TMA yatolea ufafanuzi juu ya taharuki ya hali ya anga kuwa na Rangi mbili - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, April 17, 2020

TMA yatolea ufafanuzi juu ya taharuki ya hali ya anga kuwa na Rangi mbili

Na Karama Kenyunko globu ya jamii. 
KUFUATIA kuwepo kwa taharuki na maswali kutoka kwa Umma juu ya muonekano wa anga kuwa na rangi nyekundu au ya chungwa jana Aprili 16,2020 katika baadhi ya maeneo nchini, Mamlaka ya Hali ya hewa nchini TMA imetolea ufafanuzi hali hiyo na kusema kuwa ni hali ya kawaida kutokea.
Katika taarifa yake iliyotolewa leo Aprili 17, 2020 imeeleza kuwa, hali hiyo hutokea wakati jua linapozama au kuchomoza katika mazingira yenye kuwa na hali ya hewa kama vile mawingu, matone madogo madogo ya maji na barafu katika anga mara mvua inapokatika na jua linapokuwa katika upande tofauti na eneo mvua inaponyesha. 
Taarifa hiyo imeeleza kuwa hali  hiyo husababisha kutawanywa kwa miale ya mwanga wa jua na hivyo kutokana na ukubwa wa matone ya maji katika wingu na chembechembe za vumbi katika anga, sehemu ya miale ya jua inayotawanywa zaidi katika mazingira hayo ni mawimbi ya miale ya jua inayohusiana na rangi nyekundu au chungwa na hivyo kufanya anga kuonekana katika rangi hizo ambapo Mawimbi madogo sana 
huwakilisha rangi ya blue na makubwa rangi nyekundu au rangi ya chungwa. 
Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa, hali hiyo haina tofauti sana na namna Upinde Mvua unavyojitokeza angani, isipokuwa upinde wa mvua unakuwa na rangi zote saba za spectrum ya mwanga mabadiliko ambayo hayana madhara yoyote kwa anga.
"Katika hali iliyozoeleka mara nyingi, anga huonekana kuwa rangi ya bluu kutokana na kutawanywa kwa mawimbi ya miale ya jua kunakofanywa na gesi ya Nitrojeni na Oksijeni ambazo ndizo hufanya sehemu kubwa ya gesi katika hewa...., hali hiyo inatokana na molekuli za gesi hizo kuwa ni ndogo sana hivyo hutawanya sehemu ya mawimbi madogo zaidi ya miale ya jua iliyo katika rangi 
ya blue na katika spectrum ya mwanga Rangi ambayo huonekana katika macho ya binadamu kwa kipindi hicho" imeeleza taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad