HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, May 28, 2020

Benki ya NMB na SatF zazindua utoaji wa huduma za kidijitali kwa vikundi vya kuweka na kukopa

Benki ya NMB na kampuni ya Savings at the Frontier (SatF) leo wamezindua huduma mahsusi kwa vikundi vya kuweka na kukopa nchini. Kwa ushirikiano huo, NMB na SatF zinakusudia kuwafikia zaidi ya vikundi 28,000 na wanachama wake walio nje ya mfumo rasmi na kuwaunganisha kwenye huduma za kifedha. 

Mfumo huo mpya utatoa nafasi kwa vikundi vya kuweka na kukopa pamoja na wanachama wao kutumia huduma za kidijitali za NMB zitakazowawezesha kufungua akaunti binafsi, kufungua akaunti za vikundi na kuweza kuzihudumia kupitia simu ya mkononi. Njia hii itawafanya wakidhi mahitaji ya wanachama bila kulazimika kukutana au kwenda tawi la benki na hivyo kutunza fedha kwa njia salama na ya uhakika. 

Mfumo huu ni maboresho ya huduma ya ‘NMB Pamoja Account’ ambayo ni mahsusi kwa ajili ya Vyama vya Kuweka na Kukopa Vijijini (VSLA), Vyama vya Kijamii vya Akiba (SILC), Benki za Kijamii Vijijini (VICOBA), Vikundi vya Kijamii vya Akiba (CBSG), Mashirika ya Kijamii (CBO), Makundi ya Familia na Marafiki na kuyaunganisha na benki yenye mtandao mpana zaidi nchini. 

Akizungumza kwenye uzinduzi wa NMB Pamoja Account, Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya NMB – Ruth Zaipuna alisema: “Lengo letu ni kuziba pengo lililopo kati ya taasisi za fedha na makundi yasiyo rasmi ya kuweka akiba na kukopa kwa kuyasogezea huduma za kibenki karibu yao. Huduma hii ambayo ni nyongeza kwenye NMB Pamoja Account, ni nafuu, inapatikana kila mahali na wakati wowote na ni rahisi kuitumia.” 

Katika kuimarisha mkakati wa Benki ya NMB kufikisha huduma za kifedha kwa wananchi, NMB Pamoja Account ni huduma kamili iliyounganishwa na Akaunti ya Chapchap inayowaruhusu wanachama wa kikundi kuhamisha fedha kutoka akaunti ya chama kwenda kwa mwanachama bila gharama yoyote, huku ikitoa urahisi na uwezo wa kutoa michango, kuangalia salio, kupata taarifa fupi na kufungua akaunti ya kikundi kwa kutumia simu ya mkononi, kwa kupiga *150*68# bila makato yoyote ya gharama za uendeshaji ya kila mwezi, haya yote yakiambatana na riba nzuri inayotolewa kwenye akaunti kwa mwaka. 

“SatF inafurahi kuungana na Benki ya NMB ili kutoa suluhu ya huduma za kifedha kwa vikundi. Tunaamini ushirikiano huu utasaidia kuvifikia vikundi yenye wanachama walio nje ya mfumo rasmi kwenye huduma za kifedha nchini. Hii inaenda sambamba na mpango wa Benki Kuu ya Tanzania kuongeza idadi ya wananchi wanaotumia huduma za kifedha hususan kwa wanawake,” alisema Mwakilishi kutoka SatF, Janet Hayes 

Ushirikiano wa Benki ya NMB na kampuni ya SatF utaongeza kasi ya ufikishaji wa huduma za kifedha kwa wananchi. Ni ushirikiano unaokusudia kuhamasisha na kuongeza uwekezaji na ushiriki wa wadau wengine katika sekta ya huduma za fedha. Wakati Benki ya NMB ikiongoza kwa huduma bora, zilizo karibu na wananchi na zenye tija zaidi nchini, SatF inakuja na uzoefu wa kimataifa wa kujenga misingi ya kuboresha uwakilishwaji wa wananchi walio nje ya mifumo rasmi ya kifedha ili kukuza uchumi na kupunguza umasikini. 

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB – Ruth Zaipuna (kushoto) na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara Ndogo na za Kati wa NMB - Filbert Mponzi (Kulia) wakiwa wameshika alama ya uzinduzi rasmi wa akaunti ya NMB Pamoja. Katikati ni Mteja wa NMB Bi. Zaina Mikidadi, kutoka kushoto ni Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB - Benedicto Baragomwa, Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa wa Serikali wa NMB Alfred Shao na Kaimu Afisa Mkuu Rasilimali watu- Emmanuel Akonaay.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad