hiyo, Mei 10, 2020.

Na Zuena Msuya Tanga,
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, ametoa siku kumi kwa Mamlaka ya Udhibiti huduma za Nishati na Maji (EWURA) kumpatia majibu ya uwiano wa viwango vya bei ya mafuta katika maghala ya Kupokea na kuhifadhia mafuta nchini.


Dkt. Kalemani alisema hayo alipofanya ziara ya kutembelea ghala la kuhifadhia mafuta la kampuni ya GBP iliyoko mkoani Tanga, Mei 10, 2020, ili kuona kama agizo lake alilolitoa mwezi Machi, 2020, la kuwataka waagizaji mafuta nchini wanaagiza shehena kubwa kutokana na tishio la kuwepo kwa virusi vya Corona.
Pia alifanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini katika wilaya ya Mkinga na Muheza mkoani huo pamoja na kuwasha umeme.
Baada ya kupata taarifa ya mwenendo wa uingizaji,upokeaji na uhifadhi wa mafuta nchini katika maghala pamoja na mambo mengine, Dkt.Kalemani aliiagiza EWURA kufanya tathmini ya bei ya mafuta katika maghala hayo kwa lengo la kuboresha biashara ya mafuta kwa maslahi ya watumiaji na wafanyabiashara.
Dkt.Kalimani alisema kuwa, serikali imeweka utaratibu wa kuweka maghala ya kupokea na kuhifadhi mafuta katika kila ukanda wa nchi kwa lengo la kuwapunguzia gharama za usafiri wafanyabiashara wa mafuta wanaotembea umbali mrefu kuyafuata mafuta hayo, pia kuwezesha watumiaji kupata huduma hiyo kwa haraka, karibu na kwa bei nafuu wakati wote.
Sambamba na hilo kulinda ubora wa miundombinu ya barabara nchini kwa kuwa magari yanayobeba mizigo mizito ikiwemo mafuta yamekuwa yakichangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa barabara.
“EWURA na PBPA nawapa siku 10,muangalieni uwiano na uratibu sahihi wa bei ya mafuta katika maghala ili bei hizo zisitofautiane sana na taratibu za bei zilizowekwa, kwa kuwa mafuta yapo mengi nayakutosha, na mniletee majibu, Lengo la serikali ni kuhakikisha mafuta yanapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu wakati wote kwa kuwanufaisha wafanyabiashara na watumiaji”, alisema Dkt. Kalemani.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara wa mafuta kwa kanda ya kaskazini ikiwemo Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro,Manyara na Tanga kutumia ghala la kuhifadhi na kupokea mafuta lililopo mkoani Tanga kuliko kuyafuata mkoani Dar Es Salaam.
“Wafanyabiashara wanaofuata mafuta Dar es salam watalazimika kuuza kuwauzia watumiaji kwa bei ya juu hivyo kuwakandamiza watumiaji hii si sahihi na ndiyo maana karibu kila ukanda wa nchi tumeweka ghala la kuhifadhi na kupokea mafuta,tofauti na ilivyokuwa awali mafuta yote yalikuwa yakipatikana mkoani Dar Es Salaam pekee”,alisisitiza Dkt. Kalemani
Alitoa wito kwa makampuni yote ya uwagizaji wa mafuta nchini kwa kushirikiana na EWURA na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja (PBPA)kushirikiana kwa pamoja kuendelea kuleta mafuta mara dufu ili kujihakikishia uwepo wa mafuta nchini hata kama ugonjwa wa corona utaendelea kuwepo.
Dkt. Kalemani alifafanua kuwa mafuta yaliyopo nchini kwa sasa yanauwezo wa kutumika zaidi ya miezi miwili hadi mitatu mbele na bado kila siku wanapokea mafuta, ambapo kwa sasa nchi inapokea inapokea mafuta lita milioni 428.7 tofauti na awali kabla ya agizo kutoka ilikuwa ikipokea mafuta lita milioni 185.
Aidha aliwataka wafanyabiashara ya mafuta kujenga vituo vya mafuta katika maeneo yaliyo vijijini ili kulinda ubora wa mafuta na kusogeza huduma karibu na watumiaji hasa wadogo akitolea mfano waendesha pikipiki ambao ndiyo wanaotegemeo kubwa la usafiri katika maeneo ya vijijini.
Alisema kuwa watumiaji wadogo wa vyombo vya moto, wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kutafuta huduma ya mafuta, na wengine wamekuwa wakihifadhi mafuta katika nyumba zao jambo ambalo linahatarisha usalama wao.
Aidha alisema kuwa pia kumekuwa na tabia ya kuuza kiholela mafuta na uhifadhi mbovu wa mafuta hayo na hivyo kupunuza ubora waviwango vya mafuata kwa watumiaji na hivyo hata kulazimu mafuta hayo kuchanganywa na hivyo kuchangi uharibifu wa yyombo vinavyotumia mafuta hayo.
“Wafanyabiashara nendeni mkajenge vituo vidogo vya mafuta vijijini, mrahisishe huduma ya upatikanaji wa mafuta na bei nafuu kwa watumiaji wadogo ambao wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo,tuungane kutekeleza lengo la serikali la kuhakikisha kila mtumiaji wa mafuta anapata bishaa hiyo kwa wakati na kwa bei nafuu”, alisisitiza Dkt. Kalemani.
Pamoja na mambo mengine alitembelea eneo inapojengwa kifaa kitakachotumika kupima mafuta (Flow Meter), yanayoingia nchini kutoka katika Meli kwenda katika maghala ya kuhifadhi na kupokea mafuta  katika Bandari ya Tanga.
Aliiagiza mamlaka ya bandari nchini kukamilisha ujenzi wa mtambo huo haraka ili serikali ipate kiwango sahihi cha mafuta yanayoingia nchini kupitia Bandari ya Tanga ili kupata kodi na tozo stahiki.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Uagizaji mafuta ya GBP, Badar Seif Sood alimueleza Waziri wa Nishati kuwa wamefanya upanuzi wa bandari hiyo, hivyo kwa sasa inauwezo wa kuhifadhi na kupokea mafuta lita milioni 182, tofauti na walivyokuwa wananza mwaka 2017 walipokuwa wakihifadhi na kupokea mafuta lita milioni 182, na upanuzi utaendelea kulingana na mahitaji.
Aliishukuru serikali kupitia wizara ya nishati, kuendelea kuwalinda wafanyabiashata wa mafuta wakiwamo wamiliki wa maghala ya kuhifadhi na kupokea mafuta pamoja na waagizaji wakubwa wa mafuta kwa kuhakikisha wanafanya biashara zao katika mazingira rafiki: Huku akiahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa watumiaji wa mafuta hayo nchini. 
Katika ziara hiyo, Dkt. Kalemani, pia alikagua maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini katika Wilaya ya Mkinga na kuwasha umeme katika kijiji cha Mbuyuni kata ya Mapatano na kutembelea kisima cha maji katika kijiji cha Jihirini na kuliagiza Shirika la Umeme nchini (TANESCO), kupeleka na kuwasha umeme katika kisima hicho mwishoni mwa mwezi huu.

Vilevile alitembelea Wilaya ya Muheza na kukagua kazi ya usambazaji wa umeme katika kijiji cha Kwakokwe na kuwataka wananchi kuendelea kulipia gharama za kuunganishiwa umeme kwa kuwa vijijini vyote nchini vitapata umeme na kwamba wasikubali kuuziwa miundombinu ya umeme na pia watumie wakadarasi wanaotambulika na TANESCO katika kutandaza nyaya katika nyumba zao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad